HOTUBA YA MAKAMU WA PILI WA RAIS WA ZANZIBAR
MHE. BALOZI SEIF ALI IDDI - KUADHIMISHA SIKU YA SHERIA
(LAW DAY) ZANZIBAR, VICTORIA GARDEN
TAREHE 10 FEBRUARI, 2014
Mheshimiwa Jaji Mkuu wa Zanzibar,
Mheshimiwa Spika wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar,
Mheshimiwa Jaji Kiongozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mheshimiwa Waziri wa Katiba na Sheria,
Mheshimiwa Mwanasheria Mkuu,
Mheshimiwa Jaji Mkuu Mstaafu wa Zanzibar, na Majaji wa Mahakama Kuu,
Mheshimiwa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Jinai Zanzibar,
Mheshimiwa Rais wa Chama cha Mawakili Zanzibar (ZLS),
Wageni Waalikwa,
Mabibi na Mabwana.
Assalam Alaykum,
Tumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia uzima tukaweza kukutana hapa kwa ajili ya kuadhimisha Siku hii muhimu ya Sheria Zanzibar. Aidha, namshukuru Mheshimiwa Jaji Mkuu wa Zanzibar pamoja na uongozi wake wote kwa heshima mliyonipa ya kuwa mgeni rasmi katika sherehe za mwaka huu. Ahsanteni sana.
Napenda na kuwashukuru wale wote waliofanikisha sherehe hizi wakiwemo wasoma utenzi, wasanii wa Black Root Investment chini ya gwiji la sanaa Ndugu Makombora pamoja na wananchi kwa mahudhurio yenu.
Mheshimiwa Jaji Mkuu na wageni waalikwa,
Leo ni siku ya Sheria hapa Zanzibar. Leo pia ni siku ya kunukuu, Waheshimiwa Majaji na Wanasheria hupenda sana kuzungumza kwa kunukuu nukuu. Ili kula sahani moja na Waheshimiwa hawa, napenda kuanza hotuba yangu kwa kunukuu maneno yaliyosemwa na Mwanasheria Mkuu wa 64 wa Serikali ya Marekani, Bwana Robert Francis Kennedy:
“Respect of the law, in essence, that is the meaning of law day. And everyday must be law day or else our society would collapse”
Kwa tafsiri isiyo rasmi Bwana Robert anasema;
“Utii wa sheria kimsingi ndio hasa maana ya siku ya sheria. Kwa hivyo basi, kila siku lazima iwe siku ya sheria vyenginevyo jamii yetu itaangamia”
Maneno haya ya Mwanasheria Mkuu wa Marekani tukiyazingatia kwa umakini yanaweza kutusaidia kutafsiri kwa vitendo kauli mbiu tuliyojiwekea mwaka huu isemayo:
“SAIDIA MAHAKAMA KUTENDA HAKI”.
Waheshimiwa, Wageni Waalikwa,
Katika suala zima la kusaidia Mahakama kutenda haki kuna umuhimu mkubwa kwa wadau husika kushiriki, ikiwemo Mahakama yenyewe kuwa mstari wa mbele. Hapa napenda kunukuu msemo maarufu wa kizungu usemao: Self help is the best help (msaada mzuri ni ule unaotokana na wewe mwenyewe). Wakati kuna wajibu kwa wadau wengine kama Polisi, Mahakimu na kadhalika kuzisaidia mahakama kutenda haki, Mahakama nazo hazina budi kujisaidia zenyewe kwa kuhakikisha zinaendeshwa na Majaji na Mahakimu wenye kufuata maadili ya kazi zao. Ni vyema tukaelewa kuwa Mahakama na sheria ni mali za wananchi na vipo kwa ajili ya kukidhi mahitaji yao.
Kwa kuwa leo ni siku ya kunukuu, napenda kunukuu tena maneno yaliyosemwa na Mwanasheria maarufu wa Kiingereza Lord Denning:
“When a judge sits to try the case he himself is on trial before his fellow countrymen. It is on his behavior that they will form their opinion of our systems of justice”.
Kwa tafsiri isiyo rasmi Lord Denning anasema: “Wakati Jaji anapohukumu kesi ni sawa na kuwa yeye mwenyewe pia anahukumiwa na wananchi wenzake. Tabia zake ndizo zitakazowapelekea wananchi kuwa na maoni kuhusu mifumo yetu ya sheria”. Kwa bahati mbaya wapo baadhi ya mahakimu wetu wameweka kando maneno haya ya busara ya Lord Denning na ndio maana baadhi ya mahakama zetu zinalalamikwa na wananchi kwa kutokutenda haki. Ni jukumu la Mahakama kujisaidia yenyewe kwa kutenda haki kwa kutumia utaratibu wake wa kuwaondoa Mahakimu wasiofuata maadili ya taaluma zao.
Mheshimiwa Jaji Mkuu na Wageni Waalikwa,
Mdau mwengine anayeweza kusaidia Mahakama kutenda haki ni watu wenye kesi. Mahkama ina ubia mkubwa na wenye mashauri ya madai. Mahkama inapaswa kulishughulikia shauri lolote linalosajiliwa hata kama linaudhi (vexatious). Wenye mashauri watasaidia utendaji haki kwa wakati wakiheshimu sheria na taratibu, wakizingatia muda uliowekwa kisheria kwa kila tukio ndani ya shauri kufanyika, wakileta mashahidi wao ndani ya muda waliopangiwa, wakiteua wasimamizi wa mirathi mapema iwezekanavyo na wakiepuka kusababisha uakhirishwaji wa kesi usio wa lazima. Wito wangu ni kuwataka wenye mashauri kuwa makini zaidi (diligent) kwenye uendeshaji wa mashauri yao.
Mawakili wa kujitegemea pia ni wadau wakubwa wa Mahkamani, kwani wao ndio wanaowawakilisha na kuwasimamia wenye mashauri mahkamani. Pamoja na jukumu hilo la kuwakilisha wateja wao lakini pia wao kama maafisa wa mahkama wanalo jukumu kubwa la kusaidia mahkama kutenda haki tena kwa wakati. Mahakimu ni vyema kujielewa kuwa wao ni watumishi wa umma. Wapo kwa ajili ya kuwatumikia wananchi na sio vyenginevyo.
Mdau mwengine ni Jeshi la Polisi. Huyu ni mdau muhimu katika kuhakikisha haki inatendeka na kwa wakati. Polisi ndiyo wanaokamata watuhumiwa wa uhalifu na kuwahoji na ndipo kesi inapelekwa mahkamani. Kwa mujibu wa sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya 2004 pamoja na maamuzi mbali mbali ya Mahkama ya Rufani mshtakiwa anatakiwa kuhojiwa na kuchukuliwa maelezo yake ndani ya kipindi cha masaa manne(4) toka kukamatwa kwake.
Aidha, kwa mujibu wa sheria hiyo hiyo upelelezi unatakiwa ukamilike ndani ya miezi minne tokea shauri linapofikishwa mahkamani isipokuwa kwa makosa makubwa kama ya mauaji ambapo upelelezi unatakiwa ukamilike ndani ya miezi tisa.
Pia mshtakiwa anatakiwa afikishwe mahkamani katika kipindi kisichozidi masaa 48 tokea akamatwe. Kwa ufupi, lengo la sheria hizi ni kuhakikisha kwamba mtuhumiwa anafikishwa mahkamani mapema baada ya kukamatwa na kushtakiwa na kesi yake inapaswa kushughulikiwa mapema iwezekanavyo. Sasa tujiulize hivi kweli Jeshi letu la Polisi linayatimiza hayo? Mbona kila siku tunasikia nyimbo za upelelezi haujakamilika? Jeshi la Polisi liwe makini katika upatikanaji wa haki mapema.
Chuo cha Mafunzo nae ni mdau muhimu katika utendaji haki. Chuo kina jukumu la kuwafikisha mahabusu mahkamani. Hivyo wanatakiwa kuwafikisha kwa wakati na bila kukosa kila wanapotakiwa na mahkama kuhudhuria kesi zao. Jambo hili husaidia kesi kusikilizwa kwa wakati.
Ofisi ya Mwanasheria Mkuu na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini ni wadau muhimu sana katika kufanikisha utendaji haki kwa wakati. Ofisi hizi ndizo zinazoiwakilisha Serikali kwenye kesi Mahkamani. Wanasheria wa Serikali huiwakilisha Serikali katika kesi za madai zile ambazo Serikali imeshtaki au imeshtakiwa chini ya maelekezo ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na pia Wanasheria wa Serikali huendesha kesi za jinai mahkamani chini ya maelekezo ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini. Maamuzi na umakini wao huongeza kasi ya utendaji haki kwa wakati.
Mdau mwengine ni Baraza letu Tukufu la Wawakilishi ambalo ndilo lenye mamlaka ya kutunga sheria. Mchango wao kwenye utendaji haki kwa wakati ni kwenye kutunga sheria zinazochangia uendeshaji mashauri. Kwa wakati kama ilivyowekwa muda wa upelelezi katika kesi za jinai. Mchango mwengine wa Baraza la Wawakilishi ni kutunga sheria zinazoeleweka kwa urahisi na wananchi.
Siwezi kuwasahau wananchi kama wadau muhimu. Maoni na hisia za watu juu ya haki na vyombo vya Haki za Jinai unachangia na kuleta mageuzi kwenye utendaji haki. Utii wa sheria na wa amri za mahkama husukuma gurudumu la haki. Bila kusahaulika wadau wengine ni mashahidi, wazee wa Baraza, Madalali, vyombo vya habari na mashirika ya kiraia.
Mheshimiwa Jaji Mkuu,
Natambua kuwa Serikali ni mdau mkubwa tena ni muhimu katika utendaji wa haki tena kwa wakati, kwa upande wake Serikali itahakikisha kuwa watendaji wazuri wa Taasisi zake zinazosimamia sheria wanapatikana, maslahi bora yanapatikana; vitendea kazi vya kuridhisha vinapatikana; na bajeti yenye kukidhi mahitaji ya uendeshaji wa Taasisi hizo, kwa lengo la kuongeza ufanisi nayo inapatikana.
Mheshimiwa Jaji Mkuu na wageni waalikwa, napenda kuziomba Taasisi zote za sheria zilizokuwepo hapa kwamba tufanye kazi kwa uadilifu mkubwa na kufuata maadili ya kazi zetu kwani wananchi ambao ndio walipa kodi wetu wanalalamikia utendaji wetu. Hivyo tuondoshe tamaa na muhali katika kazi. Tukifanya hivyo tutapiga hatua kubwa ya kuiletea nchi yetu maendeleo na wananchi wataendelea kutuamini.
Kabla ya kumalizia napenda kusisitiza kwa wananchi wote kwamba ni jukumu letu kuhakikisha tunaisaidia mahkama na vyombo vya sheria katika utendaji wao wa kufanya haki kwa kufuata misingi na kanuni tulizojiwekea. Bila ya msaada na mashirikiano ya pande zote hizo jukumu tulilowakabidhi halitofanikiwa. Kila mmoja atimize wajibu wake.
Mheshimiwa Jaji Mkuu na Wageni Waalikwa, kwa kumalizia nawashukuru Viongozi wa Serikali, Dini, Vyama vya Siasa, Vikosi vya Ulinzi na Usalama, Waandishi wa Habari na Waalikwa wote kwa kufika kwenu katika maadhimisho haya ya Siku ya Sheria.
Aidha, nazishukuru Taasisi mbali mbali zilizosaidia na kuwezesha sherehe hizi kufanyika. Mwisho kabisa naishukuru Kamati ya Maandalizi ya sherehe kwa kazi yao nzuri ya kuandaa na kufanikisha sherehe hii. Nawatakia mafanikio katika mwaka mpya wa Mahkama lakini tujuwe kuwa kila siku ni siku ya sheria.
Nawashukuru tena kwa kunialika kujumuika nanyi katika kusherehekea siku hii muhimu – Siku ya Sheria, Zanzibar.
Ahsanteni sana kwa kunisikiliza.