Quantcast
Channel: ZanziNews
Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Tumkumbuke Riffat Said, Miaka 14 baada ya kifo chake

$
0
0
Na Mahmoud Zubeiry, aliyekuwa Zanzibar
MIONGONI mwa magolikipa wazuri wa mchezo wa mpira wa miguu ambao Tanzania imewahi kuwa nao katika miaka mbalimbali, ni Rifat Said Mohammed ambaye sasa ni marehemu.
Marehemu Rifat aliyefariki dunia tarehe 9 Mei, 2000 kisiwani Zanzibar, anakumbukwa sana na wapenzi wa soka hapa nchini, kwa kuzidakia kwa mafanikio klabu za Miembeni, Mlandege na hatimaye Malindi SC.
Bado unakumbukwa; Marehemu Rifat Said Mohammed kushoto akiwa na mkewe Rahma enzi zao uhai wao. Picha hii ilipigwa mwaka 1994

Kwa upande wa Tanzania Bara, Riffat alidakia klabu za Coastal Union ya Tanga na Yanga SC ya Dar es Salaam.
Aidha umahiri wa mlinda mlango huyo aliyekuwa na umbo refu ambalo ni miongoni mwa sifa muhimu sana kwa wachezaji wanaochezea nafasi hiyo ya kudhibiti mpira usitinge nyavuni mwake, uliwavutia pia makocha wa timu za taifa za Zanzibar na Tanzania na kumjumuisha kwenye vikosi vilivyoshiriki mashindano mbalimbali ya Afrika.
Lakini, Rifat aliyezaliwa tarehe 23 Septemba 1968, na wakati anaitwa na Mola alikuwa na umri wa miaka 32, aliacha mjane na watoto wawili walikuwa wadogo wakati anafunga pumzi.
Mtoto wake wa kwanza mwanamke anayejulikana kwa jina la Meyya, wakati huo alikuwa na umri wa miaka mitatu, na sasa ametimiza 19.
Aidha, mwingine wa kiume Said, alikuwa akikaribia miaka miwili na tayari ametimiza miaka 17 sasa.
Mke mwema aliyetunza kiapo cha ndoa; Kulia ni mjane wa marehemu Rifat, Rahma Haidar na kulia ni binti yao, mtoto wao wa kwanza, Meyya

Kutoka kulia Said Riffat, mtoto wa marehemu, katikati Mahmoud Zubeiry na kushoto mke wa marehemu, Rahma

Kwa kuwa BIN ZUBEIRY ilikuwa rafiki wa karibu wa marehemu Rifat, ilipata raghba ya kuitafuta familia yake baada ya miaka mingi kupita tangu marehemu baba yao aage dunia na kuacha huzuni kubwa kwao na kwa wadau wa michezo hasa soka nchini.
Dhamira ya kutaka kukutana na familia hiyo, ni kufahamu namna watoto wake walivyoweza kukua baada ya kipindi kigumu cha msiba huo wa kuondokewa na nguzo hiyo ya aila.    
Baada ya kuwasiliana na watu wa karibu na familia hiyo kutaka kujua namna nitakavyojua iliko, BIN ZUBEIRY ikapiga shoto kulia hadi mtaa wa Michenzani mjini Unguja, block namba 7, ghorofa ya nne wanakoishi watoto hao pamoja na mama yao mzazi.  
Sina budi kumshukuru kwa dhati mjane wa marehemu, Bi. Rahma Haidar kwa kunipa mapokezi mazuri sana licha ya kuwa ilikuwa mara ya kwanza kukutana naye.
Niseme tu, mlango wa nyumba ya mwenyeji wangu huyo ulikuwa uwazi na kwa bashasha na kila aina ya heshima na taadhima, alinitaka nijisikie kama niko nyumbani, hali iliyonipa uhuru wa kufanya mahojiano na familia hiyo kwa ufanisi mkubwa.
Mama huyo wa watoto wawili, ni muajiriwa wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Zanzibar, akiwa Msaidizi Muhasibu katika Idara ya Utabibu wa Mifugo.
Kulia marehemu Rifat akiwa amembeba Said alipokuwa mdogo na kushoto ni Said alivyo hivi sasa


Marehemu Rifat akiwa na mchezaji mwenzake wa Malindi mwaka 1995, Hassan Wembe kushoto

