Na Jumbe Ismailly,Singida
DIWANI wa kata ya Unyambwa, manispaa ya Singida, Nd. Shaban Salum na wenzake, wameburuzwa katika mahakama ya Hakimu Mkazi mjini hapa,wakikabiliwa na shitaka la kuchoma moto basi la kampuni ya Mtei Express na kusababisha hasara ya shilingi milioni 70.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka iliyowasilishwa mahakamani hapo, washtakiwa wengine ni Salum Shaban (20), Hashimu Hamisi (20),Hassani Selemani (54) na Michael Andrew (30).
Wengine ni Ahmed Abdurahmani (24), Yassini Emmanueli (23), Shabani Hamisi (29), Japheth Eliakimu (38), Ally Mohammedi (29), Ally Japhari (19) na Shamushidini (32).
Mwendesha mashtaka, Mussa Chemu alidai Januari 9,mwaka huu saa 1:30 asubuhi katika kitongoji cha Ijanuka,kijiji cha Kisasida,washtakiwa wote kwa pamoja walichoma moto basi la kamapuni ya Mtei Express na hivyo kusababisha hasara ya shilingi milioni 70.
Mbele ya hakimu, Asha Mwetindwa,washtakiwa hao wote kila mmoja kwa wakati wake walikana kutenda kosa hilo na kesi hiyo,imeahirishwa hadi Januari 30 mwaka huu itakapotajwa tena.