HOTUBA YA MAKAMU WA PILI WA RAIS WA ZANZIBAR,
MHE. BALOZI SEIF A. IDDI
KATIKA UFUNGAJI WA MKUTANO WA KUMI NA MBILI
WA BARAZA LA WAWAKILISHI ZANZIBAR
TAREHE 07 AGOSTI, 2013
UTANGULIZI:
1. Mheshimiwa Spika, napenda kuchukua fursa hii adhimu kwanza kumshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa kutuwezesha kwa mara nyingine tena kukutana hapa katika mkutano huu wa Kumi na Mbili wa Baraza la Wawakilishi ambao unamalizika ndani ya mwezi Mtukufu wa Ramadhani kwa mafanikio makubwa sana. Aidha, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuijaalia nchi yetu kuendelea kuwa katika hali ya amani, utulivu, usalama na mshikamano, mambo ambayo ni muhimu kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
2. Mheshimiwa Spika, naomba pia kutoa pongezi zangu za dhati kwako binafsi Mheshimiwa Spika pamoja na Wasaidizi wako wote, wakiwemo Mheshimiwa Naibu Spika na Waheshimiwa Wenyeviti wa Baraza kwa kuendelea kuliongoza Baraza letu kwa busara, hekima na ufanisi mkubwa kwa kufuata misingi ya kidemokrasia na Kanuni za Baraza. Pia, napenda kuwapongeza Wenyeviti na Wajumbe wa Kamati mbali mbali za Kudumu za Baraza la Wawakilishi na Wajumbe wote wa Baraza hili Tukufu kwa kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa hekima na uadilifu mkubwa.
3. Mheshimiwa Spika, kwa heshima kubwa napenda kuchukua fursa hii kumshukuru kwa dhati Kiongozi wetu mpendwa, Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa uongozi wake thabit na imara uliojaa hekima, busara na upeo mkubwa unaozingatia malengo na matarajio ya maendeleo ya nchi yetu.
4. Mheshimiwa Spika, sina budi pia kutoa shukrani nyingi kwa Makamu wa Kwanza wa Rais, Mheshimiwa Maalim Seif Shariff Hamad kwa kumshauri na kumsaidia vyema Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi katika kuiongoza nchi yetu kwa misingi ya utawala bora. Vile vile, naomba kuwapongeza sana Mawaziri, Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu, Naibu Makatibu Wakuu, Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Watendaji wote wa Serikali kwa kuendelea kutekeleza majukumu yao vyema kwa lengo la kuharakisha maendeleo ya nchi yetu.
5. Mheshimiwa Spika, aidha, napenda kuwashukuru sana Waandishi wa vyombo vyote vya Habari. Sisi sote hapa ni mashuhuda jinsi Waandishi wa Habari katika Baraza walivyoweza kufuatilia kwa makini mwenendo mzima wa matukio mbali mbali ndani na nje ya Baraza, ikiwemo utoaji wa taarifa za hoja, michango na mijadala iliyojitokeza Barazani na kuwafikia wananchi wetu. Nachukua nafasi hii kuvipongeza na kuvishukuru sana vyombo hivyo kwa kutekeleza vyema jukumu lao kuwapasha habari za Baraza wananchi ipasavyo. Natoa pongezi za pekee kwa wakalimani wa lugha ya alama kwa kazi kubwa waliyoifanya katika kutafsiri mijadala kwa ishara ili kuwawezesha wananchi wetu wenye ulemavu wa kutokusikia kupata taarifa juu ya mijadala yetu ndani ya Baraza.
6. Mheshimiwa Spika, kwa masikitiko makubwa naomba nizungumzie juu ya tukio la msiba uliotupata nchini kwetu hivi karibuni. Taifa letu lilipokea kwa mshituko na huzuni kubwa taarifa ya vifo vya wapiganaji wetu saba wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), ambao wameuawa nchini Sudan baada ya kuvamiwa na Waasi wa Darfur katika harakati za kusaidia kuweka amani nchini humo. Vifo vya wapiganaji hao ni msiba mkubwa kwetu sote. Ni dhahiri kuwa Wapiganaji wetu hao wameonesha ujasiri na moyo wa uzalendo mkubwa kwa wananchi wa Tanzania na kwa Bara la Afrika. Ni ukweli usiopingika kuwa Wapiganaji hao wamekufa kishujaa na nimefarajika sana kuona kwamba mazishi yao yamepewa heshima zote za Kitaifa. Katika tukio hilo la kuhuzunisha walikuwamo wanajeshi wawili kutoka Brigedi ya Nyuki ya Zanzibar ambao ni Sajenti – Shaibu Shehe Othman na Koplo Mohammed Juma Ali. Naomba kuchukua nafasi hii kwa niaba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, kutoa salamu za rambirambi kwa familia, ndugu, jamaa, marafiki na wananchi wote na nawaomba wawe na subira katika kipindi hiki kigumu cha huzuni na maombolezo, Mwenyezi Mungu azilaze roho za Marehemu pahala pema peponi, Amin.
MASUALA MUHIMU YALIYOJIRI NCHINI
7. Mheshimiwa Spika, wakati Serikali ipo katika hatua ya kutekeleza malengo ya maendeleo, hususan kutekeleza mikakati na sera ya matumizi na umiliki wa ardhi, juhudi kubwa zinaendelea kuchukuliwa ili kuhakikisha ardhi tuliyonayo inatumiwa ipasavyo na inatoa tija kubwa zaidi. Lengo la mikakati na sera za ardhi ni kutatua kwa uadilifu migogoro ya ardhi inayojitokeza mara kwa mara hapa nchini.