Nilipomdadisi mama huyo mwenye umri wa miaka 43, ni vipi alimudu mzigo wa kuwalea wanawe hao baada ya marehemu mumewe kufa huku ndoa yao ikiwa changa na katika rika la ujana, hakuacha kutoa shukurani kwa wazazi wa marehemu Rifat, mama yake Mariam Mabrouk, na baba yake, Sheikh Said Mohammed kwa kuubeba kikamilifu mzigo huo.
Aidha, ndugu wa marehemu akiwemo dada yake  Hurina (shangazi yao), wamekuwa na msaada mkubwa sana katika ulezi wa malaika hao wa Mungu, na wakaweza kusoma vizuri.
Mashallah! Meyya amefanya mtihani wa taifa wa kidato cha Nne mwaka jana, na matokeo yaliyotoka yanaonesha amefanya vyema kwa kupata divisheni mbili, na sasa anajiandaa kuendelea na ngazi nyengine ya juu.
Msichana huyo ametokea shule ya sekondari ya binafsi Laurette iliyoko, Chukwani nje kidogo ya Manispaa ya Zanzibar.
Kwa upande wake, Said anaendelea na masomo katika shule ya kijiji cha kulelea watoto yatima Zanzibar SOS, Mombasa Unguja akiwa kidato cha Tatu.
“Alhamdulilahi, siwatoi shukurani wakwe zangu na wifi zangu, kwani tangu kufa kwa marehemu mume wangu, wamenishika mkono hadi watoto wangu wamekua na kusoma,” alitoa ya moyoni Rahma.
BIN ZUBEIRY ilitaka kujua, wakati watoto wake walipopata fahamu na kusimuliwa kwamba baba yao alifariki wakiwa wadogo, walizipokeaje habari hizo?
Akijibu suala hilo, Bi. Rahma alisema walikuwa majasiri na kukubaliana na ukweli, ingawa walitamani nao wangemuona kama ilivyo kwa wenzao wengine ambao wazazi wao bado wako hai.   
Kwa kuwa mtoto wa nyoka ni nyoka, mtu angedhani watoto wa marehemu watakuwa wamefuata nyayo za baba yao katika tasnia ya michezo hasa huyu wa kiume, Said.
Kwa kweli Said ana umbo sawa na marehemu baba yake linalomruhusu kukaa golini, na wakati nikimuhoji, alinithibitishia kwamba anacheza mpira ingawa si kwa ushindani wa kitimu zilizo rasmi, bali huwa anajumuika na vijana wenzake mtaani kukuza vipaji vyao.
Alisema, awali alikuwa akicheza nafasi ya mlinda mlango, lakini baadae akabadili na kujikita kwenye nafasi ya kiungo mshambuliaji yaani namba 8 na 10.  
Hata hivyo, mama yake Said hakumpa mwanya wa kushughulika sana na mchezo huo kwa hofu kwamba unaweza kumuathiri kimasomo.
Marehemu Rifat katikati waliochuchumaa akiwa na kikosi cha Malindi mwaka 1995

Marehemu Rifat wa kwanza kulia waliochuchumaa akiwa na kikosi cha Yanga SC mwaka 1993 mjini Kampala, Uganda

