HOTUBA YA RAIS WA ZANZIBAR NA MWENYEKITI WA
BARAZA LA MAPINDUZI, MHE. DK. ALI MOHAMED SHEIN,
KATIKA SHEREHE ZA MAADHIMISHO YA MIAKA 50 YA
MAPINDUZI YA ZANZIBAR , UWANJA WA AMAAN
TAREHE 12 JANUARI, 2014
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein Akihutubia sherehe Mapinduzi Amaan.
Mawaziri wa Nchi Rafiki mliohudhuria hapa leo,
Mheshimiwa Dk. Jakaya Mrisho Kikwete,
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ;
Mheshimiwa Dk. Mohamed Gharib Bilal,
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ;
Mheshimiwa Mizengo Kayanza Peter Pinda,
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ;
Mheshimiwa Maalim Seif Sharif Hamad,
Makamu wa Kwanza wa Rais, Zanzibar ;
Mheshimiwa Balozi Seif Ali Iddi,
Makamu wa Pili wa Rais, Zanzibar ;
Mheshimiwa Mzee Ali Hassan Mwinyi,
Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ;
Mheshimiwa Benjamin William Mkapa,
Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ;
Mheshimiwa Dk. Salmin Amour Juma,
Rais Mstaafu wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi;
Mheshimiwa Dk. Amani Abeid Karume, Rais Mstaafu wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi;
Viongozi Wakuu Wastaafu Mliohudhuria;
Waheshimiwa Mawaziri wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ;
Mheshimiwa Mama Anne Makinda, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ;
Mheshimiwa Pandu Ameir Kificho, Spika wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar ;
Mheshimiwa Othman Chande Mohamed, Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ;
Mheshimiwa Omar Othman Makungu, Jaji Mkuu wa Zanzibar ;
Waheshimiwa Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa;
Mheshimiwa Abdalla Mwinyi, Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi;
Waheshimiwa Viongozi wa Serikali na Vyama vya Siasa;
Ndugu Wananchi, Mabibi na Mabwana;
Assalaam Alaykum,
Kwa unyenyekevu mkubwa, namshukuru Mwenyezi Mungu, Muumba Mbingu na Ardhi na vyote vilivyomo ndani yake, kwa kutujaalia uhai na uzima wa afya, tukaweza kukusanyika hapa leo kuadhimisha miaka 50 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar , ya tarehe 12 Januari, 1964. Namuomba Mola wetu aibariki shughuli yetu hii iwe ya mafanikio.
Kwa niaba ya wananchi wa Zanzibar , natoa shukrani zangu za dhati kwako Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania , Mheshimiwa Dk. Jakaya Mrisho Kikwete, kwa kuungana nasi katika sherehe zetu hizi adhimu na muhimu. Vile vile natoa shukrani kwa wageni wetu wote kutoka nje ya nchi yetu akiwemo Mheshimiwa Yoweri Kaguta Museveni, Rais wa Jamhuri ya Uganda, Mheshimiwa Dk. Ikililou Dhoinine, Rais wa Muungano wa Comoro, na Mjumbe Maalum, Waziri wa Makaazi na Maendeleo Miji na Vijiji Mheshimiwa Jiang Weixin anayemwakilisha Rais Xi Jinping wa Jamhuri ya Watu wa China. Kadhalika, natoa shukrani kwa viongozi wote wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, waliopo madarakani na waliostaafu, Mabalozi wa nchi mbali mbali, Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa, Viongozi wa dini na vyama vya siasa na wananchi wote kwa kuhudhuria kwa wingi kwenye sherehe hizi.
Kuwepo pamoja nasi wageni wetu mbali mbali kunatupa faraja kubwa sana . Kuja kwenu kunatudhihirishia kuwa Mapinduzi yetu yanaheshimika na yanapewa taadhima kubwa ndani na nje ya nchi yetu. Tuna kila sababu ya kujivunia uhusiano wetu na kuja kwenu ni uthibitisho wa juhudi zetu za pamoja za kuyaenzi Mapinduzi yetu.
Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,
Leo ni siku muhimu sana katika historia ya wananchi wa Zanzibar , ambapo miaka 50 iliyopita walikata minyororo ya utawala wa Kisultani na ukoloni wa Kiingereza uliodumu kwa miaka 132. Wananchi walikataa kwa vitendo kudharauliwa, kunyanyaswa, kubaguliwa na kutoheshimiwa katika nchi yao .
Ukombozi wa watu wa Zanzibar ulifanywa na Chama cha Afro-Shirazi, ambacho kilianzishwa tarehe 5 Februari, 1957, kwa madhumuni ya kuikomboa Zanzibar kutokana na madhila ya wakoloni, mabwanyenye na mabepari. Madhila haya walitendewa wananchi kwenye mambo yote muhimu katika maisha ya binadamu, kama vile kubaguliwa katika kupata elimu, huduma za matibabu, makaazi, chakula, ubaguzi kwenye kazi, ubaguzi na dhulma kwenye matumizi ya ardhi, ubaguzi katika kupata haki, na kadhalika.
Leo tunapoadhimisha sherehe za Mapinduzi kutimiza miaka 50, hatuna budi kuwakumbuka na kuwashukuru wazee wetu Waasisi wa Chama cha Afro-Shirazi walioongozwa na Rais wake wa Kwanza , Marehemu Mzee Abeid Amani Karume. Tunawakumbuka na tunawashukuru kwa ushujaa wao na jitihada zao za kupigania haki, kuleta usawa na maelewano na kuondoa kila pingamizi walizokuwa wakizipata wananchi wa Unguja na Pemba .
Kwa hivyo, leo ni siku ya kumbukumbu ya ushindi wa Chama cha Afro-Shirazi na ushindi wa wananchi wa Zanzibar na kwamba Mapinduzi yaliinua na kusimamisha utawala wa wanyonge na yaliweka usawa na kuwakabidhi tena wafanyakazi na wakulima wa Zanzibar, heshima yao na ubinadamu wao katika nchi yao.
Namuomba Mwenyezi Mungu amrehemu Jemadari wa Mapinduzi yetu Matukufu ya tarehe 12 Januari, 1964 Marehemu Mzee Abeid Amani Karume pamoja na waasisi wengine wa Mapinduzi hayo waliotangulia mbele ya haki na awape umri mrefu wale wote ambao wapo hai. Siku zote tutawakumbuka, tutawaenzi na tutawashukuru kwa kujitoa muhanga kwa ajili ya kutukomboa. Kutokana na jitihada zao na mapenzi kwa nchi yao , hivi sasa tupo huru na tunasherehekea miaka 50 ya Mapinduzi yetu na tutaendelea kuwa huru wakati wote. Hatutokubali kutawaliwa, kudhulumiwa, kubaguliwa na kudharauliwa katika nchi yetu.
Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,
Leo tunafikia kilele cha Maadhimisho ya Sherehe za Miaka 50 ya Mapinduzi ya tarehe 12 Januari, 1964 ni siku ya furaha kubwa na ya kusherehekea kwa vifijo na hoi hoi kama tulivyokaribishwa katika uwanja huu wa Amaan na tulivyojionea wenyewe muda mfupi uliopita. Hata hivyo, sherehe hizi zinatukumbusha umuhimu wa kuendelea kuyalinda, kuyatetea na kuyadumisha mapinduzi yetu kama tulivyofanya katika kipindi cha miaka 50 iliyopita, kwa mafanikio makubwa.