Miongoni mwa hatua zinazoendelea kuchukuliwa kuhusiana na suala la migogoro ya ardhi ni zoezi linaloendelea la usajili wa ardhi na kuhakikisha kwamba ardhi yote ya Zanzibar inasajiliwa na taarifa zake zinawekwa katika daftari maalumu. Madhumuni ya zoezi hilo ni kuiwezesha Serikali kupata taarifa sahihi za watu wote ambao wana haki ya matumizi ya ardhi. Pia, hatua hiyo itaiwezesha Serikali kupanga matumizi mazuri ya ardhi pamoja na kuweka kumbukumbu sahihi za wamiliki wa ardhi hizo nchini.
8. Mheshimiwa Spika, katika hatua nyengine ya kupunguza mrundikano wa kesi za ardhi, Serikali imepanga kuanzisha Mahakama za Ardhi katika kila Mkoa pamoja na kuongeza idadi ya Mahakimu wa Mahakama ya Ardhi Unguja na Pemba ili kurahisisha na kuharakisha mwenendo wa kesi za migogoro ya ardhi ambazo zimekuwa zikiongezeka siku hadi siku.
9. Mheshimiwa Spika, azma ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni kuwa na miji ya kisasa yenye huduma za aina zote. Katika suala la upangaji wa miji na matumizi ya ardhi, Serikali inaendelea na zoezi la utayarishaji wa “Master Plan” ya Mji wa Zanzibar na Mpango wa Mji wa Chake Chake. Lengo ni kuipanga upya miji hiyo ambapo suala la makaazi, biashara, viwanda na maeneo ya michezo na mapumziko yamezingatiwa kwa kina kwani maeneo haya yote ni muhimu kwa uchumi na afya za wananchi wetu.
10. Mheshimiwa Spika, naomba kuchukua nafasi hii kutoa wito kwa wananchi na Viongozi kufuatataratibu za usajili wa ardhi ili kuhakikisha tunakuwa na matumizi mazuri ya ardhi pamoja na kupata ufumbuzi wa kudumu wa migogoro ya ardhi inayojitokeza mara kwa mara. Lakini pia, ningependa kuwasihi Watendaji wa Wizara ya Ardhi kutekeleza maagizo ya Viongozi yenye nia ya kuleta suluhu katika migogoro ya ardhi inayojitokeza kwani wakati mwingine wanachukua muda mrefu kutekeleza maagizo hayo.
11. Mheshimiwa Spika, kwa muda mrefu sasa Zanzibar imekuwa ikitumia chanzo kimoja cha umeme. Hali hii imepelekea kupata malalamiko kutoka kwa wananchi pale inapotokea hitilafu za kukosekana kwa umeme au kupanda kwa gharama za huduma hiyo muhimu. Kwa msingi huo, Serikali imetoa kipaumbele katika kutafuta chanzo cha nishati mbadala ya uhakika badala ya kutegemea chanzo kimoja cha umeme. Hivyo, kwa kupitia Wizara inayohusika, Serikali inaendelea na utafiti yakinifu wa kupata nishati mbadala. Tunatarajia baada ya utafiti huo, Zanzibar itaweza kupata chanzo chengine cha nishati mbadala na hatimae kuwekeza katika uzalishaji wa nishati hiyo. Mpaka hivi sasa wamejitokeza wawekezaji kadha walioonyesha nia ya kuwekeza katika miradi ya umeme mbadala. Wapo wa kutumia solar, wapo wa kutumia upepo, wapo wa kutumia takataka na wapo wa kutumia mawimbi ya bahari. Hivi sasa Serikali inachunguza ni mradi wa aina gani utakuwa wa manufaa zaidi kwa nchi, kiuchumi na kimazingira.
12. Mheshimiwa Spika, hivi sasa tunakabiliwa na changamoto nyingi za uharibifu wa mazingira, na zaidi tatizo hilo limejitokeza kutokana na kuwepo kwa athari za mabadiliko ya tabianchi, maendeleo ya sekta ya utalii, ujenzi wa miundombinu na ukosefu wa miundombinu ya uondoaji wa taka pamoja na uingizaji wa bidhaa chakavu za elektroniki na mifuko ya plastiki. Katika juhudi za kukabiliana na hali hiyo, Serikali imechukua hatua za kuanzisha Sera mpya ya Mazingira ya mwaka 2013, Mkakati wa Zanzibar wa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, kuweka Kanuni za Usimamizi Endelevu wa Maliasili zisizorejesheka pamoja na kufanya mapitio ya Sheria ya Mazingira Namba 2 ya Mwaka 1992.
13. Mheshimiwa Spika, sambamba na hatua hizo, Serikali imekamilisha muongozo ambao utaitaka kila Taasisi kuwa na wajibu wa kutekeleza mipango yake kwa kuzingatia masuala ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi. Kwa kuzingatia umuhimu wa suala hilo, Serikali inawashauri wananchi kupanda miti kwa wingi katika maeneo mbali mbali hasa miti ya matunda na mazao ya biashara.Naomba kuwatanabahisha wananchi kwamba Serikali haitamvumilia mwananchi yeyote ataekwenda kinyume na taratibu za uhifadhi wa mazingira nchini. Kwa sababu kama hatukuwa waangalifu katika kuyalinda mazingira yetu, nchi yetu itaweza kupata majanga makubwa.
