JUMUIYA ya Kiislamu Zanzibar (ZADEO), imetoa changamoto kwa mtu au taasisi yoyote inayoidai kupeleka malalamiko yake katika vyombo vya sheria ili kudai haki.
Akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Umoja wa Watu Wenye Ulemavu Zanzibar Kikwajuni jana, Rais wa jumuiya hiyo Haji Ameir Haji, alieleza kusikitishwa kwake na kitendo cha Waziri wa Katiba na Sheria, Abubakar Khamis Bakary, kumuita yeye mwizi, tapeli na muongo.
Ameir alilazimika kutoa ufafanuzi huo, baada ya hivi karibuni kutajwa katika kikao cha Baraza la Wawakilishi, kuwa amewatapeli watu waliotaka kwenda Hijja kwa msaada wa jumuiya hiyo.
Alisema kama kulikuwa na watu waliopeleka malalamiko kwa Waziri huyo, naye alipaswa kufuata taratibu za kisheria na kutafuta ukweli wa kina kutoka pande zote badala ya kumchafua katika chombo hicho cha kutunga sheria.
“Hili ni suala la kidini na linahitaji kushughulikiwa kwa taratibu za kidini, dini haitaki kumtangaza mtu mabaya yake, bali kama amekosea aelimishwe na ikiwa habadiliki afikishwe katika vyombo husika,” alieleza.
“Tangu nitajwe katika Baraza la Wawakilishi, nimekuwa nikisubiri hao wanaonidai wanishtaki lakini hakuna hata mmoja aliyekuja kuniambia kitu wala kupeleka kesi polisi, huu ni ushahidi kwamba madai haya yamelenga kunichafua mimi na jumuiya yangu,” aliongeza.
Alisema amebaini wapo baadhi ya watu wanaotumia nafasi zao kutaka kumharibia sifa mbele ya jamii, nchi na serikali kwa jumla, lakini akasema, hilo halimrudishi nyuma katika jitihada zake za kuisaidia Zanzibar na wanajamii wanaohitaji huduma zake na za jumuiya ya ZADEO.
Alikiri kuwa kulikuwa na baadhi ya watu walioshindwa kwenda Hijja mwaka uliopita, lakini akasema hayo yalitokana na matatizo ya kiutendaji yaliyojitokeza wakati wa kuwaorodhesha kwenye mitandao na kwamba haikuwa nia ya ZADEO wala yeye, kuwakosesha safari hiyo.
Akionesha ushahidi wa nyaraka, Rais huyo wa ZADEO, alisema jumuiya yake iliyosajiliwa mwaka 2002 kwa taratibu zote za kisheria, inatambulika serikalini na imekuwa ikipata ushirikiano mkubwa hata katika serikali kuu.
Hata hivyo, alisema kimsingi ZADEO wala yeye hawapeleki watu katika ibada ya Hijja, bali wanachofanya ni kuwaombea unafuu, kwani nafasi hizo haziuzwi.
Alitoa mfano kwa kusema katika mwezi wa Mei mwaka huu, aliwakutanisha viongozi wa taasisi zinazosafirisha mahujaji zilizopo nchini na uongozi wa Shirika la Ndege la Yemen (Yemen Air), kulitaka kuwapunguzia gharama mahujaji wa Zanzibar na lilikubali kufanya hivyo.
Kuhusu kukwama kwa watu hao kwenda Makka, Ameir alisema alichukua juhudi kubwa kuwasaidia kwa kufuatana nao kila katika taasisi husika, na baadae akajitokeza mtu mmoja mkubwa na maarufu na kuwaambia fedha zao watumie kwa mambo mengine na kwamba yeye atagharamia safari yao.
Hata hivyo, Ameir alisema mtu huyo (jina tunalo), aliwageukia dakika za mwisho wakati safari ikikaribia na mzigo wote na lawama ukamuangukia yeye.
Alisema kwa sasa hakuna hata mtu mmoja anayewadai, na akaeleza kwamba yuko tayari kugharamia mkutano na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi ili aeleze kwa kina kilichotokea, ili wafahamu ukoko na utandu, na wasikitumie chombo hicho kwa kinga ya kutoshitakiwa, kuwadhalilisha wasioweza kufika katika baraza hilo kujitetea kwani hiyo si demokrasia na haifuati misingi ya utawala bora.