Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Makazi, Maji na Nishati Nd. Ali Khalil Mirza Kushoto na Mwenzake wa Wizara ya Kilimo na Maliasili Nd. Afan Othman Maalim wakikabidhiana ahati za usimamizi wa Mashamba ya Serikali ambayo yalikuwa chini ya usimamizi wa Wizara ya Ardhi.
Nyuma yao ni Mkuu wa Wilaya ya Chake chake Bibi Mwanajuma Majid.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akimkabidhi nyaraka za Mashamba ya Serikali Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo na Maliasili Zanzibar Ndu. Afan Othman Maalim hafla iliyofanyika katika ukumbi wa Tasaf Ofisi ya Makamu Pili wa Rais wa Zanzibar Chake Chake Pemba.
Walioshuhudia kati kati yao ni Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba Mh. Dadi Faki Dadi na Mkuu wa wilaya ya Chake chake Bibi Mwanajuma Majid.
Picha na Hassan Issa OMPR
Na Othman Khamis Ame
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imefikia uamuzi wa Mashamba yote ya Serikali yaliyokuwa chini ya usimamizi na uangalizi wa Wizara ya Ardhi, Makazi, Maji na Nishati kuanzia sasa yatasimamiwa na Wizara ya Kilimo na Mali asili Zanzibar.
Hatua hiyo imekuja baada ya Serikali kuzingatia kwa kina kwamba Wizara ya Kilimo na Maliasili ndio yenye dhamana ya kusimamia uhuishaji wa miti hasa mikarafuu na minazi ambayo ndio inayoonekana kusheheni zaidi katika mashamba hayo.
Hati za makabidhiano ya usimamizi wa mashamba hayo ya Serikali zilifanyika katika ukumbi wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania { Tasaf } wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar uliopo Chake chake Kisiwani Pemba na kushirikisha pia watendaji wa Wizara zote mbili.
Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Makazi, Maji na Nishati Nd. Ali Khalil Mirza alimkabidhi hati hizo Katibu Mkuu mwenzake wa Wizara ya Kilimo na Maliasili Nd. Afan Othman Maalim tukio ambalo lilishuhudiwa pia na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi.
Akikabidhi hati hizo Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Makazi, Maji na Nishati Nd. Ali Khalil Mirza alisema Wizara hiyo ilikuwa ikidhibiti mashamba 111 ya Eka Tatu Tatu Unguja na Pemba kuanzia mwaka 1989 ambayo wananchi waliokuwa wakiyatumia kwa shughuli zao za Kilimo kwa sasa wamefariki Dunia.
Nd. Mirza alisema hati hizo zilizomo kwenye madaftari Manne zinaonyesha rikodi zote za uwepo wa mashamba 8,215 ya eka tatu tatu Zanzibar ambazo kwa mujibu wa sera za mabadiliko ya ardhi zilikuwa chini ya iliyokuwa Kamisheni ya Ardhi na Mazin gira tokea mwaka 1989.
Akipokea Madaftari hayo yenye hati za kumbu kumbu za mashamba hayo ya Serikali Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo na Mali asili Nd. Afan Othman Maalim aliwaomba watendaji wa Wizara ya Ardhi kuendelea kutoa ushirikiano wa utambuzi wa
Mashamba hayo kwa lengo la kulinda Mali za Serikali.
Nd. Afan alifahamisha kwamba kutokana na umuhimu uliojitokeza hivi sasa wa matumizi makubwa ya mashamba unaotokana na mabadiliko ya Dunia bila shaka zinaweza kujitokeza hitilafu na changamoto zitakazohitaji kutatuliwa kwa pamoja kati ya taasisi hizo.
Mapema Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Baraza lake la Mapinduzi iliamua kuunda kamati Maalum kujaribu kufuatilia kasoro zilizomo za matumizi mabaya ndani ya mashamba yote ya Serikali.
Balozi Seif alifahamisha kwamba ripoti ya Kamati hiyo ilithibitisha kwamba mengi ya mashamba ya Serikali hasa yale yaliyokuwa yalisimamiwa na Wizara ya Ardhi, Makazi, maji na Nishati yalikosa usimamizi mzuri.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alitolea mfano Mashamba mengi ya mikarafuu hasa Kisiwani Pemba kwa kipindi kirefu yalikosa huduma inayostahili na kusababisha upungufu wa uzalishaji wa zao la Karafuu.