14. Mheshimiwa Spika, katika muktadha wa kuhifadhi mazingira na kumlinda mtumiaji, naomba kuliarifu Baraza lako Tukufu kwamba Serikali kupitia Taasisi zinazohusika imeweza kuangamiza tani 700 za unga wa ngano mbovu ulioingizwa nchini kinyume na Sheria. Naomba kuchukua nafasi hii kuishukuru kwa dhati Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais, kwa mashirikiano makubwa iliyotupa kufanikisha uangamizaji wa unga huo. Katika kuhakikisha kuwa tunakuwa na mfumo madhubuti wa kusimamia ubora wa bidhaa nchini, Serikali inaifanyia marekebisho Sheria ya Chakula, Dawa na Vipodozi ya Mwaka 2006 kwa lengo la kudhibiti uingizaji na utumiaji wa bidhaa hizo.
15. Mheshimiwa Spika, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inawaagiza wafanyabiashara wote kuwa makini wakati wa kuingiza nchini bidhaa zao zisiwe zilizopitwa au zinazokaribia kupitwa na muda wake wa matumizi pamoja na bidhaa mbovu. Serikali itawachukulia hatua kali wafanyabiashara wote watakaokwenda kinyume na agizo hili, kwani ni wajibu wa Serikali kuwalinda wananchi wasile vyakula vibovu vitakavyoweza kuwaletea madhara.
16. Mheshimiwa Spika, katika kufanikisha utekelezaji mzuri wa masuala ya viwango vya bidhaa, Serikali inaijengea uwezo Taasisi ya Viwango ya Zanzibar (Zanzibar Beurau of Standards – ZBS) ili iweze kuweka viwango vya bidhaa zinazoingizwa na kutengenezwa nchini. Azma hiyo inatokana na umuhimu wa kuepusha nchi yetu kugeuzwa kuwa jaa la kutupia bidhaa mbovu na zisizo na viwango na kulinda afya za wananchi wetu. Wizara ya Biashara inaagizwa kuona umuhimu wa kuzikagua bidhaa kabla ya kuingizwa nchini kwani kumekuwepo na malalamiko kuwa Zanzibar ni njia ya kupitisha bidhaa mbovu. Taasisi ya Viwango ya Zanzibar (ZBC) inashauriwa kufungua ofisi nje ya nchi ili kuzikagua bidhaa zinazotaka kuingizwa nchini kabla ya kuingizwa nchini bidhaa hizo.
17. Mheshimiwa Spika, kuhusu suala la kuendeleza zoezi la Mabadiliko ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hivi sasa jamii imeshaunda Mabaraza ya Katiba ya Wilaya na hatua za kukusanya maoni kupitia Mabaraza hayo inaendelea. Napenda kuwapongeza Wajumbe wote wanaowakilisha Mabaraza hayo kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kuwasilisha mawazo yao kwa amani na utulivu. Hilo ni jambo la msingi sana katika kuhakikisha kuwa Wazanzibari wanawasilisha maoni yao ya Kikatiba kwa kufuata taratibu zilizowekwa kwa misingi ya demokrasia. Ni matarajio yetu kwamba ushiriki wa wananchi kupitia Mabaraza hayo utakuwa na mafanikio na hatimae tutaweza kupata Katiba ambayo itakuwa na maslahi ya kisiasa, kiuchumi na kijamii kwa nchi yetu na wananchi wake. Hivyo, wananchi wanaombwa kutoa maoni yao kwa uhuru na uwazi bila ya woga.
18. Mheshimiwa Spika, katika hatua nyengine zinazochukuliwa kuimarisha Demokrasia na Utawala Bora nchini, Serikali inaendelea kuratibu vyema zoezi la uhakiki wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kupitia Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC). Lengo la zoezi hilo, ni kuwaandikisha wale wote wanaostahiki na kuwatoa wale ambao hawastahiki. Hili ni zoezi muhimu kwa maslahi ya kisiasa kwa wananchi wetu. Napenda kutoa wito kwa wananchi wote kushiriki kwa kikamilifu katika zoezi hilo. Katika kufanikisha zoezi hili kwa amani na utulivu, nawasihi wananchi wote kufuata sheria na taratibu za uandikishaji zilizowekwa ikiwemo kuwa na ithibati zote zinazohitajika ili kuweza kuandikishwa bila ya bughudha. Wananchi wanaonywa kutowafanyia hila au vurugu wananchi wenzao ili kuwazuia wasijiandikishe. Hilo ni kosa la jinai na mtu atakayebainika kufanya hivyo atachukuliwa hatua za kisheria.
19. Mheshimiwa Spika, ni jambo la faraja kuona kuwa sekta ya uvuvi imezidi kuimarika kutokana na kuongezeka kwa shughuli za uvuvi wa baharini na pia wananchi wengi wameanza kufuga samaki na mazao mengine ya baharini. Mafanikio makubwa yameweza kupatikana hasa katika kisiwa cha Pemba.
