Amuombea kura Mahmoud Thabit Kombo kwa wananchi wa Kiembesamaki
Na Andrew Chale, Zanzibar
BALOZI Ali Abeid Aman Karume ambaye pia ni MNEC wa Chama cha Mapinduzi CCM, Amesema Taifa linaitaji muundo wa Serikali mbili ilikuujenga Muungano thabitio uliasisiwa na viongozi wakuu ambao wameufikisha hapa ilipo sasa.
Balozi Ali Karume alisema hayo jioni ya leo (Januarin23) kwenye mkutano wa hadhara wa kumnadi Mgombea wa nafasi ya Uwakilishi kwa chama hicho kupitia jimbo la Kiembesamaki, Mahmoud Thabit Kombo, ambapo aliwataka wanakiembe samaki kumchagua mgombea huyo ilikwenda kuwatetea na kuwatumikia katika kuunda mambo mbalimbali ikiwemo suala hilo la Muungano na Serikali mbili.
Mkutano huo uliobeba umati mkubwa wa wananchi wa Kiembesamaki , ulifanyika kwenye eneo la ofisi ya CCM Chukwaani, ambapo pia uliudhuliwa na makada mbalimbali wa chama hicho.
Akielezea kwa kina juu ya Mapendekezo ya Rasimu ya pili ya Katiba, yenye mambo mbalimbali ikiwemo masuala ya mfumo wa serikali tofauti ya ‘Serikali tatu’, na ‘Serikali mbili’, Balozi Ali Karume alisema kuwa CCM inaunga mkono mfumo wa Serikali mbili na itapigania hilo mpka mwisho ikiwemo kuamasisha wananchi wake.
“Tunahitaji Katiba ya Serikali Mbili, hizo kelele nyingi munazozisikia hao hawajui hilo suala. Mimi nawaeleza kuwa, Tuchague Katiba yenye mfumo wa Serikali mbili kama wazee wetu walivyoweza kuipigania nchi hii na kufikia hapa ilipo” alisema Balozi Ali Karume.
Na kuongeza kuwa, Kupitia waasisi wa vyama vya siasa vilivyoipelekea nchi kuwa huru ikiwemo vyama vya ASP na TANU na baadae CCM, Wazee hao waliweza kuweka misingi imara ya uongozi na Serikali hiyo ya Muungano ndiyo iliyofanya Taifa kukua hadi leo hii kufikia hapa kwa umoja, usawa na mshikamano.
Akifafanua hilo, alisema ni heri Serikali mbili kwani, endapo Wananchi watataka vingine basi itatokea hali tofauti kwa kila mtu kudai Serikali yake. “ Endapo kila mtu atataka kuleta suala hili, walitakiwa kuliangalia kwa mapana yake na wananchi waamue. Maana itatokea ukienda Pemba na kuuliza “Munataka Serikali yenu, watakujibu ndiyo”, hivyo hivyo ukienda kule Kisiwa cha Tumbatu ukiwauliza munataka Serikali yenu lazima watajibu ‘Tunataka’, Pia hata ukienda pale Tomondo, ukiwauliaz wananchi munataka Serikali yenu, watajibu ‘ndiyo tunataka”, hivyo ni wakati wa kuangalia kwa mapana na pili kuwaenzi watawala wetu waliotutangulia kwani wao waliweza kuweka misingi imara na makini” alisema Balozi Ali Karume.
Na kuendelea kusema kuwa, CCM na wananchi wake watalipinga hilo la Serikali tatu, na zaidi watalidai la kuwa na Katiba ya Serikali mbili, kwani endapo wataliacha hilo, basi watatokea watu wachache ambao nao watadai Serikali zao. “ Watatokea kundi la watu wanataka Serikali ya Kikoloni?, wengine watataka Serikali ya kupigana tu na kila mmoja atadai Serikali yake, na nchi kuharibika, CCM hatutaki kuwa hivyo na zaidi tunataka kuimalisha Muungano wetu” alisema Balozi Ali Karume.
Hata hivyo aliwaeleza kuwa wananchi watambue hiyo Serikali tatu, imechanganywa ndani ya Muungano, kwani ni wakati wa kuendelea kuenzi Muungano ikizingatia zaidi ya Wazanzibar laki tatu wapo Bara na mambo mengine mengi yaliyowekwa na watawala waliopita.
“Wazanzibar tumewekeza Bara kwa vizazi, zaidi ya malaki ya wazanzibar wapo huko Bara, sasa uvunje Muungano na Serikali hiyo tatu, munadhani nini kitakachofuata?.. alihoji Balozi Ali Karume.
Kwa upande wake, Mgombea wa nafasi ya Uwakilishi wa jimbo hilo, Mahmoud Thabit Kombo aliwapongeza wananchi wa CCM wa Kiembesamaki kwa kujitokeza kwa wingi kwenye kampeni hizo ambapo aliwahidi kuwatimizia mambo mbalimbali pindi atakapopata nafasi ya kuwawakilisha kwenye Baraza la Wawakilishi.
“Umati huu unanipa faraja, hivyo nawaombeni kura zenu na ikifika Tarehe Mbili Mwezi wa Pili, siku ya Jumapili Saa Mbili, 2014, kura yako ya Ndiyo ni kwa Mahomoud Thabit Kombo”.
Akielezea changamoto wanazokabiriana nazo wananchi wa jimbo hilo hasa wakazi wa eneo la Chukwani, likiwemo suala la Barabara inayopitia Chukwani -Buyu , Mahmoud Thabit Kombo alisema atakapoopata nafasi ya kuingia kwenye Baraza la Wawakilishi, atahakikisha anambana Waziri wa Miundombinu kuhakikisha Barabara hiyo inajengwa kiwango cha lami.
“Wananchi wa Chukwani, natambua kero mbalimbali munazokabiriwa nazo, kubwa zaidi ni suala la hii barabara, nitahakikisha nitakapopata nafasi ya kuwawakilisha nitambana Waziri wa Miundombinu, ilikutenga fedha za kujengwa kiwango cha lami, na hadha ya vumbi na mambo mengine yatakwisha kabisa” alisema Mahmoud Thabit Kombo.
Na kuongeza kuwa, pia atahakikisha atatekeleza majukumu ya Ilani ya Chama na kama Mwakilishi pindi watakapomchagua, kwa kusaidia jamii masuala yote muhimu ikiwemo kwa Vijana, Akina Mama na jamii ya Jimbo hilo.
“Nitawawezesha akina Mama kupitia vikundi vyao vya Kijasiliamali na vya kujiendeleza na kwa vijana kwenye Nyanja mbalimbali ikiwemo michezo” alisema Mahoud Thabit kombo.
Mkutano huo wa Hadhara wa CCM kwenye jimbo hilo unakuwa wa pili, kufuatia wa kwanza uliofunguliwa Januari 22, kwenye uwanja wa mpira wa Kiembesamaki na Mjumbe wa Kamati Kuu na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Mohamed Gharib Bilal.
Aidha, CCM pia inatarajia kufanya mkutano wake wa tatu wa hadhara Januari 24, utakaofanyika eneo la Buyu Pwani, huku Mgeni rasmi akitarajiwa kuwa Ndugu Shaka Hamdu Shaka (MNEC) na Naibu Katibu Mkuu UVCCM Zanzibar.