Na Madina Issa
BARAZA la Maalumaa Zanzibar limesema pamoja na walimu wa madrasa kulalamikiwa kuhusika na vitendo vya kuwadhalilisha na kuwabaka wanafunzi wao, imebainika vitendo hivyo fufanywa zaidi katika mazingira ya skuli.
Taarifa iliyotolewa na baraza hilo na kusainiwa na Katibu wa Mufti, Sheikh Suleiman Soraga, imesema wajumbe walitoa mifano ya baadhi ya walimu kuhusika kuwadhalilisha na kuwabaka wanafunzi wao na hakuna hatua zilizochukuliwa.
Hivyo, alisema baraza limewataka wajumbe kukusanya taarifa hizo kwa undani ikiwa ni pamoja na kuwabaini walimu wanaofanya hivyo, skuli wanazofundisha na wanafunzi waliohusika.
Aidha baraza hilo limelaani vikali juu walimu wa madras kuhusishwa na vitendo hivyo hasa kwa kuzingatia kwamba wao ndio walezi wa watoto.
Kuhusu mashindano ya kusaka mrembo wa kiislamu duniani, taarifa hiyo imesema wanaadamu wote wameumbwa katika maumbile mazuri na hakuna mantiki ya kushindanishwa.
“Baraza linatahadharisha jamii ya Wazanzibari kuwa na tahadhari na kuhakikisha mashindano kama hayo hayafanyiki Zanzibar,” alisema.
Aidha baraza hilo limewaomba wajumbe waliohudhuria kikao hicho kukusanya taarifa hizo kiundani zaidi ili waweze kubaini walimu wanaohusika, skuli zao pamoja na wanafunzi waliofanyiwa kitendo hicho.
Taarifa hiyo ililaani kufanyika mashindano ya mavazi kwa wasichana wa Kizanzibari yaliyofanyika hivi karibuni na kurushwa na kituo kimoja cha televisheni hapa Zanzibar .
Kuhusu ongezeko la talaka, baraza lilikubaliana kwamba talaka zimekuwa nyingi hali iliyosababishwa na upungufu wa subra kwa wanandoa, upungufu wa elimu ya ndoa na talaka na kukosekana uchamungu.
Baraza lilipendekeza Makadhi wanaofungisha ndoa waongezee katika hutuba zao juu ya wanandoa kujiepusha kuachana bila sababu za msingi.
Pia baraza lilipata nafasi ya kumsikila mwanamke mmoja mkazi wa Kivunge anaedai kuwa hujiwa na kiumbe mwenye mbawa (malaika) ambae kwa maelezo yake anadai ni Malik.
Baraza hilo limesema hakuna malaika atakaeshuka katika zama hizi kwa kiumbe wa kawaida kama mama huyo anavyodai.
Hata hivyo, baraza lilipomuuliza mama huyo kwamba anafanya ibada ya sala, alijibu hatekelezi na kwamba baraza likasema huyo ni shetani anaetaka kumpotosha hivyo kumtaka aanze kusali.