Uchambuzi wa takwimu umeonesha kwamba katika kipindi cha mwaka 2012/2013 sekta ya uvuvi imepata mafanikio makubwa matatu yafuatayo:-
20. Mheshimiwa Spika, kwanza, idadi ya samaki wanaovuliwa imeongezeka kutoka tani milioni 28.8 hadi 29.4, sawa na ongezeko la tani 651 ambayo ni asilimia 2.3. Pili, wingi wa samaki wanaovunwa umefikia jumla ya tani 9.8 kwa mwaka ambapo Pemba imevuna tani 7.7 na Unguja tani 2.1 kwa mwaka 2012/2013. Tatu, mafanikio makubwa katika zao la mwani kutoka tani 13 elfu mwaka 2011 mpaka tani 15 elfu mwaka 2013 ikiwa ni ongezeko la asilimia 16.
21. Mheshimiwa Spika, kwa jumla shughuli zote za kilimo cha mwani, uvuvi wa baharini na samaki wa kufuga, zimeweza kusaidia kuongeza kipato cha wananchi sambamba na malengo ya Mpango wa Pili wa Kupunguza Umaskini (MKUZA II) pamoja na Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi 2010/2015. Katika kuendelea kuyalinda mazalio ya samaki, tunawasihi wavuvi kuacha uvuvi haramu, kwani uvuvi haramu unaweza kusabibisha uharibifu wa mazalia ya samaki na hivyo kupunguza idadi ya samaki baharini. Wavuvi wakumbuke kuwa wakivua leo, waweke akiba ili waweze kuvua na kesho.
22. Mheshimiwa Spika, hali ya sekta ya mifugo nayo imeanza kutoa matumaini yenye kutia moyo. Miongoni mwa mafanikio hayo ni kuimarika kwa utoaji wa huduma za uzalishaji na utibabu wa mifugo. Pia kujengwa kwa mitambo mipya ya gesi asilia (biogas) kumi na moja (11), Unguja minane na Pemba mitatu. Kukamilika kwa ujenzi wa mitambo hiyo kumepelekea kuwa na mitambo 24 kwa Unguja na Pemba iliyokwisha kujengwa.
23. Mheshimiwa Spika, katika juhudi za kuwawezesha wananchi kiuchumi Serikali imetoa jumla ya mikopo 193 yenye thamani ya Shilingi Milioni 156 kwa kupitia Mfuko wa Kujitegemea. Aidha, Serikali imetoa Shilingi Milioni 303 kwa Vyama vya Ushirika na vikundi vya wajasiriamali 199 kwa kupitia Mfuko wa Zaka.
24. Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha uratibu wa utoaji wa mikopo midogo midogo, Serikali imeanzisha mtandao wa Taasisi zinazotoa huduma za fedha kwa wajasiriamali wadogo. Mtandao huo unajumuisha taasisi mbali mbali zikiwemo WEDTF, YOSEFO, Benki ya CRDB, Changamoto, Melinne SACCOS na Jumuiya ya Wafanyabiashara, Wenye Viwanda na Wakulima Zanzibar. Lengo la mtandao huo ni kubadilishana taarifa za wakopaji ili kuweza kutathmini idadi ya watu wanaofikiwa kwa huduma za mikopo na pia kuimarisha mashirikiano katika huduma zao. Hatua hii inasaidia kubainisha thamani na aina ya mikopo ambayo hutolewa na taasisi mbali mbali kwa wajasiriamali na namna mikopo hiyo inavyowasaidia wajasiriamali hao kuendesha maisha yao na kujikomboa kutoka kwenye umasikini.
25. Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha usafiri wa baharini, mnamo tarehe 10 Julai, 2013, Serikali imetiliana saini mkataba wa ujenzi wa meli ya abiria na mizigo na kampuni ya Daewoo ya Korea ya Kusini. Meli hiyo ambayo itakuwa na uwezo wa kuchukua abiria 1200 katika daraja tatu tofauti na uwezo wa kubeba mizigo yenye uzito wa tani 200, itakamilika ujenzi wake baada ya miezi 23 kuanzia Julai mwaka huu.
26. Mheshimiwa Spika, hatua hii imekwenda sambamba na ukarabati wa jengo jipya la abiria katika eneo la bandarini kwa mashirikiano na mwekezaji wa kizalendo S.S. Bakhresa wa Kampuni ya Azam Marine. Uzinduzi wa mradi huu umefanyika rasmi tarehe 8 Julai, 2013. Serikali inatoa shukurani za dhati kwa Uongozi wa Kampuni ya Azam Marine kwa mchango wao mkubwa katika kusaidia maendeleo ya shughuli za usafiri kwa kuwaondolea bughdha wasafiri.
27. Mheshimiwa Spika, tarehe 12 Januari, 2014, nchi yetu itaadhimisha miaka 50 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar. Maadhimisho hayo yanatarajiwa kuwa ya aina yake na yatazinduliwa rasmi na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mheshimiwa Dkt. Ali Mohammed Shein tarehe 15 Agosti, 2013. Kwa lengo la kufanikisha sherehe za maadhimisho hayo, Serikali inatoa wito maalumu kwa wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi kwa pamoja na sekta binafsi kushirikiana na Serikali ili kuzifanya sherehe hizo kuwa za kihistoria pamoja na kuzipa hadhi ya juu na ya kipekee.
