STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 03 Juni, 2014
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesisitiza umuhimu wa mawaziri kujibu maswali yanayoulizwa na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kwa hoja na kwa umakini mkubwa ili kufanikisha utekelezaji wa wajibu wa Baraza la kuisimamia Serikali.
Amesema si jambo la busara hata kidogo kwa Waziri kujibu maswali ya Wajumbe wa la Wawakilishi bila majibu yenye kujitosheleza na kueleza kuwa ni vyema kwa waziri anapokosa majibu Barazani kuomba kupewa muda ili ajibu swali husika kwa maandishi.
Dk. Shein alibainisha kuwa waziri kuomba kupewa muda kujibu swali kwa maandishi ni utaratibu unaotumiwa na kufaa katika mfumo wa kidemokrasia wa vyombo kama hivyo vya kutunga sheria lakini alisisitiza kuwa ni lazima waziri kutimiza ahadi yake kwa vitendo.
Rais ameeleza hayo leo wakati alipokuwa akizungumza kwenye hafla ya kuwapongeza viongozi wa wizara tatu zilizo chini ya Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kufuatia kukamilisha na kupitishwa kwa bajeti za Wizara hizo.
“Jitahidini kujibu hoja za wajumbe kwa ufanisi, kwa umakini na kwa hoja na kuepuka majibu yasiyoridhisha kwani Wawakilishi wanapouliza maswali wanauliza kwa niaba ya wananchi”alisisitiza Dk. Shein.
Kwa hivyo alihimiza ushirikiano wa karibu kati ya mawaziri na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kwani kufanya hivyo alisema ni kufanikisha shughuli za serikali kwa faida ya wananchi.
Aliwataka mawaziri kuonesha umahiri wao katika kujibu maswali hasa yale ya nyongeza ambayo yanatanguliwa na maswali ya msingi ambayo majibu yake kwa kawaida huwa yametayarishwa mapema na kusomwa Barazani.
“Mawaziri wanapojibu maswali ya msingi ambayo yametayarishwa lazima wajiandae kwa kutabiri maswali ya ziada yatokanayo na maswali ya msingi na kufanya hivyo ndio waziri anapoonesha umahiri na umakini wake” Dk. Shein alisema.
Katika hotuba yake hiyo fupi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi aliwapongeza viongozi na watendaji wa Wizara hizo tatu kwa kuweza kutayarisha bajeti za ofisi zao na hatimae kupitishwa na Baraza.
Wizara hizo ni Wizara ya Nchi,Ofisi ya Rais Ikulu na Utawala Bora, Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Idara Maalum za SMZ na Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Kazi na Utumishi wa Umma.
Alibainisha kuwa kipindi cha bajeti ni kipindi muhimu kwa serikali na wizara zake kwa kuwa bajeti ndio uhai wa serika li hivyo kitendo cha wizara kufanikisha bajeti yake na kupitishwa na Baraza ni kitu cha kujivunia.
Katika mnasaba huo, Dk. Shein amezikumbusha wizara wajibu walionao katika kutekeleza mipango ya wizara kwa mujibu wa bajeti na kusisitiza kuwa huu sasa ni wakati wa kuongeza kasi katika utendaji ili kufanikisha malengo ya bajeti.
Alisisitiza umuhimu wa viongozi wa wizara na Idara za Serikali kuongeza kasi na uwezo wa kusimamia utekelezaji wa bajeti hiyo na kuonya kuwa pasi na usimamizi mzuri kunaweza kusababisha malengo ya wizara kutofikiwa.
Sambamba na pongezi kwa Wizara hizo Dk. Shein amezishukuru Kamati tatu za Baraza la Wawakilishi kwa kusimamia vyema bajeti za Wizara hizo.
Amezitaja kamati hizo kuwa ni Kamati ya Katiba na Sheria, Kamati ya Kudumu ya Kusimamia Shughuli za Ofisi za Viongozi Wakuu wa Kitaifa na Kamati ya Kuchunguza na Kuthibiti Hesabu za Serikali na Mashirika(PAC).
Akitoa shukrani kwa niaba ya Wizara hizo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Kazi na Utumishi wa Umma, Haroun Ali Suleiman aliahidi kuwa Wizara hizo zitaendelea kufanyakazi kwa bidii ili kukamilisha malengo ya Wizara pamoja na kuzingatia mapendekezo na maelekezo yaliyotolewa na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wakati wa kujadili bajeti hizo.
Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822