Quantcast
Channel: ZanziNews
Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

MAFAO YA WABUNGE KUFURU… Milioni 160 kwa kazi gani?

$
0
0

Na Salim Said Salim
INASADIKIWA kama inavyosadifu kutoka kwenye mabaraza ya nchi mbalimbali, kwamba baadhi ya wabunge (wawakilishi wa wananchi) wametawaliwa na ubinafsi, hususan panapokuwa na masilahi yanayowahusu.
Imeshuhudiwa nchi jirani ya Kenya, wabunge walijiongezea mafao ya kumaliza muhula wa Bunge wa miaka mitano hali iliyosababisha wananchi wa Kenya kuandamana kupinga mafao hayo!
Hata hivyo, kwa nguvu ya kura za wabunge, hoja ya kuongeza mafao ya wabunge ilipitishwa.
Nilidhani wakati ule nilipokuwa nikifuatilia masuala ya mafao ya wabunge wa Kenya, kwamba wabunge wa Tanzania hawatafuata ‘nyayo’.
Nilikuwa najidanganya! Yaleyale yaliyofanywa na wabunge wa Kenya ndiyo yanayotokea hapa Tanzania. Ama kweli ukiona mwenzako ananyolewa na wewe tia maji chako kichwa.
Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977 (Toleo la 2005), Bunge ni chombo kikuu kilichopewa madaraka kwa niaba ya wananchi, kuisimamia na kuishauri serikali na vyombo vyake vyote katika utekelezaji wa majukumu yake kwa mujibu wa katiba (tazama Ibara ya 63(2) kwa ufafanuzi).
Kwa maana hiyo, Bunge, pamoja na mambo mengine lina kazi mbili; yaani, kuisimamia serikali na kuishauri serikali.
Kumbe ubunge ni kazi! Binafsi nilikuwa sifikirii kwanini baadhi ya wanasiasa hupigana vikumbo na kunyukana majimboni kutafuta ubunge.
Kumbe kazi ya ubunge inalipa kiasi hiki! Kweli, ukistaajabu ya Musa (kugeuza fimbo kuwa nyoka) utayaona ya Firauni (aliyejiita Mungu ilhali alishindwa kuizuia Bahari Nyekundu isimzamishe na kufa humo)
Wabunge wetu wamepoteza utukufu wa Bunge na sasa wamegeuza baraza hilo kuwa kilinge cha kutetea masilahi binafsi.
Shilingi milioni 160 za mafao ya baada ya kustaafu ni kufuru kubwa kwa maisha ya wananchi kwa kuwa ubunge si kazi ya kipato isipokuwa ni kazi ya kuwatumikia wananchi.
Mada hii imeandikwa kwa uchungu kutokana na ushahidi wa juu ya mafao yaliyoainishwa na kunukuliwa na vyombo mbalimbali vya habari juu ya wabunge ‘kujipendelea’ na kujiongezea mafao yanayokadiriwa kuwa shilingi milioni 160 kwa kila mbunge.
Japokuwa mafao hayo kwa wabunge yanaweza kuonekana ‘kiduchu’ kutokana na uchu, uroho au umero wa baadhi ya wabunge wenye ushawishi katika upitishaji wa sheria zenye masilahi ya upande mmoja pasipo kuzingatia uadilifu na insafu ya kuwatumikia wananchi kwenye njia ya kuwafanya waamini kwamba Bunge lipo kwa masilahi ya wananchi; badala yake, na kwa hili la mafao limelifanya Bunge letu kuonekana la kimasilahi zaidi.
Kama tutatumia ukokotozi rahisi; tufanye hivi: sh milioni 160 ukizigawa kwa miaka mitano ya ubunge unapata sh milioni 32 kwa mwaka kama mafao ya mbunge.
Shilingi milioni 32 ukizigawa kwa siku 365 unapata sh 87,671.23 kwa siku ambazo ni sawa na sh 3,652.96 (kwa makadirio ni 3,653) kwa saa.
Kwa jinsi hii, saa moja ya kuwa mbunge ni sawa na sh 3,653 za mafao ya ubunge kwa ukokotozi huu bila ya kuzingatia kwamba katika saa hilo mbunge amefanya nini chenye kuweza kulipwa.
Hii ndiyo haki ya kuwa mbunge kwenye Bunge la wananchi maskini kama wa Tanzania, siyo?!
Inatia shaka kubwa nia na dhamira ya wabunge kama kweli walitafuta uwakilishi kwa kuwakilisha wananchi ambao kwa maisha yao kijamii na kiuchumi ni duni huku wakibebeshwa mzigo mzito wa ‘Deni la Taifa.’
Wabunge wetu wameshindwa kuisimamia na kuishauri serikali juu ya matumizi mazuri na endelevu ya rasilimali za taifa katika kupunguza deni hili na hatimaye kuwaletea wananchi maisha bora.