Sherehe hizo zitajumuisha mafanikio ya utekelezaji wa sekta zote za uzalishaji na utoaji wa huduma kwa kuonesha maendeleo yao ya miaka 50 ya Mapinduzi. Madhumuni ya kufanya sherehe hizo yanatokana na haja ya wananchi wa Zanzibar kuelewa na kutathmini wapi tulipotoka, tulipo sasa na wapi tunapokusudia kwenda kwa mtazamo wa kuinua hali za maisha ya wananchi walio wengi na kuharakisha maendeleo ya nchi kwa jumla.
MAMBO MUHIMU YALIOJITOKEZA BARAZANI
28. Mheshimiwa Spika, katika Mkutano huu wa 12 wa Baraza lako Tukufu, Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza walijadili na kupitisha Bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha 2013/2014. Aidha, Waheshimiwa Mawaziri wamewasilisha Miswada miwili ya sheria ambayo ina umuhimu mkubwa kwa ustawi na maendeleo ya nchi yetu.
29. Mheshimiwa Spika, Mswada wa kwanza uliojadiliwa ni Mswada wa Sheria ya Kutoza Kodi na Kubadilisha baadhi ya Sheria za Fedha na Kodi Kuhusiana na Ukusanyaji na Udhibiti wa Mapato ya Serikali na mambo mengine yanayohusiana na hayo. Madhumuni ya mswada huo ni kudhibiti mianya ya uvujaji wa mapato ya Serikali na kuweka utaratibu mzuri wa udhibiti ukusanyaji wa mapato.
30. Mheshimiwa Spika, Mswada wa Pili ni Mswada wa Sheria ya Matumizi ya Fedha za Umma (Appropriation Bill).
31. Mheshimiwa Spika, katika kikao hiki cha kumi na mbili Waheshimiwa Mawaziri wa Wizara zote waliwasilisha hotuba za Mapato na Matumizi za Wizara zao kwa mwaka fedha 2013/2014, na Waheshimiwa Wajumbe walipata nafasi ya kuzijadili, kuzichangia kwa uangalifu, umakini na uadilifu mkubwa na hatimae kuzipitisha. Waheshimiwa Wajumbe walipata nafasi ya kuhoji kwa yale mambo ambayo walihisi hayakuwa bayana na yalihitaji ufafanuzi na Waheshimiwa Mawaziri kwa mujibu wa Kanuni za Baraza walitoa ufafanuzi unaostahiki na hatimae Wajumbe walizipitisha bajeti za mwaka huu, ingawa baadhi ya Bajeti hizo zilipita kwa mbinde. Hii imeonyesha umakini mkubwa waliokuwa nao Wajumbe wa Baraza. Naomba kusisitiza kwamba baada ya Baraza kufanya kazi kubwa ya kuzichambua, kuzihakiki na kutoa mapendekezo katika Bajeti za Wizara mbali mbali, Uongozi wa Wizara zote kuwa makini katika matumizi na usimamizi kwa mujibu wa malengo na taratibu za matumizi ya fedha. Waheshimiwa Mawaziri na Makatibu Wakuu wanaombwa kusimamia kwa makini matumizi ya fedha za Wizara zao zilizoidhinishwa na Baraza hili.
32. Mheshimiwa Spika, baadhi ya Wajumbe katika uchangiaji wa bajeti ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi walihoji juu ya uagizaji wa kuku kutoka nje ya nchi. Mjadala mrefu ulitokana na wasiwasi wa baadhi ya Wajumbe hao kuwa uingizaji wa bidhaa hiyo utadhoofisha soko kwa wafugaji wa ndani na hatimae kuwakosesha kipato wafugaji hao. Ukweli dhana hiyo sio kweli kwani Serikali inazingatia sana hali za wananchi wake si wafugaji au wafanyabiashara pekee. Kabla ya Serikali kufanya uamuzi huu, ililitafakari kwa kina suala hili na hatimae kufanya uamuzi huo baada ya kuona kuwa haukuwa na madhara kwa wafugaji wetu.
Hata hivyo, naomba kueleza kuwa Serikali kwa muda mrefu hapo nyuma iliamua kuchukua hatua za kuimarisha ushindani wa kibiashara. Lakini tatizo kubwa linalojitokeza ni kwamba mahitaji ya soko la kuku Zanzibar ni kubwa. Kwa hivyo, kwa kipindi hiki si vyema kuchukua hatua yoyote ya kubana uingizaji wa kuku kutoka nje hadi pale soko la ndani litakapoweza kujitosheleza. Kwani tukichukua hatua hiyo ghafla tunaweza kuhatarisha mahitaji halisi ya biashara katika sekta nyengine hasa sekta ya utalii nchini.
33. Mheshimiwa Spika, nawaomba Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza lako Tukufu wasilichukulie suala hili kuwa sawa na wenzetu wa Tanzania Bara. Tukijilinganisha na wao kwa hali zetu tutakosea kwani sababu zao ni tofauti na zetu kwa sababu:-
a) Wenzetu Tanzania Bara wana wafugaji wengi wanaozalisha kwa viwango vinavyotakiwa.
b) Waliamua kuzuia uletaji wa kuku pamoja na mambo mengine kwa sababu ya maradhi. Mambo ambayo uletaji wa kuku wetu huwa yanazingatiwa kwa kiwango kikubwa.
c) Wananchi wetu wengi hawawezi kumudu bei za kuku hapa nchini. Hii ni kutokana na gharama kubwa mno za uzalishaji.