Tunaposherehekea miaka 50 ya Mapinduzi ya tarehe 12 Januari, 1964, vile vile tunasherehekea umoja wetu uliotokana na muungano wa nchi mbili zilizokuwa huru; Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na kuzaliwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania , tarehe 26 April, 1964. Muungano wetu umetokana na sera sahihi za vyama viasisi vya TANU na ASP na sasa CCM pamoja na uongozi bora na thabiti wa waasisi wa nchi yetu Marehemu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Marehemu Mzee Abeid Amani Karume na viongozi wa awamu nyengine waliofuata baadae.
Wakati tunasherehekea miaka 50 ya Mapinduzi, ni wazi kwamba tunasherehekea amani, umoja na maendeleo yaliyopatikana. Kwa hivyo, tunapaswa kuuenzi na kuuendeleza umoja na mshikamano wetu ambao ndio siri kubwa ya kuendelea kuwepo kwa hali ya amani na utulivu yenye kuimarisha maendeleo yetu.
Kwa msingi huo, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeiweka kauli mbiu ya maadhimisho haya isemayo: “Tudumishe amani, umoja na maendeleo ambayo ni matunda ya Mapinduzi yetu – Mapinduzi Daima”.
Nafarijika sana kuona wananchi wa Zanzibar wameungana na Serikali yao katika kipindi cha miaka 50 kwa kuyatekeleza madhumuni na malengo pamoja na shabaha ya Mapinduzi yetu na kupatikana maendeleo ya kisiasa, kiuchumi na kijamii.
Katika kipindi cha miaka 50, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar , imeweza kuyatekeleza na kuyaendeleza madhumuni, malengo pamoja na shabaha ya Mapinduzi. Katika kipindi chote hicho, Serikali ilipanga mipango yake na iliitekeleza kwa mafanikio makubwa. Kwa hivyo, ni wazi kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imefanya mambo mengi ya maendeleo kuliko yale yaliyofanywa na wakoloni, kwa muda wa miaka 132 ya utawala wao. Maelezo nitakayoyatoa yanadhihirisha ukweli huo.
Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,
Katika kipindi cha miaka 50 iliyopita, nchi yetu imepitia katika mifumo miwili ya kisiasa na demokrasia kwa mujibu wa Katiba ya nchi. Mara tu baada ya Mapinduzi ya 1964, nchi yetu ilikuwa na mfumo wa chama kimoja cha siasa hadi mwaka 1992 uliporejeshwa mfumo wa vyama vingi vya siasa nchini. Mfumo wa vyama vingi vya siasa umetanua demokrasia kwa kuwapa fursa wananchi kujiunga na chama chochote cha siasa na kuchagua viongozi wanaowataka. Tangu kurejeshwa mfumo wa vyama vingi vya siasa mwaka 1992, jumla ya chaguzi nne (4) zimeshafanyika ambapo wananchi walikichagua Chama cha Mapinduzi kuiongoza nchi yetu.
Katika kuimarisha umoja na mshikamano miongoni mwa wananchi, mwaka 2010, Zanzibar ilifanya mabadiliko ya 10 ya Katiba yake ya mwaka 1984, iliyoviwezesha vyama vya siasa vyenye uwakilishi katika Baraza la Wawakilishi kushirikiana katika kuiongoza Zanzibar . Hatua hii iliiwezesha Zanzibar kuunda Serikali yenye Muundo wa Umoja wa Kitaifa ambayo kwa kiasi kikubwa imesaidia kuimarisha umoja wetu na mshikamano na kuchangia katika kuongeza kasi ya maendeleo.
Tunasherehekea miaka 50 ya Mapinduzi yetu, wakati nchi yetu ikiwa imepiga hatua kubwa za mafanikio katika kuimarisha suala la Utawala Bora na Haki za Binaadamu. Zanzibar ina Katiba yake ya mwaka 1984 iliyoundwa kwa misingi ya kusimamia na kuendeleza malengo ya Mapinduzi.
Nchi yetu inafuata mfumo wa mgawanyo wa madaraka kati ya Mamlaka tatu; Mamlaka ya Utendaji (Serikali). Mamlaka ya Kutunga Sheria na Kusimamia Utekelezaji wa Shughuli za Umma (Baraza la Wawakilishi) na Mamlaka ya Kutekeleza Utoaji Haki (Mahakama). Mfumo wa aina hii haukuwepo kabla ya Mapinduzi ya tarehe 12 Januari, 1964.
Baraza la Wawakilishi liliundwa mwaka 1980 na Tume ya Uchaguzi ilianzishwa mwaka 1993 kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984. Taasisi hizi zinatekeleza vyema majukumu yao na kupelekea wananchi kutumia haki zao za kidemokrasia kwa mujibu wa sheria. Katika kusimamia suala la kupambana na rushwa na uhujumu uchumi, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeanzisha Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi katika mwaka 2012 na imeanza kazi zake vizuri.
Tunapotathmini suala la Utawala Bora, katika kipindi hiki cha miaka 50 ya Mapinduzi ni dhahiri kwamba mafanikio makubwa yamepatikana kwenye Mahakama zetu kwa kuwa na Mahakimu na Majaji wengi zaidi ambao wote ni wananchi na wameendelea kutoa hukumu kwa kuzingatia misingi ya haki. Aidha, ndani ya kipindi hiki sheria kadhaa zimepitiwa na kurekebishwa na nyengine mpya zimetungwa zikiwemo za kulinda haki za watoto na kuanzishwa kwa Mahakama ya Watoto mwaka 2012. Zaidi ya hayo, wananchi wanaelimishwa kwa njia mbali mbali ili kuelewa umuhimu wa kutii sheria, kujiepusha na vitendo visivyofaa katika jamii na kuishi kwa uadilifu.
Katika kipindi cha miaka 50 ya Mapinduzi, Serikali imechukua juhudi za kuimarisha uchumi wa nchi yetu. Mafanikio makubwa yamepatikana katika ukusanyaji wa mapato ya Serikali ambapo kwa wastani yameongezeka mwaka hadi mwaka. Kwa mwaka wa fedha 2012/2013 mapato yalifikia TShs. bilioni 266.2 kutoka TShs. milioni 59.67 mwaka 1964/1965.
Vile vile, uchumi wetu umekuwa ukikua kila mwaka na kwa mwaka 2012/2013 umefikia asilimia 7.0 na kwa mwaka 2013/2014 unatarajiwa kukua kwa asilimia 7.5. Pato la Taifa limekuwa likiongezeka kutoka thamani ya TShs. bilioni 16.6 mwaka 1990 na kufikia thamani ya TShs. bilioni 1,352 kwa mwaka 2012.
Kadhalika, pato la mtu binafsi nalo limekuwa likiongezeka kutoka TShs. 726,000 (US$462) mwaka 2010 na kufikia TShs. 1,003,000 (US$ 656) mwaka 2012, kiwango ambacho kimevuka maelekezo ya Ilani ya CCM ya 2010-2015 ya kufikia TShs. 884,000 ifikapo mwaka 2015.
Mfumko wa bei umeendelea kudhibitiwa na hadi Disemba, 2013 umefikia asilimia 5.0 kutoka asilimia 9.4 mwaka 2012.
Tunaposherehekea miaka 50 ya Mapinduzi, vile vile, tunajivunia kuimarika kwa sekta ya fedha. Hivi sasa idadi ya benki za biashara imefikia 10 kutoka benki mbili (2) zilizokuwepo kabla ya Mapinduzi.
