Quantcast
Channel: ZanziNews
Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Dhana ya utawala bora ikikosa mwega

$
0
0

Na A K Khiari

Moja katika utaratibu mzuri aliojiwekea Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein, ni utaratibu wa kukutana na watendaji katika wizara zake kila baada ya miezi mitatu ili kuweza kupata kujua yanayojiri katika wizara hizo yakiwemo mafanikio, matatizo na changamoto zinazowakabili.

Utaratibu huu pia humpa picha nzuri Mheshimiwa Rais kuweza kwanza kuwasikiliza watendaji wake na kisha kutoa maagizo na maelekezo ya nini kipewe kipaumbele na yepi ya kuzingatiwa katika kutekeleza maagizo ya Rais katika programu ya mpango kazi.

Kwa utaratibu huu, lazima tumpongeze Rais wetu kwa kuweza kuwa karibu na watendaji  bila ya kupitia Mawaziri au Makatibu wake na kupata maelezo ya moja kwa moja kutoka kwa wahusika wa ngazi za chini kama wakurugenzi na kadhalika.

Ni katika utaratibu huu tumeweza kuona jitihada za watendaji wanavyokuwa makini katika kuziandaa ripoti za kuweza kumweleza Mheshimiwa Rais juu ya yaliyojiri katika vitengo vyao.

Naamini kuna mengi mazuri yamejitokeza katika utaratibu huu na ndio maana Mheshimiwa Rais amekuwa akiuendeleza kila baada ya miezi mitatu na hivyo kuwapa watendaji majukumu ya ziada ya kujipanga wakati wanapokwenda kuonana na Rais.

Katika mrejesho ambao kwa mtu aliye mbali na jikoni (Ikulu) ambaye hupewa kila kinachokubalika kutolewa na Ikulu kwa waandishi wa habari ni kwamba kumeonekana kwamba Ikulu sasa si mahala tena ambapo kulipokuwa mbali na watendaji ambapo kufika sehemu muhimu kama ile huwa ni nadra sana. Sasa kila baada ya miezi mitatu hufika pale.

Ni mwanzo na hatua nzuri ya kupongezwa kwa Rais wetu.
Hata hivyo kuna jambo ambalo bado linanipa uzito katika kuamini kwamba utaratibu huu hauna changamoto ambazo zinaweza kukwamisha na kuleta tija inayokusudiwa kwa sababu zifuatazo.

Kwanza

Ninaweza kujiaminisha kwamba washauri wa Rais huwa wanafanya tathmini kila baada ya miezi mitatu kuangalia utaratibu huu na kufanya mrejesho ( feedback) jinsi wanavyouona ila siioni sehemu yoyote inayoonesha kuwepo kwa kuhakikiwa Ripoti hizi ili kuona maendeleo yale (Progressive) isije kuwa na umahiri tu wa kuandikwa ripoti hizi ila panapokuja utekelezaji ni kwamba kama hubakia kwenye ripoti tu.

Je Mhe Rais ameweza kujipangia utaratibu mwengine wa kuchagua japo  baadhi ya ripoti hizi (randomly) na kufanya ziara hasa za ghafla (field) kuweza kujionea hali halisi ili akapata picha ya kinachoendelea (reality on the ground) ili alinganishe na anacholetewa? Au ameridhishwa na maelezo ya watendaji wake na hivyo hakuna haja ya kufuatilia zaidi? Ninafahamu kutingwa kwa majukumu mengi kwa Mhe Rais lakini akipata muda japo mdogo basi ni vyema tungelimuomba angeliutumia katika kuhakikisha anapata kuona upande mwengine wa shilingi.

Khalifa Umar ibnul Khattaab, alipokuwa Kiongozi wa Waislamu (Amiirul Muuminiin), alikuwa akitoka usiku kwenda kukagua na kujionea mwenye hali halisi ya wananchi wake. Alifika Marikiti kuhakikisha kwamba maagizo aliyokuwa akiyatoa yanatekelezwa na hakuridhishwa tu na kutoa, maagizo na kisha kusubiri ripoti, alijiwekea utaratibu maalum wa kukagua yeye mwenyewe.