Kwa maana hiyo Serikali haikupuuza ushauri wa baadhi ya Wajumbe wa Baraza bali itaendelea kufanya utafiti wa hali halisi ya biashara hiyo ili tufaidike sote, wafugaji na walaji pia.
34. Mheshimiwa Spika, kwa kuelewa wasiwasi wa wafugaji wa kuku wa ndani, Serikali itaendelea kuangalia mwenendo mzima wa uzalishaji na uagizaji wa kuku ili kuhakikisha kuwa wafugaji wa ndani hawaathiriwi na suala hilo, kama Baraza lilivyoelekeza. Serikali itawasaidia wafugaji wetu ili wazalishe zaidi ili tuweze kupunguza uagizaji kidogo kidogo hadi pale tutakapojitosheleza kwa ukamilifu.
35. Mheshimiwa Spika, baada ya kukamilisha kazi za awali za mradi wa E-Government ikiwemo kutandika Mkonga wa “Fibre Optic” Serikali imeendelea na kazi za kuimarisha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano. Kutokana na umuhimu wa suala hilo, hata Wajumbe wa Baraza walichangia sana juu ya haja ya kukamilisha mradi wa E-Government. Hivyo, napenda kuchukua nafasi hii kuwahakikishia Wajumbe pamoja na wananchi kuwa Serikali imekusudia kwa dhati kufanikisha mradi huu haraka iwezekanavyo.
36. Mheshimiwa Spika, madhumuni hasa ya mradi huu yanalenga katika kuendesha na kusimamia matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano katika sekta ya Utumishi wa Umma ili kuhakikisha kuwa usimamizi wa kumbukumbu za eletroniki pamoja na teknolojia ya habari na mawasiliano unatumika katika kuimarisha huduma za Utawala Bora. Mradi huu utaanzisha mfumo wa pamoja utakaotumiwa na Taasisi zote za umma pamoja na kuweka mazingira mazuri ya utekelezaji wa jumla kwa mujibu wa dhana ya kuimarisha utoaji wa huduma za Serikali zilizounganishwa ki-eletroniki.
37. Mheshimiwa Spika, Serikali ya mtandao kwa muda huu tulionao ni kitu cha lazima. Kwa msingi huo, naomba nitoe tahadhari kuwa mafanikio ya mradi huu yatafikiwa sambamba na jamii kuweza kutumia vyema teknolojia ya kompyuta. Hatua hii itapelekea haja ya Viongozi, watumishi wa Serikali pamoja na wananchi kuchukua juhudi za makusudi kujifunza kutumia kompyuta. Tukizingatia kwamba teknolojia hii inakuwa kwa haraka mno na tusisite kujifunza hivi sasa kwani tukijifunza baadae tutakuwa tumechelewa mno na hivyo tutapitwa na wakati.
38. Mheshimiwa Spika, napenda kulihakikishia Baraza lako Tukufu kuwa, Serikali inaendelea na juhudi za kuimarisha sekta za utoaji huduma, ikiwemo sekta za maji safi na salama, afya, elimu na miundombinu. Kwa upande wa uzalishaji, Serikali itaendelea kutoa kipaumbele kwa kuimarisha sekta za kilimo, mifugo na uvuvi, viwanda vidogo vidogo, utalii na biashara nchini. Lengo kuu la juhudi hizi zinazochukuliwa na Serikali ni kukuza uchumi na kupunguza umasikini katika nchi yetu.
39. Mheshimiwa Spika, napenda kuchukua fursa hii kusisitiza mambo yafuatayo: Kwanza, Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wajue kuwa tumemaliza Mkutano wa Baraza hili la kumi na mbili na hivyo ni vyema wakarudi katika Majimbo yao ili kushirikiana na wananchi wao katika harakati za kuleta maendeleo kwa nia ya kuimarisha maelewano baina ya wananchi na Wawakilishi wao. Pili, katika suala la ardhi tunawaomba wananchi na Viongozi kufuata taratibu zilizowekwa katika suala la uhifadhi wa mazingira, umiliki na matumizi mazuri ya ardhi, pamoja na Viongozi wa ngazi zote kuacha kabisa tabia potofu zinazochangia ongezeko la migogoro ya ardhi nchini. Tatu, kwa upande wa Watendaji Wakuu wa Serikali tunasisitiza uwajibikaji kwa mujibu wa Sheria ya Utumishi wa Umma na kuhakikisha utekelezaji wa malengo ya bajeti unaendeshwa kwa misingi ya uadilifu kama ilivyosisitizwa katika mkutano huu wa kumi na mbili kwa azma ya kufikia matarajio ya Wizara zetu. Agizo hili liende sambamba na utekelezaji wa Sheria ya Matumizi ya Fedha za Umma na tuepukane kabisa na mtindo wa utekelezaji wa kufanya kazi kwa kutumia uzoefu “business as usual.” Serikali itaendelea kuliunga mkono Baraza la Wawakilishi katika juhudi zake za kuwafichua Watendaji wabadhirifu na wabinafsi na kuwachukulia hatua wanazostahiki. Lakini kuifanikisha kazi hii lazima sote tuwe na sauti moja, ya kuwafichua na siyo wengine kuwa mawakili wa wafichuliwa.