Kuhusu Mipango ya Maendeleo, kabla ya Mapinduzi hapakuwepo mipango ya aina hiyo iliyokuwa rasmi. Katika kuimarisha Mipango ya Maendeleo Tume ya Mipango ya kwanza iliundwa 1977 ambapo Mpango wa Maendeleo wa miaka mitatu 1978/79 – 1980/1981, uliandaliwa.
Utaratibu wa kuwa na Tume ya Mipango umeendelea hadi hivi sasa. Katika mwaka 2000 Dira ya Maendeleo ya Zanzibar 2020 ilizinduliwa na utekelezaji wake ulianza. Mpango wa kwanza wa utekelezaji wa Dira ulikuwa ni Mpango wa Kupunguza Umasikini uliotekelezwa mwaka 2002 hadi 2005. Mpango huo ulifuatiwa na Mpango wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini (MKUZA I) mwaka 2007/2010 na baadae (MKUZA II) 2010/2015.
Mipango yote hii inalenga katika kuimarisha uchumi na kupunguza umasikini wa kipato, kuimarisha huduma na ustawi wa jamii pamoja na kuimarisha utawala bora na Umoja wa Kitaifa, ambapo utekelezaji wake umeleta mafanikio makubwa.
Dhamira ya kuimarisha maisha ya wananchi wa Zanzibar iko wazi na lengo la Dira 2020 liko pale pale ili nchi yetu iwe katika uchumi wa kiwango cha kati. Tutaendelea kufanya kila jitihada ili uchumi uweze kukua kwa asilimia 8-10, ifikapo mwaka 2020. Lengo hili litaweza kufanikiwa ingawa uchumi wetu unakabiliwa na changamoto nyingi.
Sekta ya biashara ni miongoni mwa sekta muhimu katika maendeleo ya ukuaji uchumi hasa ikizingatiwa kuwa nchi yetu ni kisiwa chenye eneo dogo kwa kuendeleza kilimo na mambo mengine yanayohitaji ardhi kubwa. Kwa kuzingatia umuhimu huo, mara baada ya Mapinduzi hadi leo hatua mbali mbali zimechukuliwa ili kuimarisha mazingira ya ufanyaji wa biashara.
Kwa hivyo, mwaka 1963, Serikali ya kikoloni iliendeleza utaratibu wa kusafirisha bidhaa na kununua bidhaa, bidhaa zenye thamani ya TShs. milioni 117.960 zilisafirishwa na bidhaa zenye thamani ya TShs. milioni 122.920 ziliingizwa nchini.
Biashara ya usafirishaji na uingizaji wa bidhaa imeweza kuimarika ambapo usafirishaji hasa wa karafuu na mwani umeongezeka kutoka TShs. milioni 17,907 mwaka 2010 hadi TShs. milioni 67,390.5 mwaka 2012, ongezeko la asilimia 276.3. Bidhaa zenye thamani ya TShs. milioni 271,273.1 zimeagizwa, mwaka 2012 kutoka TShs. milioni 129,137 mwaka 2010. Biashara hii imefanyika kutokana na mazingira mazuri yaliyopo.
Serikali inaendelea kusimamia biashara ya karafuu kupitia Shirika la Biashara la Taifa la Zanzibar (ZSTC) lililoanzishwa mwaka 1966, na biashara hio inaendelea vizuri. Wakulima wa karafuu wanalipwa asilimia thamanini (80) ya bei ya soko na ununuzi unaendelea vizuri, ambapo bei ya kilo moja inanunuliwa na ZSTC kutoka kwa wakulima, kwa TShs. 14,000, hivi sasa, bei hii ni kubwa kuliko miaka iliyopita. Kwa mfano, mwaka 2008 ilikuwa TShs. 2,500 kwa kilo. Serikali inafanya jitihada ya kuliimarisha zao la karafuu kwa kuzifanyia karafuu za Zanzibar utambulisho maalum (branding). Hatua nzuri zimefikiwa katika utekelezaji wa mpango huu.
Serikali imeandaa sera ya maendeleo ya viwanda ambapo umiliki na uendeshaji wa viwanda kupitia sekta binafsi umehamasishwa na umeimarishwa na viwanda kadhaa vimeanzishwa na tayari sera hio imeanza kutekelezwa. Eneo Maalum la Uwekezaji (EPZ) lililotengwa na Serikali huko Fumba limeanza kutumika na kiwanda kikubwa cha maziwa kimejengwa na mwekezaji wa ndani na wawekezaji wengine wameonesha nia ya kuwekeza.
Ndugu Viongozi na Ndugu Wananchi,
Kabla ya Mapinduzi huduma za utalii hazikuwa katika msimamo madhubuti na zilifanywa na watu wachache ambao hawakujali uhusiano baina ya watalii na wananchi wa Zanzibar. Shabaha yao ilikuwa ni kuingiza fedha mikononi mwao tu.
Katika jitihada za kuimarisha huduma za utalii, Serikali ilijenga hoteli mpya tano (5), Unguja na Pemba na ililiimarisha Shirika la Utalii kwa kupewa nyenzo, vifaa na wafanyakazi. Idadi ya watalii waliokuja Zanzibar mwaka 1986 ilikuwa 29,211 na iliongezeka hadi kufikia watalii 143,282 mwaka 2007. Idadi hii ni ongezeko la takriban mara 5. Kwa mwaka 2012, idadi ya watalii iliongezeka na ilifikia 169,223 na mwaka 2013 idadi ya watalii iliongezeka na kufikia watalii 181,242. Ongezeko hili ni sawa na asilimia 7.10.
Asilimia 72 ya Wawekezaji wote wanawekeza katika sekta ya utalii hapa Zanzibar na hivi sasa zipo hoteli zenye vyumba 7995 na kati ya hoteli hizo, 26 ni za nyota tano. Sekta ya utalii ni sekta kiongozi kutokana na MKUZA II, inakuwa kwa asilimia 6 na inachangia Pato la Taifa kwa asilimia 27 na Serikali inapata asilimia 80 ya fedha za kigeni kutokana na utalii. Serikali inaendelea kuwashajiisha wawekezaji na imeweka mipango madhubuti ya kuongeza watalii ili ifikapo 2015 idadi ya watalii ifikie 500,000.
Kabla ya Mapinduzi elimu ilikuwa ikitolewa kwa ubaguzi na ilikuwa ya kulipia. Watoto wa wananchi waliowengi, ambao ni maskini hawakuwa na uwezo wa kupata elimu. Baada ya Mapinduzi, tarehe 23 Septemba, 1964, Marehemu Mzee Abeid Amani Karume, alitangaza rasmi elimu kutolewa bure; bila ya malipo na bila ya ubaguzi wowote kwa wanafunzi wa Unguja na Pemba.
Yalipofanyika Mapinduzi, tarehe 12 Januari, 1964, wakoloni walituachia skuli mbili tu za Maandalizi (Nursery) na hivi sasa zipo skuli 278 zenye wanafunzi 30,912. Kwa upande wa skuli za msingi zilikuwepo skuli 62 tu zilizokuwa na wanafunzi 19,106 kwa Unguja na Pemba. Hivi sasa, zipo skuli za msingi 342 zenye wanafunzi 247,353.
Kuhusu elimu ya sekondari, hivi sasa zipo skuli za sekondari 252 zenye wanafunzi 84,096 ikilinganishwa na skuli za sekondari za Serikali nne (4), zilizokuwa na wanafunzi 734 hadi mwaka 1963.
Kwa upande wa mafunzo ya Amali, ilikuwepo skuli moja tu. Hivi sasa zipo skuli tano (5) zenye wanafunzi 1,125.
