Na Mwandishi wetu
NCHI za Afrika zimetakiwa kuwa na msimamo mmoja kuhusu jinsi ya kukabiliana na madhara ya mabadiliko ya hali ya hewa.
Misimamo huo wa Afrika unatarajiwa kuwasilishwa kwenye mkutano mkubwa wa Dunia kuhusu masuala ya mabadiliko ya hali ya hewa unaotarajiwa kufanyika New York, Marekani Septemba, 2014.
Akiwakilisha ripoti ya Kamati ya Viongozi wa Afrika kuhusu Mabadiliko ya Hali ya Hewa Duniani, katika mkutano wa viongozi wa Afrika (AU), Rais Kikwete alisema kamati yake inataka kujikita na kujihusisha na masuala yanayohusu fedha na teknolojia, hatua za kupunguza madhara, na hatua mtambuka ambazo zitahusisha progamu za vijana, wanawake na hata kuhusisha Balozi mbali mbali za Afrika katika suala zima la mabadiliko ya hali ya hewa na pia kuhusisha Jumuiya ya Kimataifa na kufuatilia mapendekezo mbali mbali.
Aliziasa nchi za Afrika kuwa na utashi wa kisiasa na lengo la pamoja katika kukabiliana na suala hilo ili kufanikisha lengo la dunia la hali ya hewa katika kipindi cha nusu ya pili ya karne ijayo.
Alisema ili kufanikisha juhudi hizo, bara la Afrika linahitaji msaada mkubwa wa fedha na teknolojia ya kisasa.
Mapema katika kikao hicho ambacho pia kilihudhuriwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) ,Ban Ki Moon, Rais Kikwete alisema mkutano ujao wa UN kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa duniani ni chachu ya makubaliano ya mkataba wa hali ya hewa ifikapo 2015.
Ripoti za karibuni kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa inaonesha hali ya kilimo, afya, maji na nishati ziko hatarini na kwamba joto duniani limepanda kwa sentigredi 0.85, hali ambayo inaashiria hali mbaya.