Quantcast
Channel: ZanziNews
Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Sekta za Utalii Zanzibar na India kushirikiana

$
0
0

STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY

PRESS RELEASE

    Zanzibar                                                                   10 Februari, 2014

---

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Katika kuhakikisha kuwa Zanzibar inavutia watalii wengi kutoka nchini India Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeamua kushirikiana na wadau wa sekta ya utalii nchini humo kuitangaza Zanzibar katika biashara ya utalii.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein katika mkutano wake na mawakala wa safari za ndege na mashirika ya biashara ya utalii uliofanyika mjini Mumbai alisema kuwa Serikali inaamini kuwa utaalamu na uzoefu walionao katika biashara hiyo utakuwa msaada mkubwa kwa Zanzibar katika kuitangza kama kituo cha utalii duniani.

Aliongeza kuwa ndio maana katika ziara yake nchini humo alipendekeza kuonana na wadau katika sekta hiyo kuzungumza na kubadilishana mawazo ili kuona ni namna gani Zanzibar inaweza kutumia uzoefu na utaalumu wa India katika kuimarisha sekta ya utalii nchini.

Kwa hiyo aliahidi kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo itaualika ujumbe wa watu kumi wa wawakilishi wao kutembelea Zanzibar ili kuifahamu vizuri Zanzibar na vivutio vyake pamoja na kuanzisha  mawasiliano ya moja kwa moja na wadau sekta hiyo Zanzibar.


Aliwaeleza kuwa kwa mujibu wa Mkakati wa Kuinua Uchumi na Kupunguza Umasikini nchini-MKUZA sekta ya utalii ni sekta mama ambayo kwa sasa inachangia asilimia 27 ya pato la taifa na asilimia 80 ya fedha za kigeni hivyo Serikali imekuwa ikifanya kila jitihada kuimarisha sekta hiyo ili iweze kuongoza uchumi wa nchi na kufikia lengo la Dira ya Zanzibar 2020 ya kuifanya Zanzibar kuwa nchi ya kipato cha kati ifikapo mwaka 2020.

Hivyo aliwaeleza washiriki wa mkutano huo kuwa mkakati wa Serikali hivi sasa ni kuongeza idadi ya watalii wanaoitembelea Zanzibar kutoka watalii wapatao 170,000 hivi hadi watalii 500,000 ifikapo mwaka 2020.

Dk. Shein alisema kuwa anaamini kuwa wananchi wengi wa India na nchi nyingine za Bara la Asia wangependa kutembelea Zanzibar lakini bado hawaifahamu vyema hivyo ushirikiano kati ya wadau wa sekta hiyo nchini India na Zanzibar ni muhimu katika kuitangaza Zanzibar ili kuchangia kufikia lengo la watalii 500,000 ifikpo mwaka 2020.

Mara baada ya mkutano huo Dk. Shein alifanya mazungumzo tofauti tofauti na baadhi ya wawakilishi wa makampuni ya Utalii ambayo yalikubali kushirikiana na Serikali katika kuitangaza Zanzibar katika biashara ya utalii.

Katika mazungumzo hayo ilikubaliwa kuwa kuwepo na mawasiliano ya moja kwa moja kati ya taasisi zinazoshughulikia utalii nchini na mashirika hayo ili kuweka mikakati ya pamoja ya ushirikiano ikiwemo kufikia makubaliano rasmi ya ushirikiano kati yao.   

Dk. Shein alimaliza ziara yake ya kikazi ya siku tisa nchini India jana na anatarajiwa kurejea nyumbani leo mchana.      

Katika ziara hiyo Dk. Shein alifuatana na Mke wake Mama Mwanamwema, Waziri wa Fedha Omar Yusuf Mzee, Waziri wa Uwezeshaji, Ustawi wa Jamii, Vijana, Wanawake na Watoto Bibi Zainab Omar Mohamed, Waziri wa Biashara na Viwanda na Masoko Nassor Ahmed Marzui, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Dk. Mahadhi Juma Maalim na Balozi wa Tanzania nchini India Injinia John Kijazi.

Wengine ni Katibu Mkuu Wizara ya Afya Mohamed Saleh Jidawi na Katibu Mkuu Kilimo na Maliasili Affan Othman Maalim, Mshauri wa Rais Ushirikiano wa Kimataifa, Uwekezaji na Uchumi Balozi Mohamed Ramia na Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Uwekezaji Zanzibar –ZIPA Salum Khamis Nassor.

   






Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822 


Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>