Leo tunaposherehekea miaka 50 ya Mapinduzi, Zanzibar inavyo vyuo tisa (9) vya masomo mbali mbali (colleges) na kabla ya Mapinduzi ya tarehe 12 Januari, 1964, Zanzibar ilikuwa na chuo kimoja tu cha ualimu (Teacher Training College). Hivi sasa, Zanzibar ina vyuo vikuu vitatu navyo ni, Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar, Chuo Kikuu cha Zanzibar na Chuo cha Elimu Chukwani na kwa mwaka huu wa masomo vyuo hivi vina jumla ya wanafunzi 4485. Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar kimeanzisha skuli mbali mbali, na Septemba, 2013 ilianzishwa skuli ya masomo ya udaktari (school of medicine) yenye jumla ya wanafunzi 33. Lengo la mpango huu ni kujitosheleza kwa madaktari, mbali na mpango maalum uliopo sasa wa masomo ya udaktari yanayoendeshwa kwa kushirikiana na Serikali ya Cuba.
Ni dhahiri kwamba, Serikali ya Mapinduzi imefanya kazi kubwa ya kuimarisha elimu na katika kuwasomesha, kuwaandaa na kuwaendeleza watalaamu wake kwa ajili ya maendeleo ya Zanzibar, jambo ambalo halikufanyika katika miaka yote ya utawala wa kikoloni. Ingawa zipo changamoto mbali mbali zinazotokana na kuimarika kwa elimu, hata hivyo, Serikali imeandaa mipango mbali mbali ya kuzipatia ufumbuzi changamoto hizo.
Ndugu Viongozi na Ndugu Wananchi,
Katika kipindi cha miaka 50 iliyopita, Serikali ilifanya juhudi kubwa na za makusudi za kuzipanua huduma za afya ambazo zikitolewa kwa ubaguzi na hazikutosheleza mahitaji ya wananchi. Mwaka 1965 ilitangazwa rasmi kwamba huduma za afya zitatolewa bure. Mipango madhubuti ya kuziendeleza huduma za kinga na tiba iliandaliwa kutokana na Mpango wa Mwanzo wa Afya wa mwaka 1965 na Sera ya Afya ya 1999, ambapo ulifanywa uamuzi wa kuzipeleka huduma za afya karibu na wanakoishi wananchi, kuongeza upatikanaji wa vifaa, nyenzo na dawa, mafunzo ya wataalamu mbali mbali wa afya, ujenzi wa hospitali na vituo vya afya.
Hivi sasa huduma za afya zinatolewa katika hospitali tofauti 12 badala ya hospitali 5 na vituo vya afya 134 badala ya 36 kabla ya Mapinduzi. Vile vile huduma zinatolewa na hospitali za vyombo vya Ulinzi na Usalama pamoja na Idara Maalum za SMZ, taasisi za Watu Binafsi, mpango ambao kabla ya Mapinduzi haukuwepo.
Kuwepo kwa vituo vingi vya afya kunatoa nafasi kwa mwananchi kupata huduma za afya kwa kwenda chini ya kilomita tano. Zaidi ya asilimia 95 ya wananchi wanaishi ndani ya mzunguko wa kilomita 5 za huduma za afya.
Katika jitihada za kuwasomesha wataalamu wake, Serikali inatoa mafunzo katika fani mbali mbali za afya katika kiwango cha Stashahada na hivi karibuni chuo hiki kitaunganishwa na Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA).
Uwezo wetu umeimarika sana wa kupambana na maradhi ya kuambukiza na yasiyoyakuambukiza kwa kushirikiana na Shirika la Afya Duniani na Washirika wetu wa Maendeleo. Hivi sasa uwiano wa daktari kwa idadi ya watu ni 1:18,982. Hata hivyo, mnamo mwezi wa Agosti mwaka huu Serikali inatarajia kuwaajiri madaktari 38 watakaomaliza masomo yao yanayoendeshwa na Chuo cha Madaktari cha Mathansas, Cuba, kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Aidha, madaktari wengine 12 watakaomaliza masomo yao mwaka ujao katika utaratibu huo pamoja na wale wanaomaliza masomo yao katika vyuo vya udaktari vya Tanzania Bara na viliopo nchi za nje, wataajiriwa. Kwa hivyo, katika miaka michache ijayo, tatizo la upungufu wa madaktari litapungua sana.
Kadhalika, jitihada zetu za kupambana na maradhi ya Malaria zimefanikiwa sana kwa kushirikiana na Taasisi mbali mbali duniani. Kiwango cha malaria na kasi ya kuenea kwake kimepungua na kimefikia asilimia 0.3 ikilinganishwa na asilimia 45 miaka ya tisini na asilimia 12 mwaka 2005. Mipango madhubuti imeandaliwa ili mafanikio haya yaliyopatikana yawe endelevu na kiwango chake kiendelee kupungua. Jitihada zetu za kupambana na UKIMWI zimepata mafanikio ya kuridhisha na wanaoishi na virusi vya UKIMWI ambao wanatumia ARVs afya zao zimeimarika. Jitihada hizi zinaendelezwa kwa kushirikiana na washirika wetu wa maendeleo.
Ndugu Viongozi na Ndugu Wananchi,
Katika kuhakikisha kwamba wananchi wanapata maji safi na salama, mara baada ya Mapinduzi, Serikali ilitilia mkazo katika kuimarisha sekta ya maji. Katika mwaka 1964, hali ya upatikanaji wa huduma za maji safi na salama kote nchini ilikuwa ni asilimia 27 tu. Upatikanaji wa huduma hizi za maji ni muhimu kwa maisha ya watu na umefikia wastani wa asilimia 76 kwa wananchi wa mjini hadi mwaka 2010 na asilimia 60 vijijini. Jitihada mbali mbali za kuimarisha huduma hizo zinaendelea kuchukuliwa na Serikali kwa kushirikiana na Washirika wetu wa Maendeleo ili upatikanaji wa huduma za maji ufikie asilimia 95 mjini na asilimia 80, kwa vijijini ifikapo mwaka 2015 kwa kuzingatia Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu ya mwaka 2010-2015 na MKUZA II.
Serikali imechukua mkopo kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika kwa lengo la kuimarisha huduma za maji katika mji wa Wete, Chake Chake na Mkoani kwa upande wa Pemba na Wilaya ya Kati kwa upande wa Unguja na vijiji kadhaa viliomo katika Wilaya hizo vitafaidika na mradi huo. Hadi sasa visima vyote vimeshachimbwa, mabomba yamelazwa na yamefungwa na matangi ya maji yamejengwa na uchunguzi wa maji umefanyika katika miji yote mitatu ya Pemba. Kadhalika, Serikali ya Ras Al Khaimah imetoa msaada kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika uchimbaji wa visima 50 kwenye maeneo mbali mbali ya Unguja na Pemba. Visima hivyo tayari vimeanza kuchimbwa katika maeneo mbali mbali na kazi inaendelea vizuri. Jitihada za kuimarisha huduma za maji kwa Mkoa wa Mjini Magharibi nazo zinaendelea vizuri kwa kutekeleza awamu ya pili ya mradi wa JICA, mkopo kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika na visima 21 vitachimbwa kwa msaada wa Serikali ya Ras Al Khaimah. Jitihada hizi ambazo Serikali imezichukua zina lengo la kupunguza tatizo la maji Unguja na Pemba kwa madhumuni ya kutekeleza malengo ya Mapinduzi ya 12 Januari, 1964 ya kuwapatia wananchi huduma za maji safi na salama. Serikali inawaomba wananchi waendelee kuwa na subira wakati jitihada zinafanywa za kulipunguza tatizo la upatikanaji wa maji safi na salama na baadae liondoshwe kabisa.
