Na Fatuma Kitima,Dar es Salaam
WAZIRI wa Maji, Prof. Jumanne Maghembe, amekipongeza kiwanda cha mabomba cha Pipe Industry Ltd, kilichopo Vingunguti jijini Dar es Salaam kwa kutengeneza mabomba mapya kwa teknolojia ya kisasa ambapo kiwanda hicho kitasaidia kupunguza gharama za miradi ya maji.
Aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaama katika ufunguzi wa warsha ya kiwanda cha mabomba iliyoendeshwa na kampuni ya Burouge ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) juu kutambulisha mabomba yanayozalishwa na kiwanda hicho.
Prof.Maghembe alisema ni faraja kubwa kwa Tanzania kwa kujengwa kiwanda hicho chenye ubora wa kimataifa na ni jambo zuri kwa kuwa teknolojia hiyo mpya ipo nchini.
“Tumekuwa tukitumia pesa nyingi kuagiza mabomba kutoka nje hivyo ni matumaini yangu kwa sasa gharama zitapungua kwa kuwa tutakuwa tunayapa hapa nchini,” alisema.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa kiwanda hicho, Seif Seif alisema, kiwanda hicho ni cha aina yake na cha pekee si Tanzania tu bali Afrika Mashariki ya Kati.
Alisema kiwanda hicho kinazalisha mabomba imara ya kisasa kwa kutumia teknolojia ya hali ya juu inayokidhi viwango vya kimataifa.