Na Hamad Hassan OMKR
Serikali ya Japan imesema itaendelea kushirikiana na Zanzibar katika jitihada zake za kujikwamua kiuchumi, kwa kuendelea kuunga mkono miradi ya maendeleo ikiwemo ya maji safi na salama, mijini na vijijini.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Japan bw. Norio Mitsuya ameeleza hayo wakati akizungungumza na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, nyumbani kwake Mbweni.
Amesema Japan na Zanzibar zina uhusiano wa kiuchumi wa muda mrefu, na umekuwa ukiimarika siku hadi siku kutokana na nia njema ya nchi hizo.
Bw. Mitsuya akiongoza ujumbe wa watu saba wa Japan, ametaja maeneo mengine wanayoweza kushirikiana na Zanzibar kuwa ni pamoja na sekta ya kilimo, uvuvi, utalii pamoja na kuwajengea uwezo vijana wasiokuwa na ajira.
Amesema Japan imekuwa na miradi mingi ya kuwezesha makundi ya vijana kimafunzo kwa nchi za Afrika, Tanzania ikiwa miongoni mwa nchi hizo, na kutaka itumiwe fursa hiyo kuwajengea uwezo vijana wa Zanzibar.
Akizungumzia kuhusu sekta ya utalii, amesema watalii kutoka Japan wameshajiika kuitembelea Tanzania ambapo idadi ya watalii wa nchi hiyo imeongezeka kutoka watalii 4000 hadi 5000 msimu uliopita.
Ametaja baadhi ya miradi wanayokusudia kuiendeleza katika kipindi cha karibuni ni pamoja na ujenzi wa soko la samaki katika eneo la Malindi, pamoja na kujenga skuli za msingi katika maeneo mbali mbali.
Aidha Mitsuya amesema wataendelea kushirikiana katika huduma za kilimo cha umwagiliaji, pamoja na kuwashajiisha wawekezaji binafsi kuja kuwekeza katika miradi tofauti ya kiuchumi.
Nae Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, amesema Zanzibar inathamini misaada inayotolewa na serikali ya Japan, na kuwashajiisha wawekezaji wa nchi hiyo kuja kuwekeza Zanzibar hasa katika miradi ya ujenzi wa hoteli za kisasa.
Amesema Zanzibar ina maeneo mazuri ya uwekezaji kwenye sekta hiyo, na kuelezea uwepo wa wawekezaji walioanza kuwekeza katika utalii wa daraja la juu kwa kujenga chumba cha chini ya bahari kisiwani Pemba, ambapo wageni kadhaa wameanza kukitembelea.
Kuhusu kilimo cha umwagiliaji, Maalim Seif amesema licha ya juhudi na mafanikio yaliyopatikana katika kilimo hicho, bado kuna safari ndefu na kufikia matarajio ya kilimo hicho kutokana na kuwepo kwa ekari nyingi ambazo hazijaweza kuendelezwa. Hivyo ametoa wito kwa washirika wa maendeleo kuendelea kujitokeza kuendeleza kilimo hicho.
Aidha ameiomba nchi hiyo kuangalia uwezekano wa kuchangia upatikanaji wa umeme wa uhakika Zanzibar, ili kuepuka kutegemea moja kwa moja nishati hiyo kutoka Tanzania Bara.
Amesema umeme wa uhakika ndio msingi mkuu wa uwekezaji kwa sekta mbali mbali zikiwemo utalii na viwanda, na kwamba iwapo Zanzibar itakuwa na uhakika wa umeme, wawekezaji wengi zaidi watazidi kujitokeza kuja kuwekeza.
Wakati huo huo Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar alikua mgeni rasmi katika maulid ya kusherehekea kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (SAW) yaliyoandaliwa na Madrasat Imani Islamiya ya Jang’ombe, na kutoa wito kwa wazazi na walezi kutumia hekima na busara katika malezi ya watoto.
Amesema wazazi na walezi wana nafasi kubwa ya kurejesha maadili bora katika jamii iwapo watarejesha utamaduni wa malezi ya pamoja, kupendana na kuacha kufarakana kwa mambo yasiyokuwa ya msingi.
Ameipongeza madrasa hiyo kwa mafanikio makubwa iliyopata, ikiwa ni pamoja na kuongeza idadi ya wanafunzi kutoka 12 mwaka 1995 hadi 192 mwaka huu.
Ameahidi kushirikiana na madrasa hiyo katika kutafuta namna ya kuzitatua kero zinazowakabili zikiwemo upungufu wa vyumba vya kusomea.
Katika risala ya madrasa hiyo iliyomwa na mwalimu Hassan Hassan (Hasanayni) wamesema wanakusudia kuijenga upya madrasa yao ya zamani, ili kutoa nafasi kwa wanafunzi zaidi kupata vyumba vya kusomea, na kuwaomba wafadhili kujitokeza kuchangia ujenzi huo.
Hassan Hamad, OMKR