Katibu Mkuu wa CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad akiwahutubia wafuasi na wapenzi wa chama hicho katika mkutano wa kampeni za udiwani uliofanyika kata ya Magomeni Wilayani Bagamoyo.
Katibu Mkuu wa CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad akimnadi mgombea udiwani kata ya Magomeni, Njema Seif Mohd, katika mkutano wa kampeni za udiwani uliofanyika kata ya Magomeni Wilayani Bagamoyo
Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Bara) Julius Mtatiro akiwahutubia wafuasi na wapenzi wa chama hicho katika mkutano wa kampeni za udiwani uliofanyika kata ya Magomeni Wilayani Bagamoyo.
Naibu Mkurugenzi wa Haki za Binadamu, Habari na Uenezi (CUF) Abdul Kambaya, akizungumza na wafuasi na wapenzi wa chama hicho katika mkutano wa kampeni za udiwani uliofanyika kata ya Magomeni Wilayani Bagamoyo.
Baadhi ya wakaazi wa kata ya Magomeni Wilayani Bagamoyo wakisikiliza kampeni za CUF zilizozinduliwa na Katibu Mkuu Maalim Seif Sharif Hamad. (picha na Salmin Said, OMKR)
Na Hasssan hamad , OMKR
Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, amefungua kampeni za uchaguzi wa udiwani katika kata ya Magomeni Wilaya ya Bagamoyo, na kuwanasihi wakaazi hao kutochagua viongozi wanaojihusisha na vitendo vya rushwa.
Amesema kiongozi atakayechaguliwa kwa kutoa rushwa, kamwe hatoweza kukemea vitendo hivyo na badala yake ataviendeleza na kuwaacha wananchi wakibakia katika hali ya umaskini na matatizo mengi katika maeneo yao.
Maalim Seif amewashauri wakaazi hao kusikiliza sera za wagombea wote, ili waweze kuzipima na kuzichambua na hatimaye kuchagua kiongozi atakayewajali na kusaidia kuwatatulia kero zinazowakabili.
Amesema mgombea wa CUF katika kata hiyo nd. Njema Seif Mohd, ameonesha dalili njema kwa kuwa mwaminifu na mtu anayewajali wenzake, na kuwataka wakaazi hao kutofanya makosa katika uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika tarehe 09 mwezi ujao.
Kwa upande wake, mgombea wa udiwani CUF katika kata hiyo ya Magomeni Wilayani Bagamoyo nd. Njema Seif Mohd ameahidi kusimamia matatizo yanayowakabili wakaazi hao kwa lengo ya kuyatafutia ufumbuzi.
Akitaja vipaumbele vyake amesema atasimamia suala la elimu ili kuhakikisha kuwa watoto wote wanakwenda skuli bila ya vikwazo vyovyote, pamoja na kusimamia upatikanaji wa vifaa vya hospitali ikiwa ni pamoja na madawa.
Aidha amesema atasimamia mapato ya halmashauri hiyo ili kuona kuwa yanatumika kama yalivyokusudiwa.
“Nichagueni tutetee Magomeni yetu”, alijinadi Njema.
Mapema Naibu Katibu Mkuu wa CUF Tanzania Bara Julius Mtatiro, alishutumua utendaji wa halmashauri hiyo na kudai kuwepo kwa matumizi mabaya ya fedha zinazotengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo.