Quantcast
Channel: ZanziNews
Viewing all articles
Browse latest Browse all 35036

Dk Shein awaambia waathirika wa ujenzi wa Barabara Wete - Gando: Tutawalipa fidia

$
0
0
STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
    Zanzibar                                                  08 Julai, 2014
---
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amewahakikishia wananchi walioathirika na ujenzi wa barabara ya Wete-Gando na Gando-Ukunjwi kuwa watalipwa fidia lakini wanapaswa kufanya subira kwa kuwa tathmini ya athari za ujenzi huo itafanyika kwa ukamilifu baada ya ujenzi kukamilika ifikapo mwezi Disemba mwaka huu.
 
Akizungumza na wananchi wa kijiji cha Raha, wilaya ya Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba leo wakati akikagua ujenzi wa barabara hizo, Dk. Shein aliwaambia wananchi hao kuwa kwa sasa Serikali haiwezi kufanya malipo yoyote hadi hapo ujenzi utakapokalimika na kufahamu hasara kamili aliyopata kila mwananchi.
 
Wananchi wa kijiji cha Raha walilalamika kuwa ujenzi wa barabara hizo umeathiri nyumba zao pamoja na mazao na kuwa pamoja na Serikali kufanya tathmini Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano hadi sasa imeshindwa kuwalipa fidia.
 
Hata hivyo kwa mujibu wa maelezo ya Waziri wa Wizara hiyo Rashid Seif malipo ya fidia yalifanywa kwa wananchi waliovunjiwa nyumba zao tu wakati ujenzi ulipoanza na kwa wale ambao nyumba zao hazikuvunjwa zitatathminiwa mwishoni mwa mradi kwa kuwa bado athari itaendelea wakati ujenzi haujakamilika.

 
Kwa hivyo Dk. Shein aliutaka uongozi wa Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano kuweka mpango maalum wa kulipa fidia wananchi walioathirika na ujenzi wa barabara hizo hususan kwa walioharibiwa miti yao ambao ni miongoni mwa waliotoa malalamiko.
 
Akijibu malalamiko ya Bwana Bakari Rajab Bakari kuhusu kutofahamu lolote kuhusu fidia ya miti yao iliyokatwa kupisha ujenzi huo ikiwemo mikarafuu, minazi, mishelisheli na miembe, Dk. Shein aliusisitizia uongozi wa Wizara hiyo kufanya mikutano ya pamoja na wananchi ili kuwapa taarifa za mara kwa mara kuhusu hatua zilizofikiwa kuhusu malipo yao.
 
Katika hatua nyingine Dk. Shein alilazimika kuzitembelea nyumba zilizodaiwa kuathirika za baadhi ya wakazi wa kijiji hicho ili kumaliza ubishi kati ya wananchi hao na wizara kuhusu malalamiko kuwa nyumba zao hazikutembelewa wala kutathminiwa huku viongozi wa wizara wakisisitiza kuwa wamezitembelea.
 
Baada ya kufaya hivyo Dk. Shein aliwataka viongozi wa wizara na mkoa Kaskazini Pemba kuwatembelea wananchi hao ili kuweka mambo yote sawa ili kuepuka malalamiko wakati malipo yatakapowadia.
 
Akizungumzia maendeleo ya ujenzi wa barabara hizo, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza na Mapinduzi alieleza kuwa kumekuwepo na mabadiliko tangu alipozitembelea barabara hizo mwanzoni mwa mwaka huu.
 
Kwa hivyo amesisitiza Mkandarasi kumaliza ujenzi kwa mujibu wa ratiba mpya ambayo ujenzi umepangwa kukamilika mwezi Disemba mwaka 2014.
 
Alieleza matumaini yake kuwa kila upande utatimiza wajibu wake na kuona barabara hizo zitakamilka kama ilivyopangwa.
 
Awali akitoa maelezo kwa Mhe Rais, Katibu Mkuu wa Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano Dk. Juma Malik Akili alieleza kuwa ujