Na Ali Mohamed
MKURUGENZI Mwendeshaji wa Shirika la Biashara la Taifa Zanzibar (ZSTC),Mwanahija Almas Ali, amewataka Wakaguzi, Wapasishaji na Makarani wa shirika hilo, kufanya kazi kwa uadilifu na busara wanapowahudumia wakulima wa karafuu .
Akitoa nasaha kwa watendaji hao katika mkutano wa kutathmini utendaji wao katika msimu wa mavuno ya karafuu kwa mwaka 2013/2014, katika ukumbi wa Benjamin Mkapa Wete, Mkurugenzi huyo alisema pamoja na mafanikio ya shirika katika manunuzi ya karafuu bado kuna malalamiko kutoka kwa wakulima vituoni.
Alisema katika msimu wa 2013/2014 ZSTC imevuka makadirio katika manunuzi ya karafuu ambapo mafanikio hayo yanaongeza matumaini ya serikali na wananchi kwa shirika katika kuimarisha uchumi na ustawi wa wananchi kupitia zao la karafuu.
“Serikali na wananchi wana matumaini makubwa kwa ZSTC kupitia zao la karafuu katika kuimarisha uchumi na ustawi wa wananchi kwa sababu karafuu ni zao pekee Zanzibar lilochangia kwa asilimia kubwa pato la taifa hivyo watendaji tuwe makini ,” alisema.
Alisema ni lazima watendaji hao ambao wanaazimwa kutoka taasisi za serikali wawe waadilifu na kutumia busara zaidi wanapowahudumia wakulima katika vituo vya manunuzi .
Kwa upande wao watendaji hao walisema kwa kawaida huwa wanakabiliana na changamoto nyingi katika vituo vya manunuzi kutoka kwa wakulima na waliahidi kutumia busara na taaluma ya huduma kwa wateja katika kukabiliana na changamoto hizo.
Akitoa mada ya uadilifu katika biashara, Ustadh Omar, alisema kazi ni ibada hivyo ni vyema watendaji hao ZSTC wakazingatia adilifu katika vipimo ili kulifanya zao la karafuu kuendelea kuwa neema kwa wananchi.