Askari wa kikosi cha zimamoto na uokozi Zanzibar, akitoa maelezo kwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, alipotembelea banda la kikosi hicho kwenye maonyesho ya miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar huko Beit-el-Raas
Mkuu wa Taaluma wa Chuo cha Uandishi wa Habari Zanzibar Rashid Omar, akitoa maelezo kwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, alipotembelea banda la chuo hicho kwenye maonyesho ya miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar huko Beit-el-Raas.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad akiangalia bidhaa za wajasiriamali, alipotembelea mabanda ya maonyesho ya miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar huko Beit-el-Raas.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akiwa kwenye banda la Ofisi ya Makamu wa Rais, kuangalia huduma za Ofisi hiyo, alipotembelea mabanda ya maonyesho ya miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar huko Beit-el-Raas. (Picha na Salmin Said, OMKR)
Na Hassan Hamad, OMKR
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Sharif Hamad, amesema serikali imepata moyo kuona taasisi, mashirika na wananchi jinsi walivyojitokeza katika maonyesho ya miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Amesema kujitokeza kwao kwa wingi kunaashiria jinsi wananchi walivyohamasika kuonyesha na kutangaza huduma zao kwa wengine, kwa lengo la kuzitambulisha na kutafuta soko ndani na nje ya nchi.
Mhe. Maalim Seif ameeleza hayo baada ya kutembelea mabanda ya maonyesho ya miaka 50 ya Mapinduzi yaliyoko Beit- el- Raas, mjini Zanzibar.
Amesema wananchi wameonesha kuyapenda maonyesho hayo ya bidhaa na huduma, na kwamba ni vyema yakaandaliwa kila baada ya muda, bila ya kusubiri miaka 50 mengine.
Maonyesho hayo ya kwanza ya aina yake kufanyika Zanzibar, yamekuwa kivutio kikubwa kwa wenyeji na wageni, yanazishirikisha taasisi mbali mbali zikiwemo taasisi binafsi, mashirika ya umma na wajasiriamali.
Katika ziara hiyo Mhe. Maalim Seif ametembelea mabanda ya maonyesho kwa taasisi tofauti zikiwemo Jumuiya ya Wafanyabiashara, Chuo Cha usimamizi wa fedha, mafunzo ya amali, polisi na vikosi vya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.