Na Abdi Suleiman, Pemba
BAADA ya huduma za upasuaji kusimama kwa muda katika hospitali ya wilaya Chake Chake baada ya kuharibisha mashine ya dawa ya usingizi,(anaesthetic machine), hatime huduma hizo zimerejea baada ya mashine hiyo kongwe kutengenezwa.
Taarifa ya kuharibika mashine hiyo kwa mara ya kwanza ilichapishwa katika ukurasa wa mbele wa gazeti hili.
Huduma hizo zilizosimama tokea Juni 20 na kusababisha wagonjwa na wajawazito wanaohitaji kufanyiwa upasuaji kuhamishiwa hospitali za Mkoani na Chake, zimeanza kurejea tena kuanzia Jumatatu ya wiki hii.
Dk. Alawi Hamad Othman,alisema huduma hiyo imerejea baada ya masheine hiyo kufanyiwa matengenezo na mafundi wa wizara.
Hata hivyo, alisema mashine hiyo imeshachoka na wakati wowote inaweza kuharibika tena.
“Baada ya wandishi kuandika habari ya kuharibika mashine hii, fundi mkuu wa wizara alikuja na kuungana na fundi wa hospitali yetu kuitengeneza na imekubali na sasa tunaendelea kutoa huduma kama kawaida yetu, tunawashukuru (waandishi kwa kutusaidia),”alisema.
Mashine hiyo ambayo ni moja katika hospitali hiyo inayohutumia wagonjwa kutoka wilaya nzima ya Wete, ipo hospitalini hapo tokea 1992.
Baadhi ya wagonjwa waliofanyiwa upasuaji, waliiomba serikali kuharakisha kupatikana mashine mpya.
Walisema kuharibika kwa mashine hiyo kumesababisha mateso makubwa kwao.
Ali Khamis mume wa Mariyam Kambi, aliyefanyiwa upasuaji, alisema walilazimika kukaa hospitali kwa muda wa wiki moja kusubiri mashine hiyo itengenezwe huku mke wake wakiwa na maumivu makali ya tumbo.