STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 13 Januari, 2014
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amekutana na kufanya mazungumzo na Mjumbe Maalum wa Rais Xi Jinping wa Jamhuri ya Watu wa China.
Mjumbe huyo Maalum ambaye ni Waziri wa Makaazi na Maendeleo wa Miji na Vijiji Bwana Jiang Weixin amefika Zanzibar kumwakilisha Rais Xi Jinping katika Maadhimisho ya Miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Katika mazungumzo hayo ambayo yalihudhuriwa pia na Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Iddi, Dk. Shein alisema kuwa kitendo cha Raisi Xi Jinping kumtuma Mjumbe wake Maalum kushiriki katika maadhimisho hayo ni uthibitisho wa urafiki wa kweli uliodumu kwa miongo mingi kati ya Serikali na wananchi wa nchi mbili hizo.
Alimueleza Mjumbe huyo kuwa wananchi wa Zanzibar wamefarijika sana kupokea salamu za kuwatakia heri katika maadhimisho ya miaka 50 ya Mapinduzi kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Watu wa China Mheshimiwa Rais Xi Jinping.
Dk. Shein alirejea usemi wa Rais Xi Jinping kuwa urafiki wa wananchi wa Zanzibar na wenzao wa China si wa msimu bali wa wakati wote (all weather) na kwamba historia imedhihirisha hivyo katika miaka 50 ya Mapinduzi.
Alisisitiza kuwa kitendo cha Jamhuri ya Watu wa China kuwa miongoni mwa mataifa ya kwanza kuyatambua Mapinduzi ya Zanzibar kitabaki katika kumbukumbu za historia ya ukombozi wa watu wa Zanzibar.
Alieleza kuwa kitendo hicho hakiwezi kusahaulika kwa kuwa miaka 50 iliyopita wananchi wa Zanzibar walipokataa kutawaliwa na kuamua kujitawala wenyewe walihitaji kuungwa mkono na wanachi wenzao kote ulimwenguni na ndipo China bila ya ajizi ikayatambua Mapinduzi mara moja.
Mbali na kuyatambua Mapinduzi Dk. Shein alieleza kuwa katika miaka 50 ya Mapinduzi China imekuwa mstari wa mbele kushirikiana na watu wa Zanzibar katika harakati zao za kujiletea maendeleo.
Alitolea mfano ushirikiano wa Zanzibar na China mara baada ya Mapinduzi ambapo nchi hiyo ilisaidia katika uanzishaji wa viwanda mbalimbali, misaada katika kuendeleza kilimo cha kisasa, michezo, sekta ya habari pamoja na uimarishaji wa sekta ya afya ambayo ilikuwa nyuma sana humu nchini.
Aliongeza kuwa kwa Zanzibar kuzungumzia maendeleo ya sekta ya afya haiwezekani bila ya kutambua mchango mkubwa Serikali ya watu wa China na wataalamu kutoka nchi hiyo ambao walianza kufanyakazi nchini mara tu baada ya Mapinduzi.
Dk. Shein alimueleza Mjumbe huyo Maalum wa Rais Xi Jinping kuwa ushirikiano kati ya Zanzibar na Tanzania kwa jumla na Serikali na wananchi wa China umekuwa ukiimarika.
Kwa upande wake Bwana Jiang alieleza kuwa ni heshima kubwa kwake kuwasilisha Salamu za Pongezi na za Kirafiki kutoka kwa Rais Xi Jinping na wananchi wa Jamhuri ya Watu wa China kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na wananchi wa Zanzibar wakati huu wa kuadhimisha miaka 50 ya Mapinduzi.
Mwakilishi huyo Maalumu wa Rais wa china alisema kuwa Serikali na wananchi wa Jamhuri ya Watu wa China wanajivunia na kuthamini sana uhusiano na ushirikiano wake na Zanzibar pamoja na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwa uhusiano huo umejengwa katika misngi ya usawa na heshma kati ya Serikali na wanachi wa nchi mbili hizo.
Alisema miaka 50 ya wananchi wa Zanzibar kujitawala kutoka kwenye makucha ya wakoloni imeshuhudia maendeleo makubwa katika kila sekta na kwamba nchi yake ina matumaini makubwa kuwa kwa hatua hiyo iliyofikia Zanzibar ina nafasi nzuri zaidi ya kupiga hatua kubwa kwa haraka zaidi hivyo kuimarisha ustawi wa wananchi wake.
Bwana Jiang Weixin alimuhakikishia Rais pamoja wananchi wa Zanzibar kuwa Serikali ya nchi yake itaendelea kuziunga mkono jitihada zao za kujiletea maendeleo pamoja na kusisiitiza utekelezaji wa makubaliano yote ambayo yalitiwa saini wakati ziara ya Dk. Shein nchini China mwaka jana.