Na Hassan Hamad, OMKR
WAZAZI na walezi wameaswa kuacha tabia ya kuwaogopa watoto wao na badala yake wawaongoze katika malezi yenye kufuata maadili mema.
Wito huo umetolewa na mke wa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, mama Awena Sinani Massoud, wakati akizungumza katika hafla ya maulid ya kuzaliwa Mtume Muhammad (SAW), yaliyoandaliwa na Madrasat Azhar ya Tomondo kiziwa maboga.
Alisema tabia iliyozuka kwa baadhi ya wazazi kuogopa kuwakanya watoto wao ni hatari na inapaswa kupigwa vita.
Aidha aliwaomba wazazi kufuatilia maendeleo ya watoto wao katika madrasa, ili kubaini iwapo wanafahamu ipasavyo au wanahitaji nguvu ya ziada katika kuwasomesha.
Aliwakumbusha wazazi kuwazoesha watoto kuwa na subra na kutosheka na kile wanachopata kwa mujibu wa uwezo wa wazazi au familia zao.
Alisema iwapo utamaduni huo utaendelezwa, vijana wengi watazoea hali ya maisha waliyonayo na kuacha tamaa ya kuiga au kutamani baadhi ya vitu wasivyokuwa na uwezo navyo.
Aliwahimiza waislamu kuendelea kuzinduana juu ya mambo ya kheri na yale yanayomchukiza Mwenyezi Mungu, ili kulinda hadhi ya uislamu duniani.
Katika risala yao kwa mgeni rasmi, walimu na wanafunzi wa madrasa hiyo walisema wanakusudia kuanzisha skuli ya maandalizi ya kiislamu katika eneo hilo, lakini bado wanakabiliwa na tatizo la eneo la kujenga skuli hiyo.