Na Othman Khamis OMPR.
Wanachama wa Chama cha Mapinduzi na wananchi wote wamenasihiwa kuendelea kuzingatia mfumo wa Umoja uliopo miongoni mwa jamii utakaosaidia kulivusha salama Taifa la Tanzania hasa wakati huu wa mchakato wa Katiba Mpya ambao uko katika hatua ya Bunge Maalum la Katiba.
Nasaha hizo zimetolewa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dr. Ali Moh’d Shein wakati akizindua rasmi Mbio za Uzalendo zilizoandaliwa na Umoja wa Vijana wa CCM Tanzania { UVCCM } kuadhimisha miaka 50 ya Muungano wa Tanzania zilizofanyika Makao Makuu ya CCM Mjini Dodoma.
Dr. Shein ambae pia ni Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Zanzibar alisema umoja wa Wana CCM hao ndio kigezo sahihi kitakachowahakikishia nguvu za kuendeleza chama hicho sambamba na ushindi katika kila chaguzi chini ya uhamasishaji unaosimamiwa na Umoja wa Vijana wa Chama hicho.
Alieleza kwamba Vijana ndio ngao na Jeshi madhubuti la kuimarisha nguvu za Chama cha Mapinduzi muda wote kuzingatia misingi imara ya ujasiri na uzalendo iliyoachwa na waasisi wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
“ Lile sisitizo langu nililolitoa wakati nikizindua matembezi ya Vijana kuadhimisha miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar Micheweni Pemba nafurahi kusema kwamba mmefuzu vizuri katika kuelimisha jamii umuhimu wa kuendelea kuwepo kwa Muungano wa Tanzania pamoja na kulinda mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 “. Alifafanua Dr. Sheni.
Makamu Mwenyekiti huyo wa CCM Zanzibar aliupongeza Uongozi na Wanachama wa Umoja wa Vijana wa CCM kwa uamuzi wao kuandaa mbio hizo za Uzalendo zitakazojumuisha mikoa yote 31 Tanzania Bara na Zanzibar.
Alisema ujumbe wa Vijana hao unaosisitiza umuhimu wa kuuendeleza Muungano wa Tanzania utasaidia kuelimisha wananchi hasa kundi kubwa la Vijana kuelewa sababu zilizopelekea waasisi wa Mataifa haya mawili kuamua kuungana na kuwa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.
Dr. Shein alifahamisha kwamba wapo baadhi ya watu wakiwemo pia Viongozi waliowahi kushika nyadhifa mbali mbali Serikalini na Hata kwenye medani ya Kisiasa wanajaribu kupotosha wananchi kwa kuhoji mfumo wa Muungano wa Tanzania.
“ Hii tabia ya baadhi ya watu ambapo wengine tayari wameshashika madaraka kuhoji Muungano wa Tanzania. Kwanini hawatumii fursa hiyo kuwahoji Wareno, Waarabu na Waingereza waliokuja kutawala Tanzania Bara pamoja na Zanzibar wamepewa ruhusa hiyo ya kutawala na nani ? “. Aliuliza Dr. Sheni.
Makamu Mwenyekiti huyo wa CCM Zanzibar alisema Vijana wanapaswa kuendelea kukemea mambo ambayo baadhi ya watu wanakwenda kinyume na matakwa ya Wananchi walio wengi.
Alisisitiza Historia ya Kimaumbile iliyopo katika mwambao wa Mashariki mwa Tanzania inaonyesha wazi kwamba Visiwa vya Zanzibar vilikuwa pamoja na Tanzania Bara jambo ambalo linathibitisha wazi kuwa Muungano wa pande hizo ni halali kabisa.
“ Lengo na Dira ya Waasisi wa Ukombozi wa Mataifa ya Bara la Afrika ni kuona Afrika inakuwa moja jambo ambalo halikuwezekana. Lakini Zanzibar na Tanganyika zilifanikiwa Kuunga Muungano ambao hadi sasa umekuwa kigezo Barani humo “. Alifafanua Dr. Sheni.