Kabla ya Mapinduzi, ardhi ilimilikiwa na wakoloni na watu waliokuwa na uwezo, wanyonge wa Zanzibar hawakupewa nafasi ya kuitumia ardhi yao iliyochukuliwa kutokana na unyonge na umasikini wao. Tarehe 8 Machi, 1964, Marehemu Mzee Abeid Amani Karume alitangaza rasmi kwamba ardhi yote ni mali ya Serikali na iligaiwa kwa wananchi wote bila ya kujali rangi, dini wala kabila. Vile vile, tarehe 11 Novemba, 1965 aliuzindua mpango wa kugawa ardhi na aliwagawia wananchi eka tatu tatu hapo Dole. Hadi mwaka 1973, jumla ya eka 24,000 ziligaiwa kwa wananchi wa Unguja na Pemba na ugawaji huo uliendelezwa katika kipindi cha miaka 50.
Wakati tunasherehekea miaka 50 ya Mapinduzi, ni jambo la fakhari kuona kwamba wananchi wanaitumia vizuri ardhi waliyopewa kwa kuendeshea maisha yao. Katika kipindi hiki, sheria mbali mbali zinazosimamia ardhi zimetungwa pamoja na sera ya Ardhi na Mahkama ya Ardhi imeanzishwa kwa ajili ya kutatua migogoro ya ardhi.
Kuhusu matumizi endelevu ya ardhi, Idara ya Mipango Miji na Vijiji imeanzishwa na Mpango Mkuu wa Matumizi ya Ardhi wa Zanzibar wa 2013 umetayarishwa. Kadhalika, katika kipindi hiki, Serikali imewapimia wananchi viwanja katika maeneo mbali mbali Unguja na Pemba, kwa ajili ya ujenzi wa nyumba na uwekezaji na katika mwaka 2010-2013 peke yake viwanja 1393 vilitolewa.
Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,
Kabla ya Mapinduzi Matukufu wanyonge hawakuwa na uwezo wa kuishi kwenye nyumba bora. Baada ya Mapinduzi, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iliamua kuwajengea wananchi makaazi bora ya kisasa bila ya ubaguzi wowote.
Katika azma ya kuwajengea wananchi nyumba bora na za kisasa, ujenzi wa nyumba za kisasa za ghorofa ulianzishwa na Marehemu Mzee Abeid Amani Karume tarehe 11 Agosti, 1964. Ujenzi huo ulianza Kikwajuni, baadae Kilimani, Michenzani na Mombasa. Aidha, nyumba kama hizo zilijengwa huko Pemba katika mji wa Wete, Micheweni, Chake Chake, Mkoani na Kengeja. Kadhalika, nyumba hizo za maendeleo zilijengwa Makunduchi, Bambi na Chaani. Jumla ya fleti 2928 zilijengwa na kupewa wananchi. Baadae ujenzi wa nyumba za vijijini ulianzishwa katika sehemu mbali mbali za Unguja na Pemba.
Kutokana na kuimarika kwa uchumi wa Zanzibar, wananchi wengi wamepata uwezo wa kujenga nyumba zao wenyewe. Hivi sasa wananchi wanajenga nyumba bora na nzuri kuliko wakati wowote wa miaka iliyopita. Katika kuendeleza malengo ya Mapinduzi ya kuwapatia wananchi makaazi bora, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaanzisha Shirika la Nyumba hivi karibuni ambalo litakuwa linasimamia ujenzi na upatikanaji wa makaazi bora na ya kisasa kwa wananchi wa Zanzibar zitakazojengwa kwa ushirikiano na taasisi za watu binafsi na kuuzwa kwa wananchi kwa bei nafuu.
Ndugu Viongozi na Ndugu Wananchi,
Kabla ya Mapinduzi, wakoloni walitumia ardhi, zaidi kwa kilimo cha mazao ya biashara ya karafuu na nazi kwa lengo la kusafirisha nje. Uzalishaji wa mazao ya chakula kama vile mpunga na matunda kwa ajili ya mahitaji ya ndani hayakupewa umuhimu mkubwa.
Baada ya Mapinduzi, Serikali ilikiimarisha kilimo kwa kuanzisha mashamba ya mpunga na mazao mengine na juhudi hizo zililenga katika kupunguza uagiziaji wa vyakula muhimu vinavyohitajiwa na wananchi kutoka nje ya nchi.
Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,
Katika kuimarisha kilimo, mara tu baada ya Mapinduzi, Serikali iliagiza matrekta kwa madhumuni ya kuwafanya wananchi waache kutumia jembe la mkono katika kilimo cha mpunga. Sambamba na kununua matrekta, kilianzishwa kiwanda cha kutengenezea matrekta huko Mbweni kwa lengo la kuyahudumia matrekta hayo. Vile vile, wakulima walisaidiwa pembejeo za kilimo ambazo zilisaidia sana kuliimarisha shamba la Cheju na Upenja.
Jitihada za kutekeleza mapinduzi ya kilimo zilizoanzishwa hivi karibuni zimefanikiwa kwa kuagiza matrekta mapya na zana nyengine za kilimo, kutoa ruzuku katika pembejeo mbali mbali za kilimo cha mpunga kwa asilimia 75 na kuongeza kiwango cha mbolea kutoka tani 30 hadi 1500. Dawa za kuulia magugu, kiwango chake kimeongezeka kutoka lita 12,000 hadi kufikia lita 30,000 katika mwaka 2010-2013. Kilimo cha mpunga wa umwagiliaji maji, katika mabonde mbali mbali kinaendelezwa na hekta 720 zimeshatayarishwa kati ya hekta 8,521 zilizotengwa. Taasisi ya utafiti wa kilimo Kizimbani imeimarishwa kwa nyenzo, vifaa na wataalamu na Maabara mpya imezinduliwa katika sherehe za miaka 50 ya Mapinduzi.
Chuo cha Kilimo cha Kizimbani nacho kimeimarishwa na mafunzo ya Stashahada ya Kilimo yameanza kutolewa. Mafunzo kwa skuli za wakulima mashambani yameendelezwa na skuli za wakulima zenye kuhudumia kaya 24,000 zimeanzishwa.
Ndugu Viongozi na Ndugu Wananchi,
Katika kuimarisha zao la karafuu ambalo lina mchango mkubwa kwenye uchumi wetu, Serikali imechukua juhudi za kuliendeleza zao hili na imeongeza uzalishaji wa miche kutoka 500,000 mwaka 2012 na kuongeza kiwango cha miche hadi kufikia miche 1,000,000 kwa mwaka 2013/14 ambayo inatolewa kwa wakulima bure. Lengo la Serikali ni kutoa miche milioni moja kwa kila mwaka katika miaka mitatu ijayo. Katika kutekeleza Mapinduzi ya Kilimo, Serikali inaimarisha mazao ya chakula, matunda na mazao ya viungo mbali mbali kwa ajili ya biashara. Serikali inawapongeza wakulima wote kwa jitihada zao za kuimarisha kilimo na kuhakikisha kwamba wakati wote tunakuwanacho chakula cha kutosha. Kwa wakulima wa karafuu tunawapongeza kwa kuuza karafuu zao ZSTC. Takwimu za mauzo zinadhihirisha uamuzi wao. Hongereni sana. Kadhalika pokeeni pongezi za Serikali kwa kutuunga mkono kwenye mapambano yetu dhidi ya wafanya magendo ya karafuu.
