Na Salim Said Salim
TABIA ya mtu kufanya vitendo vya kuchekesha wengine (comedy) ina umuhimu wake katika maisha ya binadamu, kwani bila ya burudani hii maisha hukosa raha na furaha.
Lakini vichekesho vya aina yoyote ile huwa havifai kwa masuala muhimu kama yale yanayogusa maslahi au mustakabali wa taifa.
Katika siku za karibuni tumeshuhudia vichekesho vya aina yake kutoka kwa baadhi ya viongozi wa serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Navyo ni vya kuwataka wajumbe wa Bunge la Katiba wa kundi linalojuikana kama Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) kurudi bungeni kujadili rasimu ya pili ya mapendekezo ya katiba iliyotolewa na Tume ya Jaji Joseph Warioba.
Baadhi ya viongozi hawa, kama Rais Jakaya Kikwete, Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Gharib Bilal na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Ali Vuai walikaa kimya pale lilipotoka tamko rasmi la CCM kuwa hata UKAWA wakijitenga wajumbe wa Bunge la Katiba ambao hawakukaa pembeni wataendelea na mchakato wa kutafuta katengeneza katiba mpya.
Lakini hivi sasa kila siku unamsikia mmoja baada ya mwingine akiwataka UKAWA warudi bungeni.
Kama kweli viongozi wa Serikali ya Muungano na ya Zanzibar na CCM walikuwa wanaona umuhimu wa kuwa na mtandao mpana zaidi kutengeneza katiba, ilikuwaje hata wakawa na ubavu wa kutoa tamko lile baada ya kikao cha Kamati Kuu ya CCM?
Kwa mfano Vuai alipokuwa akipokea vifaa vya kikundi cha bendi cha Umoja wa Vijana wa CCM kutoka China aliwataka wajumbe wa UKAWA kurudi bungeni kufanya kile alichokieleza kama kutekeleza kazi waliyotumwa na wananchi.
Kwanza sijui Vuai na wenzake katika CCM na serikali wangelisemaje kama serikali yoyote ile ingelitoa msaada kwa CUF, CHADEMA au NCCR-Mageuzi.
Nina hakika ingelikuwa nongwa na tungelisikia taarifa kali za serikali na CCM za kuitaka serikali ya hiyo nchi iliyotoa msaada isiingilie mambo ya ndani ya Tanzania na isijihushe na mambo ya siasa ya nchi hii.
Lakini kwa nchi ya kigeni kuisaida CCM ni sawa, lakini ni dhambi kwa msaada kama huo kupewa wapinzani. Hii ndiyo CCM… watende au watendewe wao na wakitenda au kutendwa wengine huwa mwao.
Vuai alipokuwa akipoea zawadi hizo aliwataka UKAWA kurudi bungeni. Hivyo hili suala la Katiba ya Tazania linaihusu vipi China?
Kama kweli Vuai alikuwa anazungumza kwa nia safi na sio kufanya kichekesho basi angeliwatafuta viongozi wa UKAWA na kuwapa ujumbe huo na sio kupitia Serikali ya China.
Lakini kichekesho kikubwa zaidi ni ile kauli ya Vuai ya kutaka UKAWA wakaifanye kazi iliyowapeleka wajumbe wa umoja huo katika Bunge la Katiba.
Wanachojua Watanzania ni kuwa Bunge la Katiba lilikuwa lijadili rasimu iliyowasilishwa na Tume ya Katiba na sio rasimu inayoletwa na CCM kama ilivyotokea na kusababisha wajumbe wa UKAWA kulisusia hilo Bunge ambalo kazi yake imebadilishwa.
Watanzania walitarajia Bunge kujadili rasimu iliyowasilishwa na sio mambo mapya au mjadala wa kejeli na matusi.
Kama lile lilikuwa Bunge lilioitishwa maalumu kutengeneza kamusi ya matusi ya lugha ya Kiswahili ni sawa kwani mjadala wa rasimu ya katiba ulikuwa umewekwa upande.
Kama Vuai haelewi inapaswa afahamu kuwa Watanzania walitarajia mapendekezo yaliyokuwemo ndani ya rasimu ambayo yalitokana na maoni yao yaliyotolewa kutoka kila pembe ya Jamhuri ya Muungano, ndiyo yaliyokuwa yajadiliwe na Bunge la Katiba na sio kile kinachotakiwa na CCM.