40. Mheshimiwa Spika, kabla ya kumaliza hotuba yangu, ningependa nieleze machache kuhusu suala zima la amani na utulivu katika nchi yetu. Nalisema hili kwa sababu kila mmoja wetu naamini anafahamu umuhimu wa amani kwa nchi yoyote ile sio hapa nyumbani tu. Kwa maana hiyo ndio sababu Mataifa mbali mbali huwa makali wakati nchi zao zinapohatarishiwa utulivu na amani yao.
Hivi karibuni amejitokeza kiongozi wa kidini kutoka nje ya visiwa hivi na kuanza kupita misikitini kwa lengo la kutoa mihadhara ya uchochezi dhidi ya Serikali na Viongozi wake. Mihadhara ambayo ilikuwa ya kuwapotosha wananchi.
Kitendo hicho kwa kweli ni cha kusikitisha na hakikuwa cha kiungwana na kinakwenda kinyume na maadili ya dini yenyewe ya Kiislam, licha ya kuhatarisha amani na utulivu uliopo. Lazima ifahamike wazi kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika suala la kudumisha amani haina stahamala wala muhali. Haitosita kuchukua hatua kali kwa mujibu wa sheria za nchi kwa kikundi au mtu yeyote atakayeonekana kujiingiza kwa njia moja au nyengine katika kuchezea amani yetu. Serikali itailinda amani ya nchi na wananchi wake kwa gharama yoyote ile.
41. Mheshimiwa Spika, Zanzibar haina mgongano wowote wa dini wala waumini wa dini zozote, endapo Viongozi na waumini wake watafanya ibada zao kwa kufuata sheria na taratibu za nchi zilizowekwa. Kwa mnasaba huo, Serikali haitakubali kuona kiongozi wa dini kufanya mahubiri yanayoelekeza sura za uchochezi zinazopelekea kuondoa utulivu badala ya mshikamano wa raia wote.
Hivyo, Serikali inalaani vitendo vya mahubiri ya aina hiyo hususan kitendo cha kiongozi huyo kufanya mihadhara ndani ya misikiti kadhaa hapa nchini kwa lengo la uchochezi. Katu hakitavumiliwa, na Serikali haitahofu kutupiwa lawama kwa hatua itakazochukua dhidi ya watu wa aina hiyo. Hii ni kwa sababu sote tunafahamu kuwa amani na utulivu tulionao umepatikana kwa gharama kubwa.
Hapa ningependa kuwaasa wananchi wasiwaunge mkono viongozi wa aina hiyo, kwani hawaitakii mema nchi yetu na wanataka kuturejesha nyuma katika hali ya uadui, uhasama miongoni mwa jamii yetu.
42. Mheshimiwa Spika, kitendo cha muhubiri huyo kuleta uchochezi nchini mwetu kupitia Misikitini ni kutusababishia kutokea kwa vurugu nchini ambapo hatimae ni sisi wenyewe ndio tutakaoumizana. Muhubiri huyo amekaanga mbuyu na kuwaachia wenye meno watafune. Zikitokea vurugu na ukosefu wa amani nchini, tutakaoumizana ni sisi, yeye atakuwa hayupo wala mkewe na watoto wake. Nawasihi sana wananchi wasiyafuate mahubiri hayo.
43. Mheshimiwa Spika, nimepata habari kuwa kuna kikundi cha watu kimeanzisha utaratibu wa kupita katika maeneo mbali mbali ya Unguja na Pemba na kuwahoji wananchi kuwa ni wafuasi wa Chama gani – CCM au CUF. Wamekuwa kama wanajaribu kufanya sensa ya kujua katika maeneo hayo kuna wanachama wangapi wa CCM na wangapi wa CUF.
44. Mheshimiwa Spika, nachukua nafasi hii kuwaeleza wananchi wote kwamba Serikali haina habari na zoezi hilo na wala haijatoa agizo la kufanyika kwa sensa hiyo. Hivyo, ninawaomba wananchi wasikubali kushiriki katika zoezi hilo ambalo halina baraka za Serikali. Aidha, ningependa kukionya kikundi hicho kuliacha zoezi hili mara moja kwa sababu Serikali haiendeshi sensa ya aina hiyo.
45. Mheshimiwa Spika, katika suala hili ningependa kuwaomba Masheha wote, Unguja na Pemba kulifuatilia suala hilo kwa karibu na kuhakikisha kuwa zoezi hilo halifanyiki katika maeneo yao.
46. Mheshimiwa Spika, katika mikutano kadhaa ya Baraza, na hasa katika Mkutano huu wa Bajeti jambo moja limekuwa likijitokeza sana, nalo ni matumizi ya taarifa na nyaraka za Serikali ambazo baadhi yao ni za siri.
Kuhusiana na suala hili, kwanza nitangulie kueleza wazi kuwa Serikali inaelewa na kuthamini kuwa msingi mmoja wa Utawala Bora ni uwazi. Lakini naamini kuwa Waheshimiwa Wajumbe wote watakubaliana nami kuwa uwazi hauna maana kuwa hakuna utaratibu tena wa kupata taarifa na nyaraka za siri za Serikali, na wala haina maana kuwa ni ruhusa kwa kila mwenye taarifa ya Serikali au hata taarifa za mtu binafsi azisambaze kwa kadri apendavyo yeye, kwani kwa upande wa pili, moja ya msingi mkuu wa haki za binaadamu ni haki ya faragha. Tumeshuhudia mara kadhaa, Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza hili wakilalamika na kuwa wakati kwa taarifa zao binafsi kama zile za maslahi yao kuwekwa hadharani bila ya ridhaa zao.
