Na Salim Said Salim
RAIS wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, hivi karibuni amezungumzia umuhimu wa kuitambua historia na kuweka kumbukumbu zake vizuri ili kizazi kijacho kielewe Zanzibar ilipotoka na inapoelekea.
Dk. Shein ambaye alikuwa akizungumza wakati wa kufungua maonyesho ya biashara ya maadhimisho ya miaka 50 ya Mapinduzi amesikitishwa kuona hakuna kumbukumbu za kutosha zinazotoa picha halisi ya visiwa hivi.
Kwa hakika alichosema Rais Shein ni sawa kwa sababu nchi isiyohifadhi historia yake huwa kama mtoto yatima.
Lakini ukichunguza utaona wanaohusika na kuifanya kazi hii hawataki kufanya hivyo kwa sababu wanazozijua wao au uelewa wao wa historia ya visiwa hivi ni mdogo.
Hata hivyo, wamepewa kazi ya kuhusika na masuala haya si kutokana na uwezo wao, bali kwa vile ni watoto wa ‘ wenzetu’.
Nilipotembelea vibanda vya maonyesho nilichogundua ni upungufu mkubwa na kumesababisha niamini walikataa kujituma au upeo wao wa kuielewa Zanzibar ni mdogo.
Jingine ni tatizo la Zanzibar kuyakataa baadhi ya matokeo ya kihistoria na wana historia kwa kuzua mambo yasiyokuwa na kichwa wala miguu ili kukidhi utashi wa kisiasa.
Watu wanayajua mengi kuhusu Zanzibar ilipotoka, zipo kumbukumbu zake na maelezo sahihi ya masuala haya wapo (kikapu tele), lakini hawatumiwi. Badala yake hutafutwa wale waliokuja
Zanzibar miaka ya karibuni katika safari za mbio za Mwenge.
Kwa mfano, tuanzie na Ikulu, Ofisi ya Rais Shein. Katika sehemu hii palihitajika kufanyika kazi ya ziada ili kuonyesha sura halisi ya kihistoria ya jengo hili na ofisi hii.
Ungelitarajia kuwepo maelezo ya jumba hili linalovutia lilijengwa lini, lilitumiwa na nani wakati wa ukoloni na hata kuweka picha za Malikia wa Uingereza waliokuwa wanaishi na kufanya kazi katika jumba hilo.
Mambo ya kihistoria kama stempu ya kwanza ya Zanzibar, sarafu zilizotumika, picha za walimu na madaktari wa miaka ya nyuma na mambo mengi kama maelezo ya kuwepo kwa matumizi ya gari moshi mjini Unguja yangelipatiwa maelezo.
Watu wanasikia tu habari za majumba kama Mambo Msige, Beit el Ajaib, Nyumba ya Sukari na majengo mengine. Yote haya yana historia yake na pangelikuwepo maelezo ya kutosha juu ya majengo haya ambayo hii leo yamekuwa urithi mkubwa wa kihistoria wa Zanzibar.
Zanzibar ilitawaliwa na masultani mbalimbali wenye asili ya Oman. Haya nayo yangeonyeshwa, pamoja na picha za hao wafalme na maelezo mafupi ya yaliyofanyika wakati wa utawala wao.
Hii ni sehemu mhimu ya historia na inayo uhusiano mkubwa na kufanyika kwa mapinduzi miaka 50 iliyopita. Yote haya hayakuwepo.
Katika maonyesho haya watu wangelielezwa lini Zanzibar ilipata maji safi ya bomba, gari la kwanza lilikuja lini, simu na huduma nyingine muhimu kwa mara ya kwanza zilipatikana lini na kuwekwa picha za matukio haya ya kihistoria pamoja na mambo ya siasa, kijamii na kiutamaduni.
Kwa muda mrefu pamekuwepo na propaganda ya kupotosha historia, jambo ambalo limechochea kujenga chuki na uhasama uliokuwa ukishuhudiwa Visiwani katika miaka mingi sasa tokea kufanyika Mapinduzi mwaka 1964.
Kwa mfano watu huelezwa kuwa hapo zamani kina mama walikuwa wakifagilishwa njia masafa marefu kwa matiti. Jamani titi gani hilo linaweza kufagia njia. Au Waznzibari wa zamani walikuwa na matiti ya chuma?
Vijana wa leo wamekuwa wakielezwa unafiki ya kwamba hapo zamani waliokuwa wanapata nafasi za kusoma walikuwa ni Wahindi na Waarabu.