Tanzania ni nchi ya hao waliotoa maoni yao kwa Tume ya Katiba na sio ya CCM au chama chochote kile cha siasa. Kwa CCM kuwa chama tawala haipaswi kuwa nongwa na kutaka kuwalazimisha watu wakubali jambo ambalo ni kinyume na mapendekezo waliyotoa na kuwasilishwa na tume.
Zama za kutumia mabavu kwa kujifunika muamvuli wa kidemokrasia zimepitwa na wakati na aliyekuwa kiongozi wa China, Mao Tse-tung (baadaye jina lake lilibadilishwa na kuandikwa Mao Dze dung) alisema popote pale panapokuwepo ukandamizaji, basi huwepo upinzani (Where there is oppression there is always resistance).
Kinachotokea katika Bunge la Katiba ndio hicho alichokieleza Mao, na upinzani utatoweka tu pale ukandamizaji na mabavu ukitoweka.
Hapana ubishi juu ya umuhimu wa mchakato wa kutafuta katiba kuwa na wigo mpana, lakini hili lazima lifanyike kwa mujibu wa makubaliano na maridhiano na sio mvutano.
Tatizo lililojitokeza Dodoma ni kwa CCM kuonyesha kuwa ina nguvu za misuli na sio nguvu za hoja.
Kitendo cha kukataa moja ya sharti muhimu la utawala bora na demokrasia ya kweli la kutumika kura ya siri kufanya maamuzi, ni kielelezo cha kutoheshimu demokrasia.
Kama viongozi wa CCM kweli wanaamini kuwa kura ya wazi ndiyo demokrasia ya kweli, basi kwanza wangeonyesha mfano ndani ya chama chao kwa chaguzi zao, kama za kutafuta wagombea, kwa kutumia kura za wazi.
Ukweli ni kwamba serikali bado haijakuwa na utamaduni wa kuheshimu maoni ya wananchi na hili limeonekana kwa mapendekezo yaliyotolewa na tume nyingi zilizopewa kazi ya kukusanya maoni.
Ni vyema kwa CCM ikaacha kufanya vichekesho kwa masuala muhimu ya kitaifa na kuanza kuheshimu maoni yanayotolewa na wananchi.
Kuwalaumu UKAWA kwa kutaka Bunge la Katiba lijadili rasimu iliyowasilishwa na sio rasimu ambayo haitokani na mapendekezo yaliyokuwemo katika rasimu ni kutowatendea haki Watanzania.
Hiki ni kichekesho ambacho hakina faida wala maslahi kwa nchi. Mambo ya kitaifa hayafai kufanyiwa vichekesho au mchezo wa kuigiza.
Kwa suala la mchakato wa katiba wanapaswa kujirekebisha na wajumbe wake kufanya kazi wanayoitarajia Watanzania, kuachana na kupandikiza mambo mapya katika rasimu na kujadili yale yaliyokuwemo katika rasimu.
Historia haitawasamehe wale waliosababisha Bunge la Katiba kuwa la mvutano badala ya maridhiano na hatimaye wajumbe wa UKAWA kutoka nje.
Kuwatarajia UKAWA kurudi bungeni kujadili kitu ambacho hakimo kwenye rasimu ya katiba iliyowasilishwa na Tume ya Jaji Warioba ni kichekesho ambacho hakikubaliki.
Sio vibaya kufanya vichekesho au mzaha wa aina yoyote ile kwa baadhi ya mambo, lakini sio kwa suala muhimu kama la kutafuta katiba mpya ya nchi. Hata katiba ya kikundi cha ngoma haitaki mzaha au kichekesho!
Kwa yaliyokwishatokea Dodoma katika awamu ya kwanza ya kutafuta katiba mpya sio kuteleza, bali ni kuanguka.
Kama kweli tunakusudia kuwa na katiba yenye maridhiano na itakayozingatia maoni yaliyotolewa na wananchi, basi njia pekee ya kulivusha jahazi letu kwa salama katika safari yetu hii ni kujadili rasimu na sio mambo mapya.
Kosa limefanyika, iwe kwa makusudi au kwa kutaka kufanya kichekesho. Tujisahihishe na kama hatukufanya hivyo, basi kupata katiba yenye maridhiano itabaki kuwa ndoto.
Tuache kutumia mabavu na badala yake tuwe watu wenye hekima na busara, na tuweke mbele maslahi ya nchi na sio ya vyama vya siasa.
Vile vile tujiepushe na matusi kwani hayaleti maelewano bali hupalilia mfarakano
Chanzo : Tanzania Daima