Hivyo, naomba kutanabahisha kuwa, kwanza kwa mujibu wa Sheria ya Kinga, Haki na Fursa ya Baraza la Wawakilishi Namba 4 ya mwaka 2007, hasa kifungu cha 9 inaelezwa wazi kuwa ni haki ya Wajumbe kupata taarifa kutoka Serikalini ili mradi tu taarifa hizo hazizuiliki kutolewa kwa mujibu wa masharti ya kifungu cha 19 cha Sheria hiyo. Hata hivyo, kifungu chenyewe cha 9 cha Sheria hiyo ya Kinga, Haki na Fursa za Baraza kinaeleza wazi kuwa Wajumbe wana haki ya kupata taarifa kwa kufuata Sheria na Taratibu zilizowekwa na Sheria yenyewe, Sheria nyengine za nchi na taratibu za Serikali za kupata taarifa. Miongoni mwa taratibu zilizowekwa na Sheria ya Kinga ni kwa taarifa kutolewa na Ofisa muhusika kwa Baraza au kwa Kamati. Aidha, kama Mjumbe anataka taarifa kutoka katika Taasisi ya Umma na kama taarifa hizo si za matumizi ya jumla ya umma, utaratibu uliopo ni kwa kupitia Ofisi ya Baraza. Mbali ya Sheria hiyo ya Kinga kuweka taratibu nilizoeleza, naomba niwatanabahishe watumishi na watendaji wa Taasisi za Umma kuwa Sheria ya Siri za Serikali, Namba 5 ya mwaka 1983, chini ya kifungu cha 5 cha Sheria hiyo imeweka bayana kuwa ni kosa la jinai kwa mtu yeyote kutoa taarifa za Serikali ambazo ama amekabidhiwa au amezipata kwa sababu ya kazi au wadhifa wake kwa mtu asiyehusika. Adhabu ya kosa hilo ni kifungo kisichozidi miaka kumi na mbili bila ya faini.
47. Mheshimiwa Spika, sio nia wala madhumuni ya Serikali kuficha au kuzuia taarifa za uovu wowote unaofanywa na mtendaji yeyote wa Serikali bali inachosisitiza kufuatwa kwa taratibu. Serikali inaamini kuwa Sheria na taratibu ziliopo kwa Waheshimiwa Wajumbe kupata taarifa wanazohitaji, zinatoa fursa ya kutosha kufanya hivyo kihalali bila ya kuvunja sheria wala taratibu ziliopo. Bila ya kufuata taratibu yatajitokeza mambo kadhaa kama tulivyoanza kuyaona. Miongoni mwa mambo hayo ni pamoja na taarifa kutolewa nusu nusu au za upande mmoja ili mradi mjumbe ajenge hoja anayopenda yeye na hivyo kuwapotosha Waheshimiwa Wajumbe na wananchi kwa jumla. Aidha, baadhi ya taarifa zinapotolewa upande mmoja zinahatarisha maisha na usalama wa baadhi ya watendaji kwa kuonyesha kama kwamba wao ndio waliotoa uamuzi wakati wanafanya hivyo katika kutekeleza majukumu ya kazi zao.
48. Mheshimiwa Spika,katika Mkutano huu tunaouahirisha leo, jumla ya maswali 104 ya msingi na masuala 246 ya nyongeza yaliulizwa na Waheshimiwa Wawakilishi na kujibiwa na Waheshimiwa Mawaziri husika. Nawapongeza sana Waheshimiwa Wajumbe kwa kuja na masuala mazuri yenye lengo la kujenga zaidi na kuimarisha uwajibikaji wa watendaji wa Serikali. Aidha, nawapongeza Waheshimiwa Mawaziri kwa majibu yao ya kina ambayo hatimaye yaliwaridhisha Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza lako Tukufu.
49. Mheshimiwa Spika, ikiwa tunaendelea kutekeleza Ibada ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, naomba tuendelee kuimarisha amani na utulivu iliyopo nchini kwetu ili tuweze kunufaika na neema alizotujalia Mwenyezi Mungu pamoja na kupata fadhila za Mwezi Mtukufu wa Ramadhani. Kwa kuwa hapatakuwa na kikao chengine cha Baraza kwa kipindi hiki cha karibu naomba pia kuchukua nafasi hii kutoa mkono wa Idd-el–Fitri kwenu Wajumbe wa Baraza hili Tukufu na wananchi kwa jumla. Nakutakieni kila la kheri na baraka katika Sikukuu hii adhim ya Idd El Fitri.
50. Mheshimiwa Spika, kwa mara nyengine tena naomba kuchukua nafasi hii kukushukuru wewe binafsi, Wajumbe wa Baraza lako, Waandishi wa Habari na Wananchi wote kwa mashirikiano yao makubwa katika kuliendesha Baraza letu kwa mafanikio. Ni matarajio yetu kwamba wananchi wataendelea kuwa karibu nasi katika kuimarisha demokrasia na utawala bora pamoja na maendeleo ya Taifa letu. Nawatakia safari ya salama Waheshimiwa Wajumbe wote ya kurejea majimboni mwao.
51. Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo,sasa naombakutoa hoja ya kuliakhirisha Baraza lako Tukufu hadi siku ya Jumatano, tarehe 9 Oktoba, 2013 saa 3.00 barabara za asubuhi panapo majaaliwa.
52. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.