Na Salim Said Salim
KATIKA siku za hivi karibuni pamekuwepo na taarifa mbalimbali za kusikitisha na kutisha juu ya matendo ya ubakaji na udhalilishaji wa kijinsia Zanzibar.
Baadhi ya watu walionyooshewa vidole kuwa ndio waliohusika na vitendo hivi ni wale ambao ungetarajia kuwa mstari wa mbele kupambana na uchafu huu.
Miongoni mwa wanaodaiwa kuhusika ni wanafamilia za watu waliofanyiwa unyama huu, viongozi wa dini, walimu na askari wa vyombo vya usalama.
Hata baadhi ya viongozi wa hoteli za kitalii visiwani Zanzibar wamedaiwa kuwalinda wanaohusika na vitendo hivyo vinavyofanyika katika hoteli zao wakihofia sifa za hoteli zao kuchafuliwa na hatimaye kuathiri sekta ya utalii.
Lakini kwa bahati mbaya pamesikika taarifa za kuficha uovu huu na hata kuwakingia kifua wanaotuhumiwa, badala ya kuhakikisha kwamba sheria za nchi zinachukua mkondo wake.
Habari za watu hawa kulindwa, tena kwa ujeuri kama vile walivyofanya ni sahihi, zilisikika zikielezwa ndani ya Baraza la Wawakilishi katika kikao cha bajeti kinachoendelea.
Mwakilishi wa Uzini, Mohamed Raza, ameeleza kwa uwazi namna anavyoelewa juu ya ubakaji ulivyofunikwa kombe na Jeshi la Polisi Zanzibar ili mwanaharamu apite.
Raza alielezea namna kiongozi wa jeshi hilo alivyoonyesha jeuri ya kutojali sheria za nchi na kuwa mtumishi aliyekubuhu kwa kukosa nidhamu anayotarajiwa kuwa nayo ofisa wa polisi, hasa katika kutii amri halali anazopewa na mkubwa wake.
Kwa mujibu wa mwakilishi huyo, kamanda huyo alitakiwa aelezee madai ya ubakaji yaliyomkabili askari polisi, badala ya kufungua njia kwa sheria ichukuwe mkondo wake, alifunga mlango kwa ujeuri hilo lisifanyike.
Hii ni kusema huyo afande mkuu aliamua kufanya kazi ya uhakimu badala ya kuacha mchakato wa kutafuta ushahidi na hatimaye mahakama kutoa uamuzi unaofaa.
Kwa mujibu wa Raza, kamanda huyo alimjibu Waziri wa Katiba na Sheria, Abubakar Khamis Bakari, kwamba hakuwa tayari kutoa maelezo juu ya suala hilo kwake kwa kuwa waziri huyo alitokana na Chama cha Wananchi (CUF).
Kama maelezo haya ya Raza ni kweli, hapana sababu ya kuyatilia shaka, hasa kwa vile yamezungumzwa katika chombo chenye heshima kama Baraza la Wawakilishi, basi ni ya hatari na yanakiuka mwenendo wa utawala bora.
Ni vizuri kwa suala hili kupewa uzito unaostahiki na kama kweli limetokea aliyefanya haya awajibishwe kisheria.
Hii ni kwa sababu kulifumbia macho hili ni sawa na kuwaambia watendaji wengine wa serikali kuwa wanaweza kufanya hivyo.
Ina maana tunajishajiisha na utovu wa nidhamu na uvunjaji wa sheria kwa watendaji katika serikali.
Au ndiyo tunangojea atokee mtendaji mwingine wa serikali akatae kufuata maelekezo ya kisheria ya kiongozi anayetoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) ndiyo tuchukuwe hatua?
Hapa inafaa nikumbushe kuwa pamekuwepo tetesi nyingi (inaweza kuwa nyingine ni za uzushi) juu ya mwenendo usioridhika wa baadhi ya viongozi wa Jeshi la Polisi hali inayozusha shaka na kupunguza imani kwa chombo hiki chenye dhamana ya usalama wa raia na mali zao.
Ukiachilia ukimya uliopo juu ya upotevu wa kitara cha dhahabu cha Umoja wa Majeshi ya Polisi ya Nchi za Kusini mwa bara la Afrika (SADC) katika mikono ya uongozi wa polisi Zanzibar, yapo mengi yanayozungumzwa juu ya mwenendo wa jeshi hilo.
Mifano ni orodha hii ndefu, wapo watu wamezungumza hadharani kauli zinazoweza kusemwa ni za hatari na kibaguzi za kutaka visiwa vya Unguja na Pemba vitengane na visiwe nchi moja, Wapemba wafukuzwe Unguja. Watu waliotoa matamshi haya hawajachukuliwa hatua za kisheria.
Mara nyingi pamesikika kauli za kutukana na kukashifu watu, wakiwemo viongozi wakuu wastaafu wa Serikali ya Zanzibar na Muungano, lakini waliofanya hivyo hawakuguswa.
Jeshi la Polisi Zanzibar mara nyingi limezuia mikutano ya hadhara ya vyama vya upinzani kwa kile kilichoelezwa kuwa sababu za kiusalama.
Swali ni kwanini haijawahi kutokea hata wakati mmoja kwa CCM kuzuiliwa kufanya mkutano wake? Je, chama hiki ni cha malaika?
Ajira katika jeshi hilo nayo inalalamikiwa kwa madai kuwa baadhi ya wakubwa wametumia vibaya nafasi zao kuajiri jamaa zao wasio na sifa, mbaya zaidi wanatumia vyeti bandia na wahusika hawajaguswa.
Kama kweli tunaheshimu utawala bora na kutaka kujenga mazingira ya kweli ya utawala wa kidemokrasia, basi masuala haya yote yafuatiliwe na ukweli ujulikane.
Mwisho waliohusika wawajibishwe kisheria na kama baadhi ya taarifa za kulikandia Jeshi la Polisi hadharani ni za uongo basi wahusika nao wawajibishwe, na kama wanayo kinga kwa kuwa waheshimiwa, basi angalau ielezwe kuwa kauli zao sio za kweli.
Katika nchi nyingi hivi sasa, watu mashuhuri na viongozi mbalimbali wanawajibishwa kisheria kwa madai ya kutenda uhalifu, ukiwemo ubakaji wa watoto, wanaodaiwa kuutenda zaidi ya miaka 20 iliyopita.
Kama watu waliofanya uhalifu walikuwa hawataki wawajibishwe kisheria kwa uovu waliotenda, kinga nzuri ilikuwa kutofanya uhalifu huo.
Kila unapovumilia baadhi ya watu kuvunja sheria kwa sababu mbalimbali, basi ni sawa na kusema Zanzibar ni njema na atakayetaka kuvunja sheria avunje na atavumiliwa.
Sheria ni msumeno na haistahili kuwa na ubaguzi wa aina yoyote ile. Siku hizi katika nchi nyingi za kidemokrasia hata viongozi wakuu wa nchi wanatakiwa kuheshimu katiba na sheria za nchi, na kwa hili hakuna kinga.
Tuache kuwalinda wahalifu bila ya kujali vyeo vyao serikalini au katika vikosi vya ulinzi.
Chanzo : Tanzania Daima