STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 02 Januari, 2014
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema Zanzibar iko tayari kushirikiana na Shirikisho la Vyama vya Michezo ya Karate ulimwenguni ili kukuza vipaji wa vijana na kuimarisha michezo ya karate nchini.
Katika kufanya hivyo Dk. Shein amebainisha kuwa Zanzibar ingependa kuona ushirikiano huo unazingatia kuanzishwa kwa skuli maalum(academy) za michezo hiyo katika visiwa vya Unguja na Pemba ili kutoa fursa kwa vijana wenye vipaji kuimarisha na kuendeleza vipaji vyao hadi kufikia viwango bora zaidi vya ushindani wa kimataifa.
Dk. Shein ametoa kauli hiyo leo wakati akizungumza na Rais wa Shirikisho la Vyama vya Michezo ya Karate Ulimwenguni Bwana Antonio Espinos aliyemtembelea Ofisini kwake Ikulu.
Alimueleza Bwana Antonio kuwa Zanzibar imejaaliwa na vijana wengi wenye vya kila aina ya michezo ikiwemo hiyo ya karate lakini wanahitaji kuhamasishwa zaidi kuupenda mchezo huo ambapo njia mojawapo ni kuanzisha skuli hizo maalum kwa michezo hiyo.
Kwa hiyo amemuhakikishia Rais huyo wa Shirikisho la Vyama vya Michezo ya Karate Ulimwenguni kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iko tayari kushirikiana na shirikisho hilo na kwamba inasubiri kutoka kwake maelezo ya namna bora ya kutekeleza mpango wa uanzishwaji wa skuli hizo.
Katika hatua nyingine Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amemwambia bwana Antonio kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar iko tayari kushirikiana na wadau wengine katika kuipatia Zanzibar nishati mbadala.
Akijibu rai ya Bwana Antonio ambaye alisema ana mpango wa kusaidia wananchi masikini nchini kupata nishati ya umeme jua kwa matumizi ya majumbani Dk. Shein amesema anaafiki rai hiyo kwa kuwa inakwenda sambamba na lengo la Serikali la kuipatia Zanzibar njia mbadala za nishati.
Katika maelezo yake kwa Mheshimiwa Rais Bwana Antonio alieleza kuwa chini ya mpango huo mwananchi atapatiwa mashine ya umeme jua yenye uwezo wa kutoa nishati ya kilovolti 6 inayotosha kwa matumzi ya nyumbani.
Kuhusu michezo ya karate Rais huyo wa Shirikisho la Vyama vya Michezo ya Karate Ulimwenguni alimemueleza Mheshimiwa Rais kuwa katika ziara yake humu nchini ameshududia vijana wakionesha vipaji vya hali ya juu katika mchezo huo.
Kutokana na hali hiyo alisema ipo haja ya shirikisho lake kuanzisha ushirikiano wa karibu na makini utakaoiwezesha Zanzibar kukuza vipaji vya vijana katika mchezo huo ili Zanzibar iweze kupata mafanikio zaidi katika mashindano ya kimataifa.
Katika mazungumzo hayo walikuwepo pia Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Said Ali Mbarouk na Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo Zanzibar Bi Sharifa Khamis.