Hili si sahihi kwani Zanzibar imepata wataalamu wa fani mbali wa makabila tofauti miaka mingi kabla ya Mapinduzi. Ili kusahihisha upototoshaji huu pangekuwepo picha za wasomi wa zamani ambao wengi wao walikuwa Waswahili waliopata shahada mbalimbali nje ya nchi na kuwa wataalamu na mabingwa wa fani mbalimbali miaka 30 na zaidi kabla ya Mapinduzi ya 1964.
Baadhi ya wataalamu hawa walikuwa viongozi waliopita wa Zanzibar, kama marais wa zamani, Sheikh Aboud Jumbe Mwinyi, Sheikh Ali Hassan Mwinyi na marehemu Sheikh Idris Abdulwakil. Wote hawa walipata elimu ya juu katika miaka ya 1940 na mwanzoni mwa 1950.
Mfano mwingine ni banda la Idara ya Utamaduni. Katika banda hili zipo picha zisizozidi 20 za mchezo wa tenisi ya meza zilizobandikwa katika sehemu hiyo, lakini zote ni za miaka ya 1970 na kuendelea mbele.
Kama juhudi zingefanywa zingelipatikana picha za wanamichezo maarufu wa miaka ya 1930 na 1940 na hata kabla ya hapo.
Zanzibar ilikuwa maarufu kwa michezo mingi, kama kriketi, mpira wa magongo, lakini hapana maelezo yoyote yale kuhusu michezo hii.
Visiwa vya Unguja na Pemba ni eneo pekee katika Afrika ya Mashariki lililokuwa na wacheza gofu Waswahili (Waafrika) katika miaka zaidi ya 60 iliyopita na hili nalo lingeelezwa.
Baadhi ya michezo iliyokuwa ikichezwa Zanzibar zamani, kama kipande, kurusha vishada na vikundi vya watoto waliokuwa wakiamsha daku waliojulikana kama ‘Ngongoriko’, lakini sasa yote haya yametoweka na kizazi cha leo hakijui chochote juu ya masuala haya.
Hata mavazi ya kanzu, kofia ya bul bul na viatu vya makubadhi na mataraanda (viatu vya mbao) pamoja na matumizi ya uturi wa asili wa watu wa Visiwani wa viluwa na asumini, haukupewa nafasi katika maonyesho haya.
Siwalaumu watayarishaji kwa vile wengi wao hawayajui haya na elimu waliyopata ilikuwa ya upotoshaji ukweli.
Wazanzibari walikuwa na vyakula vyao vya asili vilivyokuwa na faida kubwa mwilini, kama manda, ambavyo siku hizi vimepotea machoni mwa jamii. Lakini hili nalo halikupewa nafasi ya watu kujua namna watu wa Visiwani wanavyopoteza utamaduni waliokuwa nao wazee wao.
Katika hotuba yake Dk. Shein alizungumzia haja ya kufanyia utafiti wa kina ili kuiibua historia ya kweli ya Zanzibar. Hili ni wazo zuri, lakini lililo muhimu ni kwa kazi hii kufanywa na watu wanaolielewa suala hili na ambao watakuwa wakweli na si wapotoshaji wa historia.
Ni vizuri kazi hii ikapewa umuhimu unaostahiki haraka ili maonyesho ya aina hii ya siku za mbele yatoe picha halisi ya Zanzibar ili watu wa Visiwani na nje wajue hasa Zanzibar imetokea wapi na ipo wapi.
Historia ina matokeo mabaya na mazuri, lakini yote haya yametokea na yanapaswa kuelezwa kwa usahihi wake. Kula chumvi au kupunguza sukari hakusaidii kwani ipo siku ukweli utadhihiri na uogo kujitenga.
Tuifanye kazi hii kwa nia safi na uadilifu kwani historia haifutiki na wanaoifumbia macho waelewe ipo siku watatokea watu watakaoeleza ukweli na wale wanaoipotosha hii leo watakuja kuumbuka na kuwatia aibu watoto na wajukuu zao kwa mambo waliyoyafanya wazee wao.
Ni kwa kuelewa vema historia ndiyo nchi inaweza kusonga mbele kwa amani na watu wake kuelewana na kuishi kwa raha, furaha, kuaminiana na kusameheana kwa makosa yaliyofanyika siku za nyuma.
Si vema na uungwana kuwalaumu na kuwahukumu wajukuu na virembwe vya vizazi vilivyopita kwa makosa yaliyofanywa na wazazi wao.
Tujifunze sasa kuwa wakweli na kama hatutaki ulimwengu utatufunza na kujutia unafiki tunaoufanya hivi sasa.
Chanzo : Tanzania Daima