Na kwa hilo alisema amefanikiwa kumvuta saidi katika masomo, na kuubana muda wake wa kucheza mpira, kwa lengo la kumjengea msingi mzuri zaidi katika elimu.    
Tukirudi nyuma katika historia ya marehemu Rifat ambaye pamoja na kuwa na marafiki wengi miongoni mwa wachezaji wenzake, lakini rafiki yake mkubwa alikuwa HajJi Mwinyi, aliyecheza naye Mlandege SC iliyokuwa ikifadhiliwa na mfanyabiashara maarufu mjini Zanzibar Abdulsatar Dawood.
Dawood pia aliwahi kuwa mlinda mlango wa klabu hiyo kabla haijapanda ligi kuu ya Zanzibar.      
Rifat alikuwa mmoja wa walinda milango mahiri kuwahi kutokea katika ardhi ya Tanzania, ambaye alipata mafanikio hadi kimataifa akiwa na klabu na timu za taifa.
Ameichezea timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars tangu mwaka 1992 hadi 1997 alipojiuzulu baada ya kukerwa na maneno ya kashfa yaliyotolewa akiwa na timu hiyo nchini Burundi.
Stars ilikwenda kucheza mechi ya kuwania tiketi ya Fainali za Mataifa ya Afrika mwaka 1998 na Rifat alikuwa langoni mjini Bujumbura akafungwa bao la shuti la mbali timu hiyo ikilala 1-0, ingawa aliokoa michomo mingi ya hatari.
Baada ya mchezo, timu ikiwa kwenye ndege inarejea Dar es Salaam yalitolewa maneno ya kumsimanga kwa kufungwa bao la mbali, naye alipotua tu Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere, akaunganisha Zanzibar badala ya kwenda kambini Jeshi la Wokovu.
Aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Hafidh Badru na wachezaji wengine wote wa Zanzibar nao wakajitoa kwenye timu kumfuata Riffat na kurejea Zanzibar, akabaki kipa Mbarouk Suleiman pekee kati ya Wazenji.
Marehemu Syllersaid Salmin Kahema Mziray akateuliwa kuwa kocha mpya na akampanga Mbarouk Suleiman katika mchezo wa marudiano badala ya Mfaume Athumani Samatta, kipa mwingine aliyekuwamo kikosini na Stars ikafungwa tena 1-0 Uwanja wa Taifa na Burundi na kutolewa kwa jumla ya mabao 2-0.
Rifat pia aliiwezesha Yanga SC kutwaa Kombe la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, sasa Kombe la Kagame mjini Kampala, Uganda mwaka 1993 baada ya kudaka vizuri kwenye mechi ya fainali dhidi ya SC Villa kuanzia dakika ya saba, baada ya kuumia kwa Steven Nemes aliyedaka tangu mwanzo wa mashindano.  
Mabao ya Said Nassor Mwamba ‘Kizota’ (marehemu pia) aliyeibuka mfungaji wa mashindano hayo na Edibily Jonas Lunyamila yaliipa Yanga SC ushindi wa 2-1 Uwanja wa Nakivubo.
Miaka miwili baadaye, Riffat alikuwemo kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Zanzibar kilichotwaa taji la kwanza na la mwisho la Kombe la CECAFA Challenge mwaka 1995 nchini Uganda. 
Mwaka huo huo 1995, Riffat alikuwemo kwenye kikosi cha Malindi ya Zanzibar kilichofika Nusu Fainali ya Kombe la CAF, wakati likiitwa Kombe la Chifu Mashood Abiola wa Nigeria- sasa limeunganishwa na Kombe la Washindi na kuwa Kombe la Shirikisho.
Mwaka 1998, Riffat alikuwemo kwenye kikosi cha Mlandege kilichofika fainali ya Kombe la Kagame na kufungwa na Rayon Sport ya Rwanda Uwanja wa Amaan visiwani Zanzibar.
Riffat atakumbukwa siyo tu kwa umahiri wake langoni, bali upole, ukarimu, uadlifu na nidhamu. Alikuwa kipa bora wakati wake, lakini hakuwa na kinyongo kuwa benchi wakidaka wenzake, kwa sababu enzi zake alikuwa amezungukwa na makipa bora wenzake kila timu aliyochezea.
Mfano timu ya taifa ya Zanzibar alikuwa anadaka pamoja na Ali Bushiri na alipokuwa Yanga alikuwa pamoja na marehemu Sahau Kambi na Steven Nemes.
Timu ya taifa alikuwa akikutana na Nemes na Mwameja Mohamed na aliwaheshimu walinda milango wenzake wote. 
Rifat aliacha flati mbili alizonunua katika maghorofa ya nyumba za Maendeleo, eneo la Kilimani ambayo mkewe ameweka wapangaji na nyingine akamnunuliwa mama yake katika maghorofa ya Michenzani.
Unaweza kusema nini kuhusu Rifat, picha halisi ya mtu muungwana aliyekuwa na kipaji na asiye na choyo. Mungu ajaalie kizazi chake, watoto wake waendelee kupata makuzi mema. Mungu amjaalie mjane wake kwa moyo wake wa ujasiri, uliomuwezesha kuwalea veyma watoto wa marehemu hata baada ya kifo cha mumewe.
Aliondokewa na mumewe akiwa bado binti mbichi, lakini akaamua kubaki mjane na hakutaka kujiingiza kwenye ndoa nyingine baada ya eda yake.    
Mungu aiweke pema peponi daima roho ya marehemu Rifat Said Mohammed. Amin.

Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>