Quantcast
Channel: ZanziNews
Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

DK. SHEIN: TUMERIDHIKA NA UHUSIANO WETU NA MAREKANI

$
0
0
STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
    Zanzibar                                                                                                  28 Februari, 2014
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema Serikali na wananchi wa Zanzibar wanajivunia uhusiano mzuri uliopo kati yao na Serikali na wananchi wa Marekani.
Akizungumza na ujumbe kutoka jiji laVellejo katika Jimbo la Califonia nchini Marekani ulioongozwa na Meya wa jiji hilo Mstahiki Osby Davis, Ikulu leo Dk. Shein alisema mbali ya kujivunia, Zanzibar inathamini na kuridhishwa na uhusiano huo ambao umejengwa na historia inayowaunganisha watu wa Zanzibar na wa Marekani kwa karne nyingi.
“Tangu tulipoanzisha uhusiano kati yetu katika ngazi ya ukonseli mwaka 1845 tumejenga historia ya urafiki wa kweli kati ya serikali zetu na watu wake na ndio maana hadi leo uhusiano wetu umekuwa mzuri huku sote tukiwa na ari ya kuuimarisha kwa faida yetu sote” Dk. Shein alisema.
Aliielezea ziara ya ujumbe huo kutoka jiji la Vallejo kuwa sio tu ni muhimu katika kuwaunganisha wananchi wa Marekani na wenzao wa Zanzibar bali ni uthibitisho wa urafiki uliopo kati ya Zanzibar na Marekani.
“Tumekuwa watu wa kutembeleana na kusaidiana kwa miongo mingi. Vijana wengi wa Zanzibar wamekaribishwa nchini Marekani na wengine wamepata fursa za masomo na kuishi huko bila vikwazo” Dk. Shein alieleza na kuongeza kuwa ndio maana Zanzibar ingependa kuona kila siku uhusiano wake na Marekeni unaimarika.
Alibainisha kuwa kutokana na uhusiano mzuri huo Zanzibar ambayo ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekuwa ikipokea misaada mbalimbali ambayo imekuwa chachu katika kuimarisha maendeleo humu nchini.
Miongoni mwa misaada hiyo aliueleza ujumbe huo ni ujenzi wa barabara huko Mkoa wa Kaskazini Pemba ambazo zimejengwa kwa msaada wa watu wa Marekani kupitia Mfuko wa Changamoto za Milenia na zinatarajiwa kuzinduliwa hivi karibuni
Aliongeza kuwa Serikali na wananchi wa Zanzibar wamefurahishwa na uamuzi wa Serikali na watu wa Marekani kwa kuwajumuisha tena katika awamu ya pili na Utekelezaji wa Miradi ya Mfuko wa Changamoto za Milenia uamuzi ambao unaonesha kuwa Marekani na Zanzibar ni marafiki wa kweli.
Kwa hiyo Dk. Shein aliuthibitishia ujumbe huo dhamira ya kweli ya Serikali na wananchi wa Zanzibar ya kuendeleza na kuuenzi uhusiano wake na Marekani.   
“Tuna malengo yanayofanana na dhamira yetu ni moja hivyo kuimarisha uhusiano wetu ndio nia yetu na ni wajibu wetu” Dk. Shein alisisitiza.   
Aliutaka ujumbe huo ambao utafanya mazungumzo na wadau mbalimbali katika sekta binafsi hususan sekta ya utalii kuangalia namna ya kushirikiana na Zanzibar katika kuendeeza utalii kati ya Zanzibar na Jimbo la Califonia na Marekani kwa ujumla.
“Ningependa kusisitiza ushirikiano katika sekta ya Utalii ambayo naamini nyinyi mna uzoefu mkubwa na maarifa hivyo sio tu kuwa tunaweza kubadilishana uzoefu lakini pia kuhimiza uwekezaji kutoka jimbo hilo kuja Zanzibar”alieleza Dk. Shein.
Kwa hiyo alimueleza Mstahiki Meya huyo kuwa ziara hiyo imefungua ukurasa mpya katika kuendeleza na kuimarisha ushirikiano kati ya watu wa Zanzibar na watu wa jimbo la Califonia na Marekani kwa ujumla.
Kwa upande wake Mstahiki Meya wa Vallejo Bwana Osby Davis alisema kufika kwao Zanzibar wanajiona wamefika nyumbani na kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa kumpa fursa yeye na ujumbe wake kuonana naye.
“Ni fahari na heshima kubwa kwetu kupata fursa ya kuonana nawe Mhe Rais  wa Zanzibar na pia kuonana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Kikwete na kufanya mazungumzo na ujumbe wangu” Alieleza Mstahiki Meya Davis akionyesha furaha.
 Amesema kuwa ziara yake hiyo ndio ni mwanzo wa ziara nyingi kama hizo kutembelea Zanzibar na Tanzania kwa jumla.
 “Sisi wananchi wa Marekani wenye asili ya Afrika tunajivunia kutambua asili yetu na ndio maana tumeanzisha juhudi kuimarisha uhusiano na asili yetu”alieleza Mstahiki Meya Davis.
Alibainisha kuwa kusema hivyo sio kwamba wao si wa Marekani lakini ni ukweli kuwa watu wa Marekani wana asili zao wengine wanatoka Japan, wengine Ujerumani, wengine wa China na kadhalika hivyo wao Afrika ndio kwao na wanajivunia kujitambua hivyo na kusisitiza kuwa huo ni ukweli wa kihistoria.

Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822  

Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>