Mbunge wa Jimbo la Kitope ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akikabidhi Seti ya TV Flat Screen kwa Timu ya Soka ya Mwache Alale United baada ya kuibuka na ushindi wa godi 5 – 3 dhidi ya African Boys ya Upenja kwenye mchezo wa Fainal ya Kombe wa Zaweda.
Pambano hilo lilichezwa katika uwanja wa Kitope na kushuhudiwa na Mbunge huyo Balozi Seif.
Nahodha wa Timu ya Soka ya Mwache Alale Abdullghani Gullan akipokea kikombe kutoka kwa Mbunge wa Jimbo la Kitope Balozi Seif Ali Iddi mara baada ya timu yake kuibuka na ushindi wa 5-3 dhidi ya African Boys ya Upenja.Picha na Hassan Issa wa –OMPR – ZNZ.
Na Othman KHamis Ame, OMPR
Hatimae Timu ya Soka ya Mwache Alale United imeibuka na ubingwa wa mashindano ya Kombe la Zaweda ndani ya Jimbo la Kitope baada ya kuilaza Timu ya African Coast ya Upenja kwa mabao 5 – 3 yaliyopatikana kwa njia ya Penalti katika pambano la fainali lililochezwa kwenye uwanja wa Kitope.
Pambano hilo lililokuwa na ushindani mkali kwa timu zote mbili lilichezwa kwa dakika 90 bila ya mshindi lilishuhudiwa na wapenzi kadhaa wa mchezo wa soka wakiongozwa na Mbunge wa Jimbo la Kitope Balozi Seif Ali Iddi.
Mabingwa hao wapya wa Kombe la Zaweda Mwache Alale United walifanikiwa kupata ushindi huo baada ya kufunga Penalti zote tano wakati wapinzani wao African Boys ya Upenja wakapata Penalti tatu na kupoteza moja.
Mgeni rasmi wa pambano hilo Mbunge wa Jimbo la Kitope Balozi Seif alikabidhi zawadi kwa bingwa wa mashindano hayo, mshindi wa pili pamoja na zawadi kwa timu zote zilizoshiriki katika mashindano hayo ambayo ni ya pili kufanyika tokea kuanzishwa kwake mwaka uliopita.
Balozi Seif aliwakabidhi mabingwa wa Kombe hilo Mwacha Alale United Seti moja ya TV, King’amuzi chake, shilingi 300,000/- taslimu, seti moja ya jezi, mpira pamoja na Kikombe cha ubingwa.
Mshindi wa Pili African Boys ya Upenja ikakabidhiwa shilingi laki 150,000/- Taslimu, seti moja ya jezi, pamoja na mpira wakati mshindi wa Tatu Mahonda Kids wakaibuka na Seti moja ya jezi, shilingi 75,000/- taslim pamoja na Mpira.
Mchezaji bora na mdogo kuliko wote katika mashindano hayo alikuwa Said Khamis Kidagaa aliyepata zawadi ya shilingi 20,000/- taslimu na Mfungaji bora wa mashindano hayo Abdull Nyafu wa African Coast ya Upenja alipata zawadi ya shilingi 20,000/-.
Mchezaji bora wa mashindano hayo Ali Alawi na Golkipa bora Siad Abdulla kutoka Timu ya Zaweda wamepata zawadi ya shilingi 20,000/- taslimu kila mmoja wakati zawadi ya shilingi 50,000/- Taslimu kwa timu bora katika mashindano hayo ilichukuliwa na timu ya soka ya Zaweda.
Muamuzi bora wa mashindano hayo aliibuka Haroun Kuchi aliyefanikiwa kupata zawadi ya shilingi 20,000/- taslim pamoja na mpira mmoja mmoja kwa kila timu ilizoshiriki katika mashindano hayo.
Timu zilizoshiriki mashindano hayo ya Zaweda Cup ni pamoja na Mbuyuni, Fujoni Boys, Mahonda Union, Kitope United,Zaweda, Mgambo F.C, Kilimani City, Kibweni Youth Organization, New Star, Mahonda Kids,washindi wa Pili African Boys ya Upenja na Mabingwa wa mashindano hayo Mwacha Alale United.
Mapema Mbunge huyo wa Jimbo la Kitope Balozi Seif alikabidhi zawadi kwa washindi wa mchezo wa Pete wanawake ambapo bingwa ni watanashati wa Kitope waliopata shilingi laki 100,000/- Taslimu, Mpira pamoja na Seti ya Jezi.
Mshindi wa pili wa mchezo huo wa netball ni timu ya wanawake ya kiwengwa iliyozawadiwa shilingi laki 100,000/- Taslimu, Mpira na Seti ya Jezi.
Akizunguma mara baada ya pambano hilo la fainal na zawadi Mbunge huyo wa Jimbo la Kitope Balozi Seif aliwakumbusha wana michezo nchini kuendelea kushikamana katika michezo ili kuleta upendo michezoni na ndani ya Jamii.
Balozi Seif aliwatahadharisha wanamichezo hao kuvitumia viwanja vya michezo kwa mnasaba wa kiungwana na ustaarabu na kuacha tabia ya kuvifanya viwanja hivyo kuwa ni maeneo ya kuporomoshwa kwa matusi.
“ Haipendezi kuona maeneo ya viwanja vya michezo nchini yanakuwa sehemu ya kuporomoshwa matusi ambayo mara nyingi huelekezwa kuwakashifu viongozi wanaowaongoza wanamichezo hao “. Aliasa Balozi Seif.
Aliwapongeza Wanamichezo pamoja na uongozi wa Kamati ya mashindano hayo ya Zaweda Cup kwa juhudi zao zilizosaidia kukamilisha mashindano hayo kwa amani na furaha.
Jumla ya shilingi Milioni 2,700,000/- zimetumika kugharamia vifaa mbali mbali vya mashindano hayo ya Zaweda Cup katika ununuzi wa TV, jezi mipira pamoja na kikombe.