Ndugu Viongozi na Ndugu Wananchi,
Kabla ya Mapinduzi huduma za ufugaji hazikuendelezwa sana na hata mifugo haikuwepo ya kutosha na ilibidi iagiziwe kutoka nchi za nje. Baada ya Mapinduzi ya 12 Januari, 1964 Serikali iliipa umuhimu mkubwa sekta ya ufugaji. Wafugaji walipewa taaluma za namna bora ya kufuga. Aidha, walipouza mifugo yao kama vile ng’ombe, kuku na kadhalika, walipewa bei za juu.
Mashamba ya ufugaji kuku wa Serikali na mazizi ya ng’ombe kwa ajili ya nyama na maziwa yalifunguliwa katika maeneo mbali mbali. Vile vile, vituo zaidi kwa matibabu ya wanyama vilifunguliwa huko vijijini katika maeneo waliyoishi wafugaji.
Katika miaka ya hivi karibuni jitihada kubwa zimechukuliwa za kuwaendeleza wafugaji kupitia programu mbali mbali, ikiwemo programu ya kuimarisha huduma za mifugo (ASDP-L) yenye kutoa taaluma ya ufugaji bora. Katika mwaka 2011/2012, vikundi vipya vya skuli za wafugaji 335 vya Unguja na Pemba vilipewa mafunzo. Aidha, wafugaji 3200 walitembelewa na kupewa ushauri wa kitaalamu.
Vile vile, katika kuimarisha huduma za utafiti na utibabu wa wanyama, matengenezo makubwa yamefanywa kwenye maabara ya Maruhubi Unguja na Chake Chake Pemba pamoja na kuimarisha vituo vya mifugo viliopo sehemu mbali mbali.
Jitihada hizi za Serikali zimesaidia sana kuyainua maisha ya wafugaji katika kupambana na umasikini.
Ndugu Viongozi na Ndugu Wananchi,
Kabla ya Mapinduzi Zanzibar haikuwa na wataalamu wa uvuvi. Kwa hivyo, mwaka 1965 Serikali iliwapeleka vijana wake nchi za nje ili kusomea uvuvi. Idara ya Uvuvi na Shirika la Uvuvi (ZAFICO) lilianzishwa ili kuendeleza uvuvi. Katika kipindi chote Serikali imefanya jitihada kubwa za kuuimarisha uvuvi kwa kuwashajiisha wavuvi wadogo wadogo wanaoishi pembezoni mwa mwambao wa bahari. Kutokana na juhudi hizo kiwango cha samaki kilichovuliwa kimeongezeka katika miaka ya hivi karibuni. Wastani wa tani 30,500 zilivuliwa mwaka 2012 ikilinganishwa na tani 28,759 mwaka 2011. Uzalishaji wa mwani vile vile umeongezeka kutoka tani 12,259 mwaka 2011 hadi tani 13,844 mwaka 2012, Zanzibar ikiwa ni ya pili baada ya Thailand kwa kuzalisha mwani kwa wingi. Wavuvi wameendelea kuwezeshwa kwa kuwapa mafunzo ya uvuvi bora unaozingatia uhifadhi wa mazingira na matumizi bora ya vifaa vya kisasa. Mafunzo kwa wavuvi juu ya udhibiti wa mazingira ya baharini yamefanywa na mradi wa MACEMP ambao ulilenga kuyaendeleza maeneo ya ukanda wa pwani ya Unguja na Pemba. Jumla ya TShs. 163.6 milioni zilitolewa kwa kuwaendeleza wavuvi wa Unguja na Pemba.
Kutokana na jitihada zilizochukuliwa na Serikali, mchango wa sekta ya uvuvi katika Pato la Taifa umepanda kutoka asilimia 6.1 mwaka 2011 hadi 6.7 mwaka 2012.
Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,
Kabla ya Mapinduzi yetu ya 1964, wananchi wengi waliokuwa wakiishi sehemu za vijijini walikuwa wakipata shida ya usafiri kwa sababu hakukuwa na barabara za maana, zilikuwa chache za lami na nyingi za udongo na kifusi. Kabla ya Mapinduzi barabara za Zanzibar zilikuwa na urefu wa km 408 ambapo Unguja ilikuwa ni km 210 na Pemba ni km 198.
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar mara tu baada ya Mapinduzi ilianza ujenzi wa barabara za lami na madaraja, mashamba na mjini. Leo tunaona fakhari kwamba hivi sasa barabara za Zanzibar zina urefu wa km. 680.70; Unguja km. 450.25 na Pemba km 230.45. Barabara zote hizi ni za lami na za kisasa.
Vile vile, barabara za Kaskazini Pemba zimejengwa upya kwa msaada wa Shirika la MCC la Marekani na ziko katika hatua ya mwisho kumalizika na zinatarajiwa kuzinduliwa hivi karibuni. Hivi sasa, Zanzibar ina mtandao bora wa barabara na ni dhahiri zitatoa mchango mkubwa katika kuimarisha uchumi wetu na kuwahudumia wananchi katika maisha yao ya kila siku.
Ndugu Viongozi na Ndugu Wananchi,
Huduma za Bandari baada ya Mapinduzi ziliimarishwa sana na Bandari ya Malindi ilibadilishwa muundo wake wa zamani uliojengwa kabla ya Mapinduzi. Bandari hio imejengwa upya kwa msaada wa Umoja wa Nchi za Ulaya. Bandari hiyo hivi sasa inahudumia abiria na makontena mengi zaidi. Kwa mfano mwaka 2012 yamepokelewa makontena 39,821 kutoka 39,293 mwaka 2011. Ongezeko hili ni asilimia 27. Serikali imeimarisha bandari hiyo kwa kununua mashine za kisasa mbali mbali. Majengo mapya ya kupumzikia abiria yamejengwa na Kampuni ya Azam Marine kwa kushirikiana na Serikali. Kwa upande wa Pemba, gati mpya ya Mkoani imejengwa, huduma za bandari zimeimarishwa pamoja na jengo la abiria.
Katika hatua za kuimarisha usafiri wa anga, Serikali imechukua hatua ya kukiimarisha na kukiendeleza kiwanja cha ndege cha Kimataifa cha Abeid Amani Karume, ambapo njia ya kurukia na kutulia ndege imeongezwa urefu hadi mita 3022 na upana umeongezwa hadi mita 45. Hivi sasa uwanja huo una uwezo wa kuhudumia ndege za aina zote kubwa. Ujenzi wa “taxiway” mpya na “apron” umekamilika na ujenzi wa jengo jipya la abiria katika eneo la pili (terminal 2) unaendelea. Kwa upande wa uwanja wa Pemba, jitihada kama hizi zitaendelezwa hivi karibuni kwa kuupanua uwanja na kujenga jengo jengine la abiria. Utiaji taa katika njia ya kurukia ndege utaanza hivi karibuni.
Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,
Katika jitihada za kupunguza tatizo la usafiri wa baharini baina ya Zanzibar na Tanzania Bara na sehemu nyengine, Serikali imeshafunga mkataba na Kampuni ya Korea ya Kusini kwa ajili ya ujenzi wa meli mpya ya abiria ambayo itakuwa na uwezo wa kuchukuwa abiria 1,200 na mizigo tani 200. Meli hiyo inategemewa kufika nchini mwezi Juni, mwaka 2015.
Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,
Huduma za umeme ni miongoni mwa sekta muhimu kwa ajili ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Ingawa Zanzibar ni miongoni mwa nchi za mwanzo Barani Afrika kuwa na huduma za umeme, tangu mwaka 1880, lakini kabla ya Mapinduzi huduma hizo ziliishia katika baadhi ya sehemu za mjini Unguja tu, kwa wale waliokuwa na uwezo. Aidha, huduma hizo hazikuwa na mchango mkubwa katika kustawisha au kuinua hali za wanyonge. Ndiyo maana, mara tu baada ya Mapinduzi, tarehe 6 Juni, 1964, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilianzisha Shirika la Mafuta na Nguvu za Umeme ambalo hivi sasa linajulikana kwa jina la Shirika la Umeme la Zanzibar (ZECO). Lengo la shirika hili ni kusambaza huduma zake ili ziwafikie wananchi katika sehemu mbali mbali wanazoishi mijini na vijijini.
Mahitaji ya umeme kwa Zanzibar kabla ya mwaka 1980 yalikuwa ni Megawati 3.5 uliotokana na majenereta na umeme huo ulikuwa ukikatika katika na kusababisha matatizo mbali mbali na ndipo Serikali ikalazimika kununua waya wa umeme uliopitishwa chini ya bahari kwa kuunganishwa na gridi ya Taifa. Kiwango cha umeme cha waya huo kilikuwa ni Megawati 45.
Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,
Hivi sasa tunaposherehekea miaka 50 ya Mapinduzi Matukufu ya 1964, mafanikio makubwa yamepatikana kwa kuwa na kiwango cha umeme cha Megawati 100 kwa Unguja na Megawati 20 kwa Pemba. Mafanikio haya yamepatikana kwa msaada wa Serikali ya Marekani kwa Unguja na Serikali ya Norway kwa Pemba. Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zilichangia jitihada hizo. Kiwango hichi cha umeme kinapatikana kupitia waya uliolazwa baharini na kuunganishwa na gridi ya Taifa baina Ras Kilomoni na Fumba kwa Unguja na baina ya Tanga na Ras Mkumbuu kwa Pemba. Usambazaji wa umeme vijijini umefikia hatua kubwa sana na katika kipindi cha miaka mitatu (3) iliyopita usambazaji huu umefikia asilimia 87.5 ya vijiji vyote vya Unguja na Pemba. Hii ni hatua kubwa sana katika kuwapelekea umeme wananchi. Haya ni mafanikio makubwa yaliyofikiwa katika kuwahudumia wananchi walioko vijijini.
Waheshimiwa Viongozi na Ndugu Wananchi,
Katika sherehe hizi za miaka 50, tunafurahia mafanikio makubwa tuliyoyapata katika sekta ya Habari, Utamaduni na Michezo. Tumepiga hatua kubwa katika sekta ya habari, kwa kutekeleza malengo ya Mapinduzi katika kuwaelimisha wananchi. Sauti ya Tanzania Zanzibar ambayo ilipewa jukumu la kuifanya kazi hiyo, iliwapa wananchi habari za ndani na nje ya nchi na kuimarisha na kuamsha msimamo wao wa kisiasa. Katika nyakati tafauti, Serikali ilinunua mitambo ya redio ya kutangazia, muda wa matangazo uliongezwa na jengo jipya la kutangazia la Rahaleo lilijengwa. Hivi sasa Shirika jipya la Utangazaji la Zanzibar (ZBC) limeundwa na linatoa matangazo yake saa kwa 24 kwa Radio na Televisheni.
Ndugu Viongozi na Ndugu Wananchi,
Utamaduni wetu ni suala la msingi katika maisha ya kila siku ya watu wa Unguja na Pemba. Kwa hivyo, baada ya Mapinduzi ya 12 Januari, 1964, tunaendelea kuutunza na kuuendeleza utamaduni wetu. Tumeziimarisha sanaa na ngoma zetu za asili, lugha yetu ya Kiswahili na michezo. Mipango ya kuwakumbuka na kuwaenzi wasanii wetu waliovuma na kuipatia sifa Zanzibar kama vile Marehemu Bibi Siti binti Saad, Marehemu Bi. Fatma binti Baraka (Bi. Kidude), Marehemu Bwana Bakari Abeid imeandaliwa. Taasisi ya kumuenzi Mwanaharakati Bibi Siti binti Saad imeanzishwa na tarehe 7 Januari, 2014, ilizinduliwa rasmi.
Lugha ya Kiswahili inaendelezwa na hivi sasa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar, kinatoa elimu ya kiwango cha Stashahada na Shahada zote. Kadhalika, michezo inaendelea kuimarishwa na kushajiisha mazoezi ya viungo kwa makundi mbali mbali ili kuimarisha afya za wananchi. Natoa wito kwa wananchi wote wafanye mazoezi kwani ni muhimu kwa ajili ya afya zetu. Mazingira mazuri ya michezo yameimarishwa kwa lengo la kuwawezesha wanamichezo kushinda katika mashindano hayo.
Ndugu Viongozi na Ndugu Wananchi,
Wakati huu tunapoadhimisha miaka 50 ya Mapinduzi, tunajivunia mafanikio makubwa yaliyopatikana katika jitihada za Serikali za kuwahudumia wazee na hatua zinaendelea kuchukuliwa za kuziimarisha huduma zote muhimu kwa ajili ya maisha yao. Aidha, kwa azma ya kulinda haki za watoto, Serikali imeanzisha sheria mpya ya kumlinda mtoto ya mwaka 2011 na masuala ya vitendo vya udhalilishaji dhidi ya wanawake na watoto yanashughulikiwa na yamewekewa mikakati madhubuti.
Katika kipindi hiki tunafurahia mafanikio ya juhudi zetu za kupambana na umasikini kwa kuwawezesha kiuchumi vijana na kinamama. Jumla ya vikundi 257 vya Unguja na Pemba na wajasiriamali 1,738 wamewezeshwa kwa kupewa mikopo. Jumla ya TShs. milioni 2,344.7 zilitolewa kutoka kwenye mifuko iliyoanzishwa na Serikali. Jitihada hizi zitaimarisha upatikanaji wa ajira.
Vile vile, jitihada mbali mbali zimechukuliwa katika kuwasaidia watu wenye ulemavu. Mipango na mikakati imepangwa kupitia Idara ya Watu wenye Ulemavu na katika mwaka 2012, Serikali imezindua mfuko maalum wa kuwasaidia. Zoezi la kuwasajili watu wenye ulemavu limefanyika katika Wilaya mbali mbali ili uratibu wa shughuli zao ufanyike kwa ufanisi.
Kwa kuzingatia umuhimu wa masuala ya mazingira na jinsi yalivyopewa kipaumbele duniani kote, Serikali ilitunga sera ya mazingira ya 1992. Sera hii ilifanyiwa mapitio na sera mpya ilitungwa mwaka 2013. Sera hii inatilia mkazo elimu ya mazingira kwa wananchi, kuhusu umuhimu wa uhifadhi na utunzaji wa mazingira. Mapambano dhidi ya matumizi ya mifuko ya plastiki yameendelezwa na tani 288 za mifuko hiyo zimekamatwa na wahusika kuchukuliwa hatua. Miradi ya vitega uchumi hufanyiwa ukaguzi wa mazingira na miradi 160 ilikaguliwa. Suala la mabadiliko ya tabia nchi linashughulikiwa kwa kufanya tafiti za athari yake kwa uchumi wa Zanzibar na jumla ya maeneo 165 yaliyoingia maji ya chumvi yameorodheshwa. Hivi karibuni, kikosi kazi maalum kimeandaliwa ili kushughulikia maeneo yanayochimbwa mchanga, mawe na kifusi.
