Na Khamisuu Abdallah
Serekali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania imetiliana saini na kampuni ya Inventions Technology ya Dar es Salam, kuweka huduma ya ideo conference katika ofisi za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
Utiaji saini huo ulifanyika katika ofisi za Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano Kisauni wilaya ya magharibi Unguja, ambapo kwa uapnde wa Serkali ya Jamhuri iliwakilishwa na Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, John Mndogo na kampuni hiyo iliwakilishwa na Mkurugenzi Mtendaji,Samwel Muro.
Akizungumza katika hafla hiyo Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia,Prof. Makame Mnyaa Mbarawa, alisema vifaa hivyo vinatarajiwa kuwekwa katika mikoa yote ya Zanzibar ili kurahisisha huduma ya mawasiliano kwa viongozi na wananchi.
Alisema uwekaji wa vifaa hivyo kutawezesha viongozi, watendaji na wataalamu kufanya kazi zao kwa kushirikiana na kuwasiliana na wadau wengine wakiwa katika sehemu zao za kazi bila ya kulazimika kusafiri na kutumia fedha.
Alisema huduma hiyo pia itapunguza gharama na muda mkubwa unaotumika katika mawasiliano na vyombo vya usafiri sambamba na kuimarisha mawasiliano serikalini.
Aidha alisema maeneo yatakayofungwa mitambo hiyo ni Ofisi ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Ikulu, Ofisi za Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano, Chuo cha Amali Mkokotoni na Makunduchi Community Center kwa Unguja.
Kwa upande wa kisiwa cha Pemba alisema ni Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais Chake Chake na Ofisi ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi iliyopo Wete.
Alisema katika kuhakikisha matumizi ya TEHAMA yanakuwa hasa katika ofisi za Serikali tayari wizara yake imeshafunga mitambo hiyo katika makao makuu ya mikoa 21 ya Tanzania Bara ikiwemo ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Fedha na ofisi ya Rais-Menejiment ya Utumishi wa Umma na TAMISEMI.
Hata hivyo, alisema uwepo wa mkonga wa taifa wa mawasiliano utawawezesha kuwepo kwa ufanisi mkubwa kupitia matumizi ya video conference na serikali kwa kuwa mkonga huo una uwezo mkubwa wa mtandao wa internet wenye kasi.
Aliongeza ujenzi wa mkonga wa taifa unaotekelezwa kwa awamu tano ambapo awamu ya kwanza na ya pili umeshakamilika na umeanza kutumia tokea mwaka 2012 zikiwa na jumla ya kilomita 7,560.
Alisema kwa sasa wizara yake ipo katika hatua ya utekelezaji wa awamu ya tatu inayohusisha ujenzi wa vituo vitatu vya kutunza kumbukumbu (internet data centres) vitakavyojengwa Dar es Salaam, Dodoma na Zanzibar.
Akizungumzia matumizi mabaya ya mitandao, alisema sheria zinaandaliwa ili kuwadhibiti watu hao.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano,Issa Haji Ussi aliishukuru Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwaletea huduma hizo.