Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Balozi Seif Ali Iddi akikabidhi mchango wa Shilingi 1,000,000/- kwa Katibu wa CCM Tawi la Mafufuni Jimbo la Bumbwini Nd. Muslih Maulid Fidia kwa ajili ya uwezekaji wa Tawi lao la CCM. Kati kati yao aliyevaa suti ni Diwani wa Wadi ya makoba Bwana Juma Zahor.
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na Uongozi wa CCM Tawi la Mafufuni mara baada ya kuukabidhi mchango wa Fedha kwa ajili ya uwezekaji wa Tawi lao.(Picha na Hassan Issa wa – OMPR)
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi Balozi Seif Ali Iddi amewapongeza Viongozi na Wanachama wa CCM wa Tawi la Mafufuni Jimbo la Bumbwini kwa uamuzi wao wa kujenga Tawi jipya la CCM lenya hadhi ya Chama chenyewe.
Balozi Seif alisema hayo wakati akikabidhi mchango wa Shilingi Milioni moja kwa ajili ya uwezekaji wa Tawi hilo kufuatia ahadi aliyoitoa ya kusaidia harakati za ujenzi wa Jengo hilo mchango alioukabidhi kwa uongozi wa Tawi hilo hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Alisema lengo la Chama cha Mapinduzi katika Maboresho yake ya uimarishaji wa Chama hicho imewaagiza Viongozi na Wanachama wa Chama hicho ngazi za Matawi, Wilaya na Mkoa kujikita katika ujenzi wa Ofisi zitakazofanana na Chama chao.
Alifahamisha kwamba wakati umefika kwa Wana CCM kuhakikisha kwamba wanaondokana na tabia iliyozoeleka katika baadhi ya Matawi Nchini kukutana katika vikao vyao chini ya Miti.
Alisema kwamba Uongozi wa Juu ya Chama cha Mapinduzi ngazi ya Taifa utaendelea kutoa muongozo sambamba na kushajiisha wanachama wake kuendeleza mpango huo hasa katika yale maeneo ambayo hadi sasa hayajaamua kujenga majengo ya kudumu na ya Kisasa ya chama chao.
Alielelezea matumaini yake kwamba juhudi zinazochukuliwa na wanachama walio wengi katika maeneo mengi Nchini za ujenzi wa majengo yao utawawezesha wanachama hao kuingia katika chaguzi za chama hicho katika mazingira mazuri ya makazi.