Pamoja na mafanikio makubwa ya kisiasa, kiuchumi na kijamii ambayo nchi yetu imeyapata, zipo changamoto nyingi ambazo zinatukabili katika kuiletea maendeleo nchi yetu. Changamoto kubwa inayotukabili ni namna gani tutaweza kuyatunza na kuyaendeleza mafanikio tuliyoyapata ambayo leo nimeyaelezea kwa furaha kubwa. Ni dhahiri kwamba jukumu letu ni kuhakikisha kwamba amani na utulivu ndio jawabu peke yake la kutatua changamoto hio na lazima tufanye kila jitihada ili tuiimarishe amani na utulivu kwa madhumuni ya kupata mafanikio zaidi.
Bila ya shaka yoyote, hali hiyo tutaifikia tu tukiwa makini, watiifu, waadilifu na tulioamua kuwa kwa maendeleo ya nchi yetu. Utiifu wa sheria ni hatua moja muhimu katika kuyafanikisha hayo. Ni jukumu la viongozi wote wa Serikali, wanasiasa, viongozi wa dini na viongozi wengine katika jamii, sote kwa pamoja tutekeleze wajibu wetu huo kwa kuhakikisha kuwa amani na utulivu vinadumishwa na sheria za nchi zinafuatwa. Ni wajibu wetu kuyalinda, kuyaenzi na kuyadumisha Mapinduzi yetu na kuuendeleza na kuudumisha Muungano wetu. Muungano wetu pamoja na Mapinduzi yetu ndizo nguzo zetu kubwa za maendeleo na ndivyo vilivyotufikisha hapa hivi sasa na ndivyo vitakavyotufikisha tunakokusudia kwenda katika miaka mingi ijayo.
Napenda niwahakikishie wananchi wote kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuendeleza Muungano wetu, kuuimarisha na kuwatumikia wananchi. Katika kuuimarisha Muungano wetu, sote tumetimiza wajibu kwa kutoa maoni yetu kwa ajili ya kuandaliwa Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tume ya Kuratibu Maoni ya Katiba Mpya imetimiza wajibu wake na imefanya kazi kubwa na tayari wamemkabidhi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Rasimu ya Pili ya Katiba kama sheria iliyoelekeza. Hatua zilizobakia nazo zitakamilishwa kwa kuzingatia sheria iliyopo ili hatimae tupate Katiba Mpya itakayoliongoza Taifa letu na kuimarisha Muungano wetu. Kwa mara nyengine tena nampongeza Mwenyekiti wa Tume hio Jaji Mstaafu Mheshimiwa Joseph Sinde Warioba na wajumbe wote wa Tume kwa kazi kubwa waliyoifanya, tena kwa wakati. Napenda nimshukuru na nimpongeze sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dk. Jakaya Mrisho Kikwete kwa kusimama imara katika mchakato wa upatikanaji wa Katiba mpya. Vile vile, nampongeza kwa kuutetea na kuuendeleza Muungano wetu na kwamba siku zote yuko tayari kuzizungumzia changamoto zinazoukabili Muungano wetu na kutafuta njia za kuzipatia ufumbuzi kila zinapotokea.
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuuendeleza na kuudumisha Muungano kwa manufaa ya nchi zetu mbili. Hivi sasa tumemaliza miaka mitatu tangu Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar yenye Muundo wa Umoja wa Kitaifa imeingia madarakani. Tumepata mafanikio ya kuridhisha, hata hivyo, bado ipo kazi kubwa mbele yetu ambayo inahitaji jitihada zetu za pamoja.
Napenda kuwahakikishia wananchi wote kuwa Serikali itaendelea kutekeleza wajibu wake wa kikatiba na sheria kwa kuilinda amani, utulivu, mali na maisha ya watu. Hivi sasa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iko salama na Zanzibar iko salama kutokana na kazi nzuri inayofanywa na vyombo vyetu vya Ulinzi na Usalama. Kwa hivyo, nchi yetu itaendelea kuwa salama wakati wote.
Kwa mara nyengine natoa shukurani, kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dk. Jakaya Mrisho Kikwete kwa kuwa nasi katika maadhimisho ya sherehe zetu za miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar. Vile vile natoa shukurani kwa wageni wetu Rais Yoweri Museveni wa Jamhuri ya Uganda, Dk. Ikililou Dhoinine, Rais wa Comoros na Mhe. Jiang Weixin Mjumbe anayemwakilisha Rais wa Jamhuri ya Watu wa China. Kadhalika natoa shukrani kwa viongozi wengine wote waliohudhuria walioko madarakani na waliostaafu. Shukurani maalum ziwaendee Makamu wa Kwanza wa Rais, Mheshimiwa Maalim Seif Sharif Hamad, Makamu wa Pili wa Rais, Mheshimiwa Balozi Seif Ali Iddi kwa ushauri wao wa kunisaidia kuiongoza Zanzibar. Zaidi ya hayo shukrani zangu nazitoa kwa nchi marafiki, Jumuiya za Kimataifa na Washirika wetu wa maendeleo na wote waliotuunga mkono katika kipindi cha miaka 50 na tukaweza kushirikiana.
Napenda niishukuru na niipongeze sana Kamati ya Halmashauri ya Sherehe na Maadhimisho kwa mwaka huu wa 50 wa Mapinduzi inayoongozwa na Makamu wa Pili wa Rais. Mnastahiki pongezi kwa kazi nzuri mloifanya katika kufanikisha sherehe zetu ambazo zilifana sana na zitaingia kwenye historia ya nchi yetu. Hongereni sana. Natoa shukurani maalum kwa makamanda na wapiganaji wetu wa vikosi vyote kwa namna walivyofanikisha sherehe hizi kwa gwaride lililopendeza pamoja na vijana wetu wa halaiki, mlivyotia fora.
Nawashukuru na nawapongeza wafanyakazi wote wa Serikali kwa jitihada zenu za kuwatumikia wananchi. Ni matumaini yangu kwamba mtaendelea kuongeza juhudi zenu ili tuweze kuyatekeleza malengo ya Dira 2020 ambayo hivi sasa tumebakiwa na miaka sita kabla ya kumaliza muda uliopangwa. Tujitahidi ili Zanzibar iwe miongoni mwa nchi zenye uchumi wa kati. Sote tudhamirie kwamba mwaka huu uwe wa kufanya kazi kwa bidii, ubunifu na nidhamu na tusifanye kazi kwa mazoea.
Namalizia kwa kutoa pongezi za dhati kwa wananchi wote kwa kushiriki katika shughuli mbali mbali za kusherehekea Mapinduzi yetu kutimiza miaka 50. Kwenu nyote nasema ahsanteni sana. Aidha, nawashukuru wale wote walioshiriki katika maandamano na waliotupa burudani. Vile vile, shukurani ziwaendee waandishi wa vyombo habari kwa kuzitangaza shughuli na sherehe zetu kwa ufanisi tangu pale tulipozizindua sherehe zetu tarehe 15 Agosti, 2013. Nasema hongereni sana.
MAPINDUZI DAIMA
MUNGU IBARIKI ZANZIBAR
MUNGU IBARIKI TANZANIA
MUNGU IBARIKI AFRIKA
Ahsanteni kwa kunisikiliza.