Na Hafsa Golo
SERIKALI imeitetea Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka, kuhusu begi za dawa za kulevya zilizotelekezwa sehemu ya kuondokea abiria katika uwanja wa ndege wa Zanzibar,ikisema taasisi hiyo haipaswi kubebeshwa lawama.
Waziri wa Sheria na Katiba, Aboubakar Khamis Bakary, alisema hayo jana wakati akihitimisha bajeti yake na kujibu hoja mbali mbali za Wawakilishi katika mkutano wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2014/2015.
Alisema wanaopaswa kulaumiwa ni maofisa wa uwanja huo kwa kuruhusu mtu kuingia na mabegi hayo hadi sehemu ya kuondokea abiria bila kujulikana.
Alisema taarifa alizonazo ni kwamba kamera za usalama zilizopo uwanjani hapo (CCTV) hazikuweza kuwabaini walioingiza dawa hizo, hivyo hakuna sababu ya kuitupia lawama ofisi ya DPP kwa kuwa kazi yake ni kushitaki pekee na wala si kufanya uchunguzi.
Kuhusu mauaji ya askari polisi yaliyotokea Bububu, pia alisema DPP hapaswi kulaumiwa kwa sababu jalada la kesi lililopelekwa na polisi kwa Mwendesha mashtaka, halikuwa na vielelezo vinavyothibitisha kwamba wahusika ndio waliotekeleza mauaji ya askari huyo, badala yake jalada lilianisha kosa la kuchoma matairi na kuharibu barabara.
Hata hivyo, alisema kuna haja ya polisi kufanya uchunguzi wa kina kuhusu matukio mbali mbali ya kihalifu ili kuondoa lawama zinazojitokeza sambamba na maofisa wa jeshi hilo kujengewa uwezo wa kufanya kazi kitaalamu.
Alisema DPP amekuwa akifanya kazi na kusimamia majukumu yake kwa mujibu wa sheria.
"Kesi zinapokosa ushahidi wa kutosha Mkurugenzi wa Mashtaka hawezi kuzifikisha mahakamani,” alisema.
Kuhusu kesi kuchelewa kupata hukumu, alisema ni pamoja mashahidi kutofika mahakamani na ukosefu wa uchunguzi wa kesi kitaalamu.
Alisema baadhi ya wakati uchunguzi unaofanywa na polisi huwa haujitoshelezi hali inayosababisha mahakama kuzitupilia mbali kesi hizo.
Aidha alisema anachofahamu Katibu wa Tume ya Kurekebisha sheria, anafanya kazi zake kwa weledi mkubwa akishirikiana na Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Mshibe Ali Bakar na katika kipindi kifupi wamezifanya marekebisho sheria nyingi zisizokwenda na wakati.
Wizara hiyo imeomba kuidhinishiwa jumla ya shilingi 11,002,870,000 na tayari bajeti ya wizara hiyo imepitishwa.