Aliwakumbusha Vijana kukataa kata kata kugawanywa kitendo ambacho mbali ya kulitia Taifa msuko suko wa ukosefu wa amani lakini pia kinaweza kuhatarisha mustakabala wa hatma yao ya baadaye.
“ Vijana mnapaswa kukataa kata kata kugawanywa. Atakaye kuja kwenu na lugha za kejeli na nyinyi wakejelini. Atakayekuja na vitisho endeleeni na safari yenu na mwacheni na ujinga wake “. Aliongeza Dr. Sheni.
Dr. Sheni alimpongeza Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Jakaya Mrisho Kikwete kwa Hotuba yake aliyoitoa wakati akilizindua Bunge Maalum la Katiba Mjini Dodoma ambayo imekosha kiu ya Watanzania waliowengi Nchini.
Mapema Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa CCM Tanzania Nd. Sistus Mapunda alisema mbio hizo za Uzalendo zitakazokuwa na lengo la kuikumbusha Jamii umuhimu wa Muungano wa Tanzania zitafanyika katika mfumo wa Kikanda.
Nd. Mapunda alisema washiriki wa mbio hizo za Mapiki piki wataishia Mkoani Kibaha Tarehe 22 April ambapo watamalizia mbio hizo kwa matembezi ya miguu yatakayoishia Mjini Dar es salaam ambapo Mwenyekiti wa CCM Taifa Rais Jakaya Mrisho Kikwete atayapokea rasmi Matembezi hayo mnamo Tarehe 25 April 2014.
Akitoa salamu za Chama cha Mapinduzi kwa Niaba ya Katibu Mkuu wa CCM Abdull rahaman Kinana, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Nd. Vuai Ali Vuai alisema Muungano wa Tanzania unategemea umakini mkubwa walionao Vijana wa UVCCM.
Nd. Vuai aliupongeza Uongozi na Wanachama wa Umoja huo kwa kuamsha ari ya uzalendo walionayo hapa nchini na kuwaahidi kwamba Chama cha Mapinduzi Taifa kitaendelea kuwaunga mkono jitihada za vijana hao.
Naye Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM Taifa Mh. Sadifa Juma Khamis akimkaribisha Mgeni rasmi Dr. Ali Moh’d Sheni kuzindua mbio hizo za Uzalendo alisema Muungano wa Tanzania bado unaendelea kunufaisha Wananchi walio wengi licha ya baadhi ya watu wachache waliofaidika nao wakifanya kejeli dhidi ya Muungano huo.
Mwenyekiti Sadifa alisema inasikitisha kuona kwamba watu hao hivi sasa wamefungua Ofisi za kupika majungu na mizengwe inayoonekana kuwa ni adui wapya miongoni mwa jamii.
Alisema mpango na dhamira yao hiyo mbaya haitavumiliwa na ukorofi wao huo lazima ufikie kikomo na kuonya kwamba nyendo zao zinatambuliwa na kufuatiliwa kwa ukaribu wa kutosha.
Alisema inasikitisha kuona baadhi ya watu hao wamekuwa mawakala, madalali na mamluki wanaotaka kuwasaliti wananchi wakati wamesahau kwamba Muungano uliopo ndio uliowafaidisha kiuchumi.
“ Ni mambo ya kusikitisha wengine ni watu wazima, wana heshima zao lakini ni watu wazima ovyo, wamefaidika sana katika Serikali hizi, wamejijenga kiuchumi, wamefaidi matunda ya Mapinduzi na Muungano sasa ni aibu unapowaona kwa hiari yao wanaamua kuwa mawakala, madalali na mamluki wa kuwasaliti wananachi “ Alisema Mwenyekiti huyo wa UVCCM Taifa Sadifa Juma Khamis.
Aliongeza kwamba Vijana kamwe hawatakuwa na muhali pamoja na uvumilivu na iko siku watasimama kuwafichua watu hao hadharani kweupe.