Hafsa Golo na Habiba Zarali
LICHA ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, kuwataka wafanyabiashara kupunguza bei za bidhaa katika mwezi mtukufu wa Ramadhan, wafanyabiashara wamepuuza agizo hilo .
Uchunguzi uliofanywa na gazaeti hili umebaina bei za bidhaa zinazotumiwa na Waislamu kwa ajili ya futari, zimepanda mara dufu katika masoko yote makuu Unguja na Pemba .
Katika soko kuu la Mombasa, bei ya ndizi mbichi, magimbi, viazi vikuu, ndizi mbivu zimepanda karibu kwa asilimia 30.
Katika soko hilo ndizi mbichi aina ya mkono wa tembo inauzwa baina ya shilingi 30,000 hadi 50 na kidole kimoja kinauzwa baina ya shilingi 3,000 na 5,000 wakati fungu la viazi vitamu linauzwa shilingi 2000 na 5,000.
Muhogo ambao uliozoeleka kuuzwa shilingi 1,000 kwa fungu moja, bei imebakia pale pale lakini wafanyabiashara wamepunguza ukubwa wa fungu.
Nazi zimepata bei ya kutisha kutoka shilingi 5000 hadi shilini 18,000 huku samaki wamekuwa adimu na hao wanaopatikana wanauzwa kwa bei kubwa hadi shilingi 10,000 kwa kipande.
Hata hivyo, bei ya nyama imebakia baina ya shilingi 8000 na 9000 kwa kilo moja.
Wakizungumzia hali hiyo baadhi ya wafanyabiashara walisema wanalazimika kupandisha bei kutokana na wakulima kupandisha bei huku bidhaa zikiwa pungufu masokoni.
Mmoja ya wauza ndizi, Kihange Haji Juma, alisema wanalazimika kuuza bei ya juu kwa sababu ndizi zimekuwa adimu na hizo zinazopatikana wanauziwa bei kubwa.
Nae mfanyabiashara wa nazi, Abdi Mohammed, alisema nazi zimekuwa adimu na kwa jumla wananunua kati ya shilingi 1200 na 1600 kwa nazi moja.
Katika masoko ya Mwanakwerekwe na Darajani, hali ni mbaya zaidi hali iliyosababisha wananchi wengi kumiminika katika soko la Mombasa .
Kisiwani Pemba, pia hali sio nzuri kutokana na bidhaa nyingi kupanda bei na kusababisha wananchi kulalamika.
Katika soko kuu la Qatar, ndizi mbichi zinauzwa hadi shilingi 20,000 na kusababisha Waislamu wengi kukimbilia futari za nafaka.
Hassan Kombo (45), mkaazi wa Chake Chake, alisema wafanyabiashara wengi huweka mbele tamaa ya pesa ifikapo mwezi wa Ramadhani, bila ya kuzingatia hali za maisha ya wananchi ambao wengi wao ni maskini.
“Hali inatisha, wafanyabiashara hawana hata huruma, tunashindwa kununua bidhaa za shambani na tunakimbilia nafaka,” alisema.
Bibi Zuhura Khamis (33), mkaazi wa Wesha, alisema imekuwa kawaida kwa wafanyabiashara kuongeza bei ifikapo mwezi wa Ramadhani licha ya serikali kuwataka kupunguza bei.
Amour Juma (49), mkaazi wa Chake Chake, alisema mwezi wa Ramadhani si wa kufanyia uchumi, bali ni wa kusaidiana lakini wafanyabiashara wanashindwa kufahamu hilo .
Kwa upande wao wafanyabiashara kisiwani humo, walisema kupanda bei kwa vyakula katika mwezi wa Ramadhani kunatokana na kupanda ushuru.