Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akisalimiana na Balozi Mdogo Mteule wa Oman aliyepo Zanzibar Bwana Ali Radhid anayetarajiwa kuanza kazi zake Zanzibar baada ya kukamilisha taratibu wa Kidiplomasia.Kati kati yao ni Mjumbe Maalum wa Serikali ya Oman Bwana Yahya Al –Ureim aliyefika Zanzibar kuwasilisha ombi la Serikali yake la kutaka kufanyika kwa Mkutano wa Kimataifa wa Wafadhi kwa ajili ya Zanzibar.
Mjumbe Maalum wa Serikali ya Oman Bwana Yahya Al –Ureim kati kati akimtambulisha rasmi Balozi Mdogo Mteule wa Oman hapa Zanzibar Bwana Ali Rashid kwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Vuga Mjini Zanzibar.
Mjumbe Maalum wa Serikali ya Oman Bwana Yahya Al –Ureim akiwasilisha ombi la Serikali yake la kutaka kufanyika kwa Mkutano Mkubwa wa Kimataifa wa Wafadhi kwa ajili ya Zanzibar. Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ.
Othman Khamis Ame
Mkutano mkubwa wa Kimataifa wa Wafadhili { Donor Conference } kwa ajili ya kustawisha Maendeleo ya Kiuchumi na Kijamii ya Zanzibar unatarajiwa kufanyika robo mwaka ya mwisho ya mwaka huu hapa Zanzibar baada kukamilika kwa mfungo wa mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Mkutano huo utakofadhiliwa na Serikali ya Oman unatatarajiwa pia kujumuisha Wawekezaji wa sekta ya fedha na uchumi kutoka Mataifa na Taasisi tofauti Duniani .
Mjumbe Maalum wa Serikali ya Oman Bwana Yahya Al – Ureim alieleza hayo wakati akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar kuwasilisha ombi rasmi la Oman la kutaka kugharamia Mkutano huo.
Bwana Yahya alimueleza Balozi Seif kwamba taratibu zimeanza kuchukuliwa katika kuona wafadhili pamoja na Wawekezaji wa Mataifa ya Ulaya, Carribean na Afrika wanashiriki katika Mkutano huo.
“ Mambo mawili yatakayobeba Mkutano huo wa kimataifa katika kusaidia ustawi wa Uchumi wa Zanzibar yatajikita zaidi katika masuala ya ufadhili pamoja na uwekezaji “. Alifafanua Bwana Yahya.
Mjumbe huyo Maalum wa Serikali ya Oman alifahamisha kwamba ujio wake hapa Zanzibar tayari ameshakutana kwa mazungumzo ya awali na Viongozi wa ngazi za juu wa Wizara ya Fedha Zanzibar ili kuanza maandalizi ya kuratibu sulala hilo.
Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alielezea faraja yake kutokana na wazo hilo la Serikali ya Oman lenye kuonyesha upendo wa uhusiano wa muda mrefu uliopo kati ya pande hizo mbili.
Balozi Seif alisema uamuzi huo wa Oman umekuja wakati muwafaka kwa vile unalenga kusaidia kustawisha Maendeleo ya Wananachi wa Zanzibar ambao wamekuwa na mafungamano makubwa na ndugu zao wa Oman.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimuhakikishia Mjumbe huyo Maalum wa Serikali ya Oman kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itajitahidi kutoa kila msaada utakaostahiki wa ushirikiano katika kuona Mkutano huo wa Kimataifa wa Wafadhili kwa ajili ya Zanzibar unafanikiwa vyema.
Balozi Seif ameendelea kuipongeza Serikali ya Oman kwa misaada yake mbali mbali ya Maendeleo inayotoa kwa Zanzibar ikiashiria Historia ya muda mrefu iliyopo kati ya pande hizo mbili.
Alisema Zanzibar na Oman zimekuwa na Uhusiano wa miaka mingi unaotokana na maingiliano ya kidamu ya wananchi wake.