Sidhani kama madhumuni ya wabunge kupitisha sheria ya kujiongezea mafao yalizingatia utashi halisi wa maisha ya watu wanaowakilishwa kwa jinsi ya kuweka mizania ya haki na usawa kwenye mchakato wa maisha ya kila mtu na wajibu wake.
Wabunge hawa si wale walioshindwa kuisimamia serikali kushughulikia masilahi ya wafanyakazi pamoja na kuwatelekeza madaktari walipogoma wakidai nyongeza ya mishahara?
Au, wabunge hawa si walewale waliowaacha walimu wa Tanzania wakipigwa kumbo la zuio la kugoma lililotolewa na mahakama kwa niaba ya serikali na matokeo yake tunashuhudia mgomo baridi unaoididimiza elimu ya Tanzania?
Je, kama wameshindwa kusimamia urekebu wa mishahara isiyokidhi haja ya wafanyakazi wa Tanzania na mafao yasiyozingatia thamani ya fedha yanayotolewa na mifuko ya hifadhi ya jamii kama PPF, kwanini wao wamejiongezea mafao?
Huu ni ubinafsi kayaya wa wabunge. Japokuwa kujipendelea ni sifa ya kimaumbile; mtu yeyote mwenye sifa ya kujipendelea hafai kuwa mwakilishi wa watu, kwakuwa mwakilishi wa watu lazima ajitoe mhanga kuwatumikia watu.
Kwa hili la mafao, kwa ujumla wake, siungani na wabunge kwa vyovyote viwavyo hadi pale itakapothibitishwa vinginevyo kwamba wabunge walikuwa na nia njema ya kujiongezea mafao ilhali wameshindwa kuwatetea wafanyakazi wa Tanzania wapate mafao yanayokidhi thamani halisi ya fedha.
Siamini kama wabunge wameshindwa kuwatetea wafanyakazi wa Tanzania wanaoteseka na maisha ya kutegemea mishahara ambayo haikidhi maisha ya kiuchumi; na sidhani kama wabunge hawatambui mazingira magumu yanayowakabili wakulima maskini wa Tanzania wanaonyanyasika na bei za mazao na au kukopwa mazao yao huku wakopaji wakitumia kivuli cha sheria zilizotungwa na Bunge kama vile ‘stakabadhi ghalani’ na mifumo mingine ya kibaguzi na uonevu kwa wakulima.
Haijalishi, wabunge kwa hili wamepoteza ‘utukufu’ wa Bunge na wameharibu mujtamaa wao mbele ya macho ya wananchi maskini wa Tanzania.
Wabunge wameonyesha kushindwa kudhibiti ubinafsi wao. Wabunge wameonyesha sura halisi ya kujipendelea.
Nchi ya Tanzania inakabiliwa na deni kubwa la taifa linaloongezeka kwa mwendo wa kuchupa; pamoja na ukweli huu, hakuna jitihada za makusudi za wabunge kuishauri serikali jinsi ya kukabiliana na deni hili.
Wabunge wengi wanaitazama 2015 huku wakitamani wapate milioni 160 ili wazitumie kwenye kinyang’anyiro cha kurudi tena bungeni. Huu ni mtazamo wa kipumbavu.
Kama wabunge wamejisahau au wamewafanya wananchi wa Tanzania kama watu wa kudanganywa muda wote; napenda kuwatahadharisha kwamba mchezo wa kutumia nafasi yao ya kufanya maamuzi yenye taathira ya upendeleo itawaangamiza kisiasa.
Wananchi wametanabahi sasa kuliko ilivyokuwa zamani; fikra za wananchi wengi zamani zilikuwa zikiamini juu ya ‘jamii ya watu walio sawa na huru.’
Siku hizi wananchi wengi wana uwezo mkubwa wa kuhoji japokuwa hoja zao zinazimwa na utaasisi na uhafidhina wa baadhi ya watu wanaodhaniwa kuwa na ushawishi kwenye taasisi za kisiasa; utafika wakati, ujinga hautatumika kuwadanganya wananchi.
Wabunge wanahitaji tafakuri mpya juu ya dhana ya kujinufaisha wao kwa kazi ya ubunge; kinyume chake, kuna hatari ya kuliweka taifa kwenye sokomoko la kimasilahi kwa kuwa kila mtu anahitaji mafao bora na yanayokidhi haja ya maisha yake kiuchumi na kijamii.
Suala hili likiachwa liendelee kama lilivyo, kuna hatari ya wananchi kupoteza thamani ya uwakilishi na wabunge wataonekana au kuchukuliwa kama wasaka tonge.
Hii itakuwa sifa mbaya kwa wabunge. Wabunge jichunguzeni dhamiri na nia zenu na jitahidini kurudisha hadhi na heshima yenu, acheni tamaa ya mafao kwa kuiga mila na desturi za mabunge ya mabwanyenye.
Chanzo : Tanzania Daima

Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>