STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 13 Mei, 2014
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Serikali imesema itaendelea kuchukua hatua kila inapowezekana ili kuimarisha mazingira ya kazi pamoja na maslahi ya watumishi wa vikosi vya Idara maalum vya SMZ lengo likiwa ni kuviwezesha vikosi hivyo kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi na kwa weledi zaidi.
Akizungumza katika hafla ya ufungaji wa Mafunzo Maalum ya Maofisa wa Idara hizo na kutoa Kamisheni kwa wahitimu leo, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein alisema dhamira ya Serikali ni kuhakikisha mazingira ya Idara hizo yanalingana na mazingira ya sasa ya utendaji kazi ambayo yanayozingatia maendeleo ya sayansi na tekinolojia.
“Serikali itafanya kila jitihada ili wapiganaji wetu tuweze kuwaandalia mafunzo ya fani mbalimbali hasa yanayoendana na sayansi na tekinolojia kwa kuwa azma yake ni kuwa na Idara za SMZ zenye nyenzo na vifaa vya kisasa vya kufanyia kazi ili kuziwezesha kutekeleza majukumu yake ipasavyo”Dk. Shein alieleza.
Alieleza kuridhishwa kwake na kazi nzuri inayofanywa Idara hizo katika kutekeleza majukumu yake yakiwemo ya kusimamia amani na utulivu, ulinzi wa uchumi, kusaidia kutoa huduma za jamii kama vile afya na elimu pamoja na huduma wakati wa maafa.
Dk. Shein aliwapongeza askari wa Idara hizo Maalum kwa kukabiliana vyema na magendo ya karafuu ambapo alieleza matokeo ya jitihda zao ni kuongezeka kwa pato la Serikali.
Hata hivyo alizitaka Idara hizo kuongeza kasi ya ulinzi hasa kukabiliana na vitendo vya baadhi ya wafanyabiashara wanaokwepa kodi kwa kuingiza na kupitisha bidhaa kinyume na sheria.
“Lazima tuongeze jitihada katika kukabiliana na vitendo hivi ambavyo vinalikosesha taifa kiasi kikubwa cha mapato kutokana na uingizaji na upitishaji wa bidhaa kupitia bandari zisizo rasmi” Dk. Shein alisisitiza.
Kwa upande mwingine alitoa wito kwa wananchi kutoa ushirikiano kwa vikosi vya ulinzi na usalama ikiwa ni pamoja na Idara Maalum za SMZ ili kukomesha hujuma hizo na uhalifu mwingine na kuwakumbusha kuwa suala la ulinzi wa nchi ni jukumu la kila mwananchi.
Katika hafla hiyo iliyofanyika huko katika kambi ya KMKM iliyopo Kama Wilaya ya Maghribi Unguja, Dk. Shein aliwataka wahitimu wa mafunzo hayo kuthibitisha kwa vitendo kile walichojifunza kwa kutekeleza wajibu wao kwa uadilifu na uaminifu mkubwa.
Kwa upande wake Mkuu KMKM Comodor Hassan Mzee alieleza kuwa askari waliopewa kamisheni wamejengewa uwezo mkubwa kupitia mafunzo hayo ambapo sasa wana uwezo wa kuongoza vyema askari walio chini yao.
Akitoa maelezo kuhusu mafunzo hayo Mkuu wa Mafunzo Mohamed Ali Bakari alieleza kuwa wahitimu wote wamemaliza vyema mafunzo yao kwa kufaulu mafunzo ya vitendo na nadharia darasani.
Alieleza kuwa jumla ya wahitimu 97 kati ya washiriki 100 wamemaliza mafunzo hayo ambao ni kutoka Idara tatu za SMZ ambazo ni Jeshi la Kujenga Uchumi-JKU, Kikosi cha Valantia-KVZ na KMKM.
Katika hafla hiyo ambayo ilihudhuriwa pia na Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Iddi, Dk. Shein alitoa kamisheni kwa wahitimu, zawadi kwa wahitimu waliofanya vyema, alikagua gwaride, na pia kuangalia maonesho kutoka askari wa Idara hizo.
Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822