Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akizungumza na Uongozi wa Ofisi ya Rais,Kazi na Utumishi wa Umma katika mkutano wa utekelezaji mpango kazi wa robo tatu ya mwaka Julai-Machi 2013/2014,katika ukumbi wa mikutano Ikulu Mjini Unguja
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (katikati) akizungumza na Uongozi wa Ofisi ya Rais,Kazi na Utumishi wa Umma katika mkutano wa utekelezaji mpango kazi wa robo tatu ya mwaka Julai-Machi 2013/2014,katika ukumbi wa mikutano Ikulu Mjini Unguja.[Picha na Ramadhan Othman,Ikulu.]
STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 02 Mei, 2014
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema ni lazima utaratibu maalum uandaliwe wa kuwaelimisha watumishi wa umma wa ngazi zote juu ya Sheria ya Utumishi wa Umma Na. 2 ya mwaka 2011 ili waweze kuifahamua na kuitekeleza kwa ufanisi.
Amesema katika kufanya hivyo Wizara haina budi kuangalia maeneo maalum na muhimu ambayo kwa watumishi hao ni lazima wayafahamu pamoja na kanuni zake ambazo miongoni mwake zinabainisha makosa mbali mbali ya kiutumishi ambayo mtumishi anaweza kuyafanya bila ya kujifahamu.
Alitilia mkazo umuhimu wa kuwepo kwa muongozo maalum kuhusu utaoji elimu hiyo ili ujumbe mmoja uwafikie watumishi hao katika tafsiri ya Sheria hiyo na kanuni zake ili kusiwepo na tofauti ya ufahamu huo.
Katika kikao hicho Dk. Shein amezikumbusha Wizara na Idara za Serikali kuwa upangaji wa miradi mikubwa ya kitaifa hivi sasa ni lazima ufanyike kwa kushirikiana na Tume ya Mipango kwa kuwa ndicho chombo kilichopewa mamlaka ya kisheria kufanya hivyo.
Alifafanua kuwa Wizara zinaweza kubuni miradi na kuishirikisha Tume hiyo ambapo ndio itakayofanya uamuzi wa kuingiza mradi husika katika mpango wa maendeleo wa nchi.
Dk.Shein alitumia fursa ya kikao hicho kusisitiza wito wake wa kutaka utekelezaji wa zoezi linaloendelea sasa la kuwapanga katika madaraja watumishi kwa mujibu wa Miundo ya Utumishi wa wafanyakazi wa Umma.
Alisema ni muhimu kwa Wizara kuimarisha kitengo chake kinachoshughulikia zoezi hilo kwa kuweka watu makini, waadilifu, wanaojituma na wanaojali wakati ili kuweza kufualitia kwa karibu utekelezaji wa zoezi hilo katika Wizara na Idara za serikali.
Katika maelezo yake ya awali katika kikao hicho yaliyosomwa na Katibu Mkuu Bi Fatma Gharib Bilal, Kaimu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Kazi na Utumishi wa Umma Haji Omar Kheri alieleza kuwa katika kipindi cha miezi tisa iliyopita jumla ya watumishi wa umma 263 wamepatiwa mafunzo ya muda mrefu katika ngazi za msingi, cheti na stashahada katika chuo cha Utumishi wa Umma.
Watumishi wengine 116 kutoka wizara mbalimbali alisema wamepatiwa mafunzo ya muda mrefu na muda mfupi nje ya nchi miongoni mwao 9 ni wa shahada za pili na waliobaki 107 mafunzo ya muda mfupi.
Kwa upande wa maadili ya kazi alisema katika kipindi hicho jumla ya watumishi wapya 195 kutoka taasisi mbalimbali za Serikali Unguja na Pemba wamepatiwa mafunzo ya maadili kazini.
Kaimu Waziri huyo ambaye pia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Idara Maalum alieleza pia kuwa katika kipindi husika jumla ya nafasi za ajira 568 zilitolewa na usaili wake umefanyika Unguja na Pemba.
Alibainisha kuwa kwa upande wa sekta binafsi jumla ya vijana 340 wamepata ajira katika sekta ya utalii hususan hoteli, wengine 410 wamepata fursa za ajira kupitia kampuni ya Danaos na vijana wengine 711 wamepata ajira nje ya nchi katika nchi za Djibout, Qatar, Oman, Saudia, Umoja wa Falme za Kiarabu na Yemen.
Kuhusu ukaguzi wa masuala ya usalama na afya makazini, Waziri alieleza kuwa jumla ya sehemu za 120 zimekaguliwa na miongozo imetolewa kwa waajiri na waajiriwa juu ya umuhimu wa kuzingatia mazingira bora ya afya na usalama kazini.
Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822