Quantcast
Channel: ZanziNews
Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Dk Shein akutana na Waziri wa Fedha wa SMT pamoja na manaibu wake

$
0
0
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akizungumza na Waziri wa Fedha wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Saada Mkuya Salum,(wa pili kulia) pamoja na Manaibu wake Adam Kigoma Malima na Mwigulu Lameck Nchemba,(kushoto) walipofika kujitambulisha kwa Rais Ikulu Mjini Zanzibar leo.{Picha na Ramadhan Othman Ikulu].

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akizungumza na Waziri wa Fedha wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Saada Mkuya Salum,alipofika kujitambulisha na  Manaibu wake Adam Kigoma Malima na Mwigulu Lameck Nchemba,(hawapo pichani) walipofika kujitambulisha kwa Rais Ikulu Mjini Zanzibar leo.{Picha na Ramadhan Othman Ikulu].


STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
    Zanzibar                                                                    23 Januari, 2014
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein leo amekutana na Waziri wa Fedha wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Saada Mkuya Salum.

Waziri Saada alifika Ikulu kujitambulisha rasmi yeye na Manaibu wake Adam Kigoma Ali Malima na Mwigulu Lameck Nchemba kufuatia mabadiliko ya Baraza la Mawaziri yaliyofanywa hivi karibuni na Rais Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Jakaya Mrisho Kikwete ambapo mabadiliko hayo yaliigusa wizara hiyo.

Katika mazungumzo yake na Waziri huyo na ujumbe wake Dk. Shein alisisitiza umuhimu wa ushirikiano na utendaji kazi wa pamoja ili kukidhi matarajio ya Serikali pamoja na matumaini makubwa waliyonayo watanzania kwao.

Alieleza kuwa kukabidhiwa kwao kuiongoza Wizara hiyo yenye majukumu mazito na inayotegemewa na Serikali katika utekelezaji wa shughuli zake ni changamoto ambayo wanapaswa kuikabili kwa kudhihirisha weledi na uwezo wao kwa kufanya kazi kwa pamoja na kwa karibu ndani ya Wizara na kwa kushirikiana na Wizara nyingine.

Dk. Shein alieleza matumaini yake kuwa uongozi huo mpya wa Wizara utaendelea pia kufanya kazi kwa karibu na Wizara ya Fedha ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kutekeleza majukumu yake kwa mambo yanayozihusu Serikali zote mbili.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi amempongeza Waziri Saada na Manaibu wake kwa uteuzi huo na pia kuwashukuru kwa kuridhia uteuzi huo kitendo ambacho alikieleza kuwa kinadhihirisha dhamira yao ya kweli ya kuwatumikia wananchi.    

Naye Waziri wa Fedha Bibi Saada Mkuya Salum alimshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuwapa fursa ya kukutana nae ambapo wameweza kujifunza mengi kutokana na nahasa zake wakati wa mazungumzo hayo.  

Aliongeza kuwa ujio wake na timu yake umelenga sio tu kujitambulisha bali pia kuuhakikishia uongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuwa Wizara yake itaendelea kufanya kazi kwa ushirikiana na kwa karibu wakati wote.

Waziri Saada alibainisha kuwa anatambua kuwa Wizara hiyo inashughulikia pia masuala ya Muungano hivyo atahakikisha kuwa kunakuwepo na ushirikiano wa karibu na utekelezaji wa haraka wa malengo yaliyowekwa kwa manufa ya Serikali zote mbili.   

Mazungumzo hayo yalihudhuriwa pia na Katibu Mkuu Kiongozi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha ya Serikali ya Muungano wa Tanzania Dk. Servacius Likwelile, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Bwana Omar Mussa, Mkurugenzi wa Tawi la Benki Kuu ya Tanzania, Zanzibar Bwana Nicodemus Mboje na Meneja wa Utawala na Fedha wa Tawi hilo Bwana Mansour Abdalla.

Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822 
  E-mail: saidameir@ikuluzanzibar.go.tz & sjka1960@hotmail.com



Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>