Quantcast
Channel: ZanziNews
Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Siasa za Kizanzibari, nani msema kweli na nani mwanasiasa?

$
0
0

Na A K Simai
Siasa za kizanzibari ni za kimaajabu sana. Wakati mwengine hupendeza wakati mwengine huchukiza na wakati mwengine hukirihisha. Ndio siasa zetu hizo tuzitake tusizitake.

Ni siasa ambazo hata ukitaka kuingia au kujihusisha kwanza lazima ule na ushibe maana kama hujafanya hivyo linaweza kukukuta jambo njiani likakuhamanisha na kusahau kwamba ulikuwa hujala.

Mheshimiwa wetu aliepewa dhamana ya kuliongoza baraza letu la wawakilishi kwa nchi yetu inayotambulika hapa kwetu kama ni nchi ilhali majirani zetu wameshindwa kutuwafiki na kututambua hivyo, alifikwa na kitahanani cha majaribu ya uongozi kwa kukanwa hadharani kwamba amewasaliti wawakilishi wa CCM Zanzibar kwa kupeleka maamuzi ya mambo ambayo hakuna aliyefahamu zaidi ya yeye Spika na kisha kuyaita hayo kama ni maoni ya Baraza la Wawakilishi wakati hakuna maamuzi yaliyofikiwa ya aina hiyo katika kumbukumbu za Baraza.

Kitahanani hiki kilimfanya Spika , Mhe Pandu Ameir Kificho kujitoa hadharani na kuleta ufafanuzi na pia kuhakikisha kwamba bado anasimama na uamuzi wa chama kilichomuweka madarakani CCM wa serikali mbili licha ya maoni aliyoyafikisha tume ya Katiba kumkana. Ingawa bado hatujaisikia Serikali yetu yenye sura ya umoja wa kitaifa ikitoa tamko kama walivyofanya wawakilishi wa CCM. Tungelipenda kuisikia Serikali kwani kiti cha Spika, ingawa kimeshikiliwa na Mwakilishi kutoka CCM,  ni mhimili mmoja mkuu wa Serikali.

Nilitanguliza kwa kusema siasa zetu na za kimaajabu kwasababu kilichofuatia baada ya hapo sasa ndio siasa. Kwanza kulianza lilikuwa ni suala la tafsiri tu ya kudai mamlaka huru katika serikali mbili. Mara Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar akasema yeye hana taarifa na maoni hayo na wala hakuwahi kuyaona. Ni nani anaesema kweli au na nani anaefanya siasa? Ni kweli kwamba wajumbe wa baraza la wawakilishi walikubaliana kupeleka maoni yao kama taasisi?

Rais wa Zanzibar aliwahi kuulizwa kuhusu msimamo wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar juu ya muundo upi wa muungano unaopendekezwa na Mhe Rais akajibu kwa ufasaha kabisa kwamba  kwa suala hili serikali haina maoni wala mapendekezo ni suala la wananchi.

Kizungumkuti kinakuja pale tunapowasikia Makamu wetu wawili wa Rais wa serikali moja inayoitwa ya Umoja wa kitaifa wanavyopingana hadharani kwa kila mmoja wao akidai muundo wa serikali tofauti mmoja akiipigia debe serikali mbili na mwengine akiipigia debe serikali tatu. Je kwa kufanya hivi wanawakilisha Serikali au wanawakilisha vyama vyao? Kwani serikali si imeshatoa tamko kwamba haina msimamo kwa hili kupitia Mheshimiwa Rais?. Huu umoja wa kitaifa uko wapi hapa ikiwa viongozi wakuu hawaoneshi dhamira ya kweli ya umoja mbele ya hadhara?

Jee na hii ni siasa pia? Hebu mie nikajitafutie chajio maana naona bado sijashiba nipate nguvu za kuzungumzia siasa za Kizanzibari.

Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>