“Inapofikia wasimamizi wa Kanuni za Chama wanapigwa vita ya wazi kwa uamuzi wao wa kukisimamia Chama, tafsir yake ni moja tu watu wanaowapiga vita hawakitakii mema chama chetu.”
Imetolewa na Paul Makonda.
Katibu wa Hamasa na Chipukizi.
“..Chama Cha Siasa chochote duniani hubomoka kutokana na migongano iliyokithiri ya muda mrefu. Uzoefu wa vyama vikubwa vilivyoporomoka umeonyesha hivyo! Chama lazima kidhibiti uchu wa madaraka wa baadhi ya viongozi wake na ndani ya serikali yake...” – Dr Eginald P. Mihanjo
“..Chama cha siasa ni itikadi. Chama cha siasa ni siasa kwa maana halisi ya neno lenyewe siasa –“siasa”. Ni mahali ambapo watu wenye madhumuni mamoja yaliyoainishwa waziwazi hukutana na kuwa kitu kimoja. Chama cha siasa sio mkusanyiko wa “majini dume yenye tamaa”, - majini ambayo yametanguliza mbele tamaa kufa na kupona-tamaa ya kutengeneza pesa au kupata vyeo kwa gharama yoyote! – Dr Bashir Ally
UTANGULIZI:
Hili ni tamko la vijana makini wa jumuiya ya umoja wa vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) kuunga mkono juhudi na utendaji wa sekretarieti ya halmashauri kuu ya Chama Cha Mapinduzi ikiongozwa na Katibu Mkuu Komredi Abdulrahaman Kinana.
Maneno ya utangulizi yamebeba dhima ya tamko hili, kufuatia taarifa zilizoripotiwa kwenye baadhi ya vyombo vya habari vikiwanukuu baadhi ya wanachama wa Chama Cha Mapinduzi,wakiwatuhumu Viongozi wa Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya CCM, Katibu Mkuu Ndugu Abdulrahaman Kinana na Katibu wa Itikadi na Uenezi Ndugu Nape Moses Nnauye.
Sisi Vijana tunatambua kuwa tuhuma hizo na maneno hayo ya hovyo yametolewa kwa nia ovu yenye kulenga kuwakatisha tamaa Viongozi hao wa Chama. Tunafahamu kuwa upo mkakati wa kiuhaini ulioandaliwa na kuratibiwa na “mtandao” ndani ya Chama ambao umejipanga kuendesha uhaini huo.
Sisi vijana wa UVCCM tunatambua na kuthamini juhudi za Katibu Mkuu na Sekretarieti yake katika kukijenga na kukiimarisha Chama kwa kuisimamia barabara misingi na shabaha ya kuundwa kwake, katika umri wetu hatukuwahi kuona Chama kikiwa karibu na wananchi kwa kufuatilia, kusikiliza na kushiriki katika utatuzi wa kero, shida na changamoto zao kama ilivyo katika kipindi hiki chini ya Comrade Kinana na timu yake. Juhudi hizi ni za kuungwa mkono na kamwe si za kubezwa na mwanaCCM muadilifu, muaminifu na mwenye mapenzi ya kweli kwa Chama.
Juhudi za kukiimarisha Chama kutoka ngazi za chini, kwa mabalozi ni mkakati bora kuwahi kutekelezwa na Chama, kukirudisha Chama kwa wanachama ni kutimiza lengo la kuundwa kwa Chama hiki, Chama hiki ni cha wanyonge, masikini wa Taifa hili, HAIWEZEKANI matajiri watake kukihodhi na waratibu mikakati ya kukihujumu kwa pesa zao hali sisi vijana tukitazama, tunasema tutakilinda Chama chetu na tutawalinda viongozi wetu waadilifu.
Ni hawa ambao wanabezwa leo ndio wameweza kurudisha Imani ya wananchi kwa Chama, Imani na matumaini ambayo tayari yalishaanza kupotea na Chama kuonekana si tena cha wanyonge, wakulima na wafanyakazi wa nchi hii.
Ni Comrade Kinana na timu yake ndio waliozunguka kwenda kukutana na wakulima wa Pamba kule mikoa ya Kanda ya ziwa na kumpeleka balozi wa China na kumshawishi kujenga viwanda ili kuboresha manufaa kwa wakulima.
Ni Comrade Kinana na timu yake ndio waliokwenda Kusini kukutana na wakulima wa Korosho na kushirikiana nao pamoja na bodi kutatua tatizo la Korosho.
Ni Comrade Kinana na timu yake ndio walioibua hoja na kero za wafugaji, walimu na wananchi kwa ujumla, na kuwataka viongozi wa Serikali kuhakikisha wanawajibika kwa wananchi walipa kodi wa Taifa hili.
Kupinga mafanikio ya Ziara hizo ni kupinga utetezi wa wanyonge.
Mtu anayebeza ziara hizo na kuwaita Viongozi waliozifanya waropokaji na wahuni wahuni ni mtu mjinga, mtu wa hovyo,hana maadili, asiyekipenda Chama, mhaini na mzandiki anayepaswa kuchukuliwa hatua kali za kinidhamu ili iwe fundisho kwa wengine.
TAMKO hili limezingatia wosia wa Baba wa Taifa, muasisi wa Chama Cha Mapinduzi Mwl Julius Kambarage Nyerere katika kitabu Chake TUJISAHIHISHE.
Imetolewa na Paul Makonda.
Katibu wa Hamasa na Chipukizi.