Katibu Mtendaji wa Bodi ya Sensa ya Filamu ya Zanzibar, Suleiman Mbarouk Suleiman (kushoto) . akifafanua jambo kuhusu filamu ya MV spice Islander. Kulia ni Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania, Joyce Fissoo.
Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania, Joyce Fissoo(kulia) akifafanua jambo kuhusu filamu ya MV spice Islander . Kushoto ni Katibu Mtendaji wa Bodi ya Sensa ya Filamu ya Zanzibar, Suleiman Mbarouk Suleiman .Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania, Joyce Fissoo(kushoto) akipeana mkono na Mwakilishi wa kampuni ya kutengeneza filamu ya Steps, Moses Mwanyilo (kulia).Katibu Mtendaji wa Bodi ya Sensa ya Filamu ya Zanzibar, Suleiman Mbarouk Suleiman (kushoto) akipeana mkono kulia Mwakilishi wa kampuni ya kutengeneza filamu ya Steps, Moses Mwanyilo.
(Picha na Magreth Kinabo)
………………………………………………………………………………
Na Magreth Kinabo – Maelezo
Viongozi wa Bodi za Filamu wa Tanzania Bara na Zanzibar wametoa ushauri kwa wasanii nchini kuacha kutumia majanga halisi kwa ajili ya kutengenezea filamu Kibiashara.
Kauli hiyo imetolewa jana na viongozi hao , wakati wa kikao cha kati ya Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania, Joyce Fissoo na Bodi ya Sensa ya Filamu ya Zanzibar, Suleiman Mbarouk Suleiman na Mwakilishi wa kampuni ya kutengeneza filamu ya Steps, Moses Mwanyilo kilichofanyika jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika kikao hicho, Bi.Fissoo alisema kampuni hiyo imetengeneza filamu ya MV Spice Islander kwa kuchukua picha halisi za ajali ya MV spice,ambayo iliwasilishwa katika ofisi yake Novemba 2013 kitendo ambacho ni kinyume na sheria , taratibu na kanuni za utengenezaji wa filamu.
Alisema filamu hiyo ilichukua picha halisi ya ajali hiyo, hivyo ofisi yake ilimwandikia barua mtengenezaji huyo kuwa ibadilishwe, lakini aliomba ashiriki kikao na bodi. Hata hivyo aliitwa mara nne kwa ajili ya kikao na bodi hiyo lakini hakushiriki badala yake alileta marekebisho ya filamu hiyo mara tano ambayo bado yalikuwa na kasoro hizo.
Naye Bw. Suleiman alisema filamu hiyo ni muhimu . Hivyo alimtaka mtengenezaji huyo kutoingilia uhuru wa mtu, jamii na Serikali na kutaka filamu hiyo ifanyiwe marekebisho, hivyo ni vema wasanii wakawa wabunifu kutengeneza filamu zinazogusa bila kutumia uhalisia wa janga na majina halisi.
Aliipongeza bodi ya filamu ya Bara kwa ushirikiano waliouonesha kwa kuwa filamu ikataliwa Zanzibar na Bara inakataliwa kwani kazi kama hiyo iliwasilishwa Zanzibar na ilikataliwa kwa kuwa ajali iliyotokea si sherehe, bali itatonesha vidonda vya watu walioathirika.
Kwa upande wake mwakilishi wa kampuni hiyo alikiri kosa hilo na aliahidi kufanya marekebisho katika filamu hiyo.