Pili

Sijui kama iliwahi kuripotiwa ila sijapata kusikia au kwa waandishi wa Rais kutoa maelezo kwamba Ripoti fulani imekataliwa na Rais kwa sababu A, B C. Wakati mwengine ripoti ukisomewa tu kwa mtu mwenye akili yenye upeo wa kuona mbali inakupa picha halisi kwamba hapa kuna kitu kina walakini. Niliwahi kumuona Rais wa Jamhuri ya Muungano, Jakaya Kikwete, akiikataa rasmi ripoti ya mafuriko yaliyotokea Morogoro mwaka jana papo hapo tena mbele ya hadhara ilipotolewa na kumuamuru Mkuu wa Mkoa kwenda kuiandika upya ili ikidhi vigezo vya kuwa ripoti.
Ushahidi uliomsukuma Rais Kikwete kuikataa ripoti ile ni kwamba kila ilipokuwa ikisomwa wananchi waliguna na kuzomea na hapo mheshimiwa Rais kuhisi kuna namna.

Watendaji wako wanapokuja Ikulu, mhe Rais hawana wa kuwazomea wala wa kuguna ili kukushtua kwamba kilichomo kwenye ripoti hizi kina walakini. Lakini upeo wako wa kufahamu mambo na kuyapima yanaweza kukupa taswira kwamba sasa tumepata mabingwa wa kuandika ripoti zilizokosa dira ya utendaji uliotukuka.

Utendaji wa aina hii hauwatii tumbo joto wahusika na kujenga mazingira kinachotakiwa  si ripoti bora bali bora ripoti.

Tatu

Miongoni mwa dhana za utawala bora ni dhana ya uwazi (transparency) na dhana ya uwajibikaji (accountability). Dhana hizi mbili ni muhimu sana katika kujenga taifa litakalokuwa imara na kuwa na maadili ya kusimamia mikakati na maazimio ya Serikali husika na kujenga umuhimu wa kujua wajibu na majukumu ya kila mmoja na kuhakikisha anayetekeleza ipasavyo.

Azma ya Rais wetu katika kuhakikisha haya yanakuwepo ni kuanzishwa Wizara maalum inayosimamia utawala bora.

Sijaona bado dhana ya uwazi au uwajibikaji katika uwasilishaji  wa ripoti hizi na feedback zake endapo yale yaliyopangwa kutekelezwa na Wizara fulani yameshindwa kutekelezeka na kuundiwa sababu za kushindwa na sababu hizi kuonekana si za msingi. Je mara zote watapewa fursa nyengine  wakajirekebishe? Au wataweza kuwajibishwa?

Dk.  Shein alipokutana na watumishi wa Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi aliwataka kuifahamu vyema dhana ya utawala bora ili wawe mfano wa kuigwa katika kuitekeleza dhana hiyo kwa vitendo.

Kama ni dhana ya utawala bora, basi inahitaji kuonekana kwa vitendo si kwa watumishi tu bali tokea kwa mheshimiwa Rais mwenyewe akionesha vipi anaisimamia dhana hii si kinadharia tu bali katika uhalisia wake.

Ikiwa Mhe Rais keshaonesha njia, anatakiwa kuwa mstari wa mbele na kutokuwa na kumsalia Mtume wala kuwa na muhali kwa wote wanaokwenda kinyume na dhana hii na hapo atajenga kigezo bora na nguzo muhimu kwa walio chini yake kuitekeleza dhana kikamilifu kwa mujibu wa taratibu zilizopo.

Mhe Rais, ni kweli kama ulivyowazindua watendaji kwamba wasifike wakati watumishi wakajiona kuwa wao ni watu wasioguswa na wasiohojiwa, mbona tayari wapo!!!.Ndiyo maana tunakuzindua jaribu kufanya ziara za ghafla ukajionee hali halisi!.

Vyenginevyo mhe Rais, hii itabakia kuwa ni dhana tu iliokosa meno na iliokosa mwega wa kuisimamia ikaweza kuisaidia serikali ili isimame katika kutekeleza misingi hii miwili muhimu ya uwazi na uwajibikaji na kupatikana kwa utawala bora.

Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>