Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiweka jiwe la msingi la jengo la michezo ya ndani liliopo pembezoni mwa uwanja wa michezo wa Gombani Chake Chake Kisiwani Pemba ikiwa ni shamra shamra za maadhimisho ya kutimia miaka 50 ya mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964
Balozi Seif akifuatilia muendelezo wa ujenzi wa jengo la Michezo ya ndani chakc chake Pemba wakati alipolikagua mara baada ya kuliwekea jiwe la msingi.
Kulia ya Balozi ni Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Said Ali Mbarouk na Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba Dadi Faki Dadi, na kushoto yake ni Rais wa Heshima wa chama cha mchezo wa Judo Zanzibar Tuyoshi Shimaoka na Balozi wa Japan Nchini Tanzania Masaki Okada.
Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ.
Na Othman Khamis Ame, OMPR
Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo imeombwa kuzidi kuimarisha michezo ya ndani angalau kwa kuanzia michezo mitatu katika kila Wilaya za Zanzibar ili kunyanyua viwango vya michezo hiyo katika maeneo mbali mbali hapa Nchini.
Ombi hilo limetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wakati akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa jengo la Michezo ya ndani liliopo pembezoni mwa uwanja wa Michezo wa Gombani Chake chake Kisiwani Pemba.
Balozi Seif alisema michezo ya ndani kwa kiasi kikubwa iliwahi kuipa sifa kubwa Zanzibar Kimataifa licha ya michezo hiyo kukosa maeneo halisi ya kuendeleza pamoja na kufanyia mazoezi michezo hiyo.
Akitilia mkazo haja ya kuanzishwa pia kwa kampeni maalum ya kuendeleza mchezo wa judo vijijini ili uwasaidie wadau wa mchezo huo kuongeza juhudi za heshima miongoni mwa washiriki wa mchezo huo.
Alisema mchezo huo kwa kiasi kikubwa pia unasaidia mbinu za kujikinga wakati mtu anapotaka kudhuriwa.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameishukuru Serikali ya Japani kupitia Ubalozi wake Nchini Tanzania na mradi wa mfuko wa GGHSP wan chi hiyo ambao umefadhili ujenzi wa uwanja na jengo hilo.
Akitoa taarifa za ujenzi wa jengo hilo la michezo ya ndani Afisa mdhamini Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Ali Nassor alisema ujenzi wa jengo hilo ulioanza tarehe 19 Agosti mwaka 2013 ulitarajiwa kukamilika ndani ya kipindi hichi cha sherehe za mapinduzi ya Zanzibar.
Ali Nassor alisema uchelewaji wa jengo hilo litakalohimili michezo ya Judo, Karati, Badminton, basketball, na hata table tennis umesababishwa na kuwepo kwa upepo mkali zilizoambatana na mvua.
Afisa mdhamini huyo wa Wizara ya Habari, Utamduni, Utalii na Michezo Pemba aliwaomba wafadhili mbali mbali wa Sekta ya michezo kuendelea kuwekeza kwenye sekta hiyo kisiwani Pemba kwa vile Wizara hiyo bado ina eneo kubwa linaloweza kukidhi mahitaji ya uwekezaji.
“ Hili eneo lililotuzunguuka ni la Wizara ya Habari lililotengwa kwa ajili ya michezo mbali mbali hivyo wawekezaji tofauti wanaruhusiwa kulitumia kwa kuanzisha michezo mbali mbali “. Alisisitiza Afisa mdhamini huyo wa sekta ya Habari.
Akitoa salamu zake Balozi wa Japan Nchini Tanzania Bwana Masaki Okada aliipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuendeleza ushirikiano wake na nchi yake.
Balozi Masaki alisema kutokana na ushirikiano huo Serikali ya Japani itaendelea kuiunga mkono Zanzibar katika miradi yake mbali mbali ya kiuchumi na ustawi wa jamii ikiwemo sekta muhimu ya michezo.
Alitolea mfano wa ushirikiano huo kuwa ni pamoja na wajasiri amali wa Kisiwa cha Pemba kupata fursa ya kuuza bidhaa wanazozizalisha za urembo moja kwa moja utaratibu ulioanza mwezi uliopita wa Disemba mwaka 2013.
Akimkaribisha mgeni rasmi Balozi Seif kwenye uwekaji wa jiwe la msingi la jengo hilo la michezo ya ndani Gombani Pemba, Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Said Ali Mbarouk alisema michezo ya ndani muda mrefu ilikuwa katika mitihani mikubwa ya kukosa maeneo maalum.
Waziri Mbarouk alisema ujenzi wa jengo hilo la michezo ya ndani utatoa fursa nzuri kwa wanamichezo wa Zanzibar kupata muda muwafaka wa kushiriki vyema michezo hiyo kimataifa na kuirejeshea Heshima yake kwenye fani hiyo.
“ Tumepata faraja na kuamini kwamba jengo letu hili litasaidia kuondoa kiu ya wanamichezo ya kukosa maeneo ya kuendeleza michezo yao ya ndani “. Alifafanua Waziri Mbarouk.
Jengo hilo la michezo ya ndani linaloendelea kujengwa pembezoni mwa uwanja wa Michezo wa Gombani Chake chake Pemba linatarajiwa kugharimu jumla ya shilingi Mia Nne na themanini Milioni litakapokamilika.