Mjumbe wa Kamati kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Balozi Seif akimkabidhi kadi mwanachama mpya wa CCM Shina nambari 23 la Tawi la CCM Fuoni Bibi Faiza Chande Ameir.
Kushoto ya Balozi ni Mwenyekiti wa Shina Nambari 23 la Tawi la CCM Fuoni Nd. Daudi Khamis, Mwenyekiti wa CCM Mkoa Magharibi Nd. Yussuf Mohd Yussuf na Katibu wa CCM Mkoa huo Aziza Ramadhan Mapuri.
Mwenyekiti wa CCM Jimbo la Mwanakwerekwe Ndugu Khamis Juma Msonge akimkaguza Mjumbe wa Kamat Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Balozi Seif Ali Iddi kuangalia jengo la Ofisi ya Jimbo hilo ambayo iko katika hatua za mwisho za ujenzi wake.
Balozi Seif akiwa mlezi wa Mkoa wa Magharibi Kichama alikuwa katika ziara ya kichama ndani ya Wilaya ya Dimani.
Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ.
Na Othman Khamis Ame, OMPR
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Balozi Seif Ali Iddi alisema kwamba mafanikio ya Uongozi ndani ya Mashina ya Chama cha Mapinduzi ni nguzo pekee inayosaidia uimarishaji wa chama hicho katika ngazi zote.
Alisema hayo wakati akizungumza na wanachama wa Shina nambari 23 la CCM Tawi la Fuoni baada ya kugawa kadi kwa wanachama wapya 15 wa CCM wa Shina hilo akiwa katika ziara ya kutembelea Wilaya ya Dimani Kichama akiwa mlezi wa Mkoa wa Magharibi.
Balozi Seif alisema kwa kuwa chama imara ni kile kinachoungwa mkono na watu walio wengi popote pale aliwapongeza Vijana hao wa shina nambari 23 kwa uamuzi wao wa busara wa kujiunga na Chama cha Mapinduzi.
Alisema nguvu ya Chama ni Vijana ambao pia ni tegemeo kwa Taifa. Hivyo aliwataka waendelee kushikamana pamoja ili kuongeza uzalendo wao katika kulitumikia Taifa lao.
“ Chama cha Mapinduzi daima kitaendelea kuthamini mashina ya CCM Mitaani kwa vile ndio yanayodumisha nguvu na uhai wa chama chenyewe “. Alisema Balozi Seif.
Akizungumzia changa moto zinazowakabili wana CCM na Wananchi wa eneo hilo
Balozi Seif ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema tatizo la bara bara linalowakabili wananchi hao liko katika hatua za mwisho kupatiwa ufumbuzi kwa kuwekwa kifusi ikiwa ni hatua ya mwanzo.
Alisema Uongozi wa Jimbo la Fuoni umeshakamilisha taratibu na idara inayohusika ya ujenzi wa bara bara katika kulifanyia kazi suala hilo linaloleta usumbufu kwa wakaazi wa eneo hilo.
Kuhusu uimarishaji wa kazi za amali kwa ajili ya kuwajengea misingi imara ya ajira wananchi hao hasa kundi kubwa la Vijana Balozi Seif alisema Serikali imeshaanzisha mfuko wa uwezeshaji na itakuwa tayari kutoa mafunzo ya ujasiri amali kwa wananchi watakaoanzisha vikundi vya ushirika.
Hata hivyo Balozi Seif aliwaonya watu wenye tabia ya ujanja wa kuanzisha vikundi vya saccos kwa kutumia mgongo wa wananchi kuacha mara moja mtindo huo unaochangia kuviza maendeleo ya jamii katika maeneo husika.
Katika kuunga mkono juhudi za wanachama hao wa CCM Shina nambari 23 Fuoni Balozi Seif aliahidi kuwapatia seti ya TV Pamoja na King’amuzi chake ili wapate fursa ya kupata habari, burdani pamoja na kuona mashindano ya kombe la dunia yanayoendelea hivi sasa Nchini Brazil.
Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya CCM Taifa akiwa pia ni mlezi wa Mkoa wa Magharibi aliitembelea Ofisi ya CCM Jimbo la Mwanakwerekwe kukagua hatua iliyofikia ya ujenzi wake.
Katibu wa Fedha na Uchumi wa Jimbo hilo ambae pia ni Katibu wa kamati ya ujenzi wa Jengo hilo Ussi Chimbeni Kheir alisema zaidi ya shilingi Milioni saba zinahitajika katika kukamilisha ujenzi wa jengo hilo.
Nd. Ussi Chimbeni alisema hadi hivi sasa gharama halisi za ujenzi huo uliopata msaada kutoka kwa Viongozi, Wana CCM na wafadhili mbali mbali wa Chama hicho umefikia shilingi Milioni 14,714,000/-.
Akizungumza na baadhi ya Viongozi hao wa CCM Jimbo la Mwanakwerekwe Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya CCM Taifa Balozi Seif aliwapongeza wana CCM hao kwa uamuzi wao wa kujenga Ofisi mpya ya Jimbo hilo inayokwenda na wakati.
Katika kuunga mkono juhudi za Viongozi na wanachama hao wa CCM Jimbo la Mwanakwerekwe Mlezi huyo wa Mkoa wa Magharibi Kichama Balozi Seif aliahidi kuchangia shilingi Milioni 1,000,000/- kuunga mkono ukamilishaji ujenzi huo wa Ofisi yao.
Mapema Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Balozi Seif alianza ziara yake kwa kukutana na Uongozi wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Dimani ukiongozwa na Mwenyekiti wa Mkoa wa Magharibi Nd. Yussuf Mohd Yussuf hapo Makao Makuu yake Kiembe Samaki.
Balozi Seif aliwasisitiza Viongozi hao kufanya kazi kwa ushirikiano ili kuondosha tofauti zinazotoa mwanya wa kuleta mgongano na makundi baina ya Viongozi pamoja na wanachama wanaowaongoza.