Na Kazija Ramadhan
SHIRIKISHO linalosimamia michuano ya kombe la dunia kwa nchi ambazo si wanachama wa FIFA, Conifa la nchini Sweeden limelazimika kufanya marekebisho ya ratiba kufuatia timu ya taifa ya Zanzibar ‘Zanzibar Heroes’ mpaka muda huu kutokua na uhakika wa kuelekea kwenye michuano hiyo.
Kwa mujibu wa mtandao wa Conifa Zanzibar ambayo ilikuwa iyanze safari ya kushuka dimbani June 2 dhidi ya timu ya taifa ya Ellan Vannin ratiba mpya inaonyesha kuwa siku hiyo kutakuwa na pambano kati ya Ellan Vannin dhidi ya Contea de Nissa.
Mabadiliko haya ya ratiba yanamaanisha kuwa huenda maombi ya mwisho yaliyotumwa na ZFA kwa rais wa Conifa juu ya kupatiwa tena ufadhili wa kuipeleka timu hiyo nchini Sweeden umegonga ukuta na sasa Zanzibar itabakia kuwa mwanachama tu wa Shirikisho hilo huku ikisubiri hadi mwaka 2016 ambapo michuano hiyo itafanyika tena na pengine hapa visiwani Zanzibar.
Heroes imeshindwa kushiriki michuano hiyo kwa madai ya kuwa kocha aliyetakiwa kuunda kikosi hicho Shaaban Ramadhan alishindwa kuwasilisha majina ya wanandinga hao mapema huku akisema wazi kuwa hayuko tayari kufanyakazi na msaidizi wake Hafidh Muhiddin aliyeteuliwa na ZFA kutoka kisiwani Pemba na chaguo lake ni kocha wa KMKM, Ali Bushiri.