Na Fatuma Kitima, DSM
POLISI kanda maalum ya Dar es Salaam limekanusha habari zilizotolewa na baadhi ya vyombo vya habari kuwa Mbunge wa Jimbo la Ubungo, John Mnyika alikoswa na bomu na kumjeruhi mmoja wa wafuasi wake katika mkusanyiko chama hicho, Mabibo jijini Dar es Salaam.
Naibu Kamishna wa Polisi Kanda Maalum, Ali Mlege alisema wafuasi wa chama hicho walikusanyika katika eneo hilo,ambapo mgeni rasmi alikuwa Mnyika.
Alisema Chadema kilikuwa kimepanga kufanya mkutano wa hadhara Julai 21 mwaka huu katika uwanja wa Sahara uliopo Mabibo kinyume na utaratibu.
Alieleza Polisi walijaribu kumwelezea Mnyika kuwa awatangazie wafuasi wake kuwa mkutano umezuiliwa kufanyika katika eneo hilo ili watawanyike.
Alisema bomu ambalo Chadema wanadai lilimkosa Mnyika na kumjeruhi mfuasi wa chama hicho, liliripuka ndani ya gari la Polisi wakati askari E.5340 D/CPL Julius alipokuwa akisogeza mabomu ya machozi ya kutupa kwa mkono na kwamba halikusababisha madhara yoyote kwa askari wala raia.
Alisema Mbunge huyo alikubaliana na polisi na kuwatangazia wafuasi wake kuwa mkutano umezuiliwa hivyo waelekee Ubungo ambako walikuwa na kibali kutoka polisi Kimara na kuondoka kwa amani katika eneo hilo bila ya madhara yeyote.
Alibainisha kuwa habari ambayo imeenezwa kuwa Mbunge huyo alikoswa na mabomu si kweli na kuomba vyombo vya habari kabla ya kutoa taarifa ni vizuri kuuliza ili kuthibitisha.
Hatahivyo alisema polisi wapo kwa lengo la kulinda watu na mali na si vinginevyo.
Wakati huo huo polisi wamemkamata tapeli hatari
anayefahamika kwa jina la Mfaume Omari maarufu Mau (29) mkazi wa Magomeni Kagera kwa kosa la kutumia majina viongozi wa serikali ,viongozi wa dini na watu maarufu kujipatia fedha.
Alisema polisi walikuwa wakifuatilia nyendo za mtuhumiwa baada kupokea taarifa kutoka kwa Mchungaji Getrude Rwakatare.
Kamishna Mlege alisema Mchangaji Rwakatare alitoa taarifa mara tu baada ya kuona jina lake linatumika vibaya.
Kamishna Mlege alisema baada ya mahojiano mtuhumiwa alikiri kutapeli watu mbalimbali wakiwemo wachezaji maarufu wa timu ya mpira nchini Tanzania.