STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 24 Februari, 2014
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein leo kwa nyakati tofauti amekutana na Balozi wa Tanzania nchini Malaysia Dk. Azizi Mlima na Balozi wa Malawi nchini Mhe Bibi Flossie Asekanao Gomale-Chidyaonga.
Akizungumza na Balozi Dk. Mlima ambaye alifikia kujitambulisha na kuaga kwa ajili ya kuripoti kituo chake cha kazi Dk. Shein alimueleza Balozi huyo kuwa Tanzania inayo mengi ya kujifunza kutoka Malaysia hivyo matarajio ya watanzania ni kuona uhusiano na ushirikiano kati ya Tanzania na nchi hiyo unaimarishwa zaidi.
“Uhusiano wetu na Malaysia ni wa miaka mingi na tumekuwa tukishirikiana na kujifunza baina yetu na hasa sisi tunayo mengi tunayoweza kujifunza kutoka ndugu zetu hao”alieleza Dk. Shein.
Alibainisha kuwa uhusiano kati ya Malaysia na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania una historia kubwa ambao ulianzishwa na waasisi wa nchi mbili hizo na kwamba ni jambo la kujivunia kwa Balozi Dk. Mlima kupata fursa hiyo kuiwakilisha Tanzania nchini humo.
“Kwa hiyo tungependa kuona katika kipindi cha utumishi wako nchini humo uhusiano wetu unaimarika kwa kupanua maeneo zaidi ya ushirikiano ikiwemo kushajiisha wawekezaji kutoka nchi hiyo kuja kuwekeza humu nchini” alisema Dk. Shein.
Aliyataja maeneo hayo kuwa ni pamoja sekta ya utalii, kilimo, viwanda vidogovidogo, viungo pamoja na kushirikiana katika mafunzo kwenye nyanja za mafuta na gesi.
Kwa upande wake Balozi Mlima alimshukuru Mhe Rais kwa nasaha zake na kuahidi kuyafanyia kazi mapendekezo na ushauri wake kwa kadri ya uwezo wake.
Akizungumza na Balozi wa Malawi nchini Mhe Bibi Flossie Asekanao Gomale-Chidyaonga, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema Tanzania na Malawi zina kila sababu za kuimarisha uhusiano na ushirikiano wao kuenzi urafiki na udugu kati yao ulioanzishwa na waasisi wa nchi hizo.
“Tumekuwa na uhusiano na urafiki wa miaka mingi tangu enzi za Marais wetu wa kwanza Mwalimu Julius Nyerere, Mzee Abeid Amani Karume na Mzee Kamuzu Banda”alieleza Dk. Shein.
Amesema ni jambo zuri kwa majirani kuimarisha uhusiano na ushirikiano wao na kueleza kuwa jitihada zinazoendelea sasa kujenga na kuimarisha taasisi za kikanda kunadhihirisha kuwa watu wa nchi hizo ni wamoja.
Alimueleza Balozi wa Malawi kuwa wapo wananchi wengi wa nchi hiyo ambao wameishi Zanzibar na Tanzania Bara na kuchanganyika na wenyeji na kufanya makazi yao humu nchini.
Hivyo alisema ni wajibu wa nchi mbili hizo kuimarisha ushirikino huo kwa manufaa ya Serikali na wananchi wa pande zote mbili.
Dk. Shein alizungumzia pia uwezekano wa kuanzisha ushirikiano katika ngazi ya elimu ya juu hususan kupitia Chuo kikuu cha Taifa Zanzibar –SUZA na Vyuo vikuu wa Malawi ili kubadilishana uzoefu wa kitaaluma ikiwemo maeneo ya utafiti.
Naye Balozi wa Malawi nchini Mhe Bibi Flossie Asekanao Gomale-Chidyaonga alimueleza Mhe Rais nchi yake imefurahishwa na uhusiano mzuri uliopo kati ya nchi na Tanzania kwa kuwa umejengwa katika urafiki na udugu wa kweli.
Alisema ushirikiano katika uendeshaji wa miradi na programu mbalimbali kati ya nchi yake na Tanzania ni ishara tosha ya ukaribu wa Serikali na wananchi wa nchi mbili hizo.
“Tumekuwa marafiki wa karibu na tunaoshirikiana katika kuendesha baadhi ya mambo yetu kwa pamoja kwa mfano mradi wa maendeleo na mazingira wa mto Songwe” alisema Balozi Chidyaonga na kuongeza kuwa fursa iliyopewa nchi yake na Tanzania kuhudumia mizigo ya nchi hiyo.
Balozi huyo alieleza furaha yake kwa Mhe Rais kuona kuwa wapo wanafunzi wengi kutoka nchini kwake katika vyuo vikuu hapa Zanzibar na kwamba wote wamemueleza kuwa wanafurahia mazingira waliyopo na maisha yao wakiwa na ndugu zao wa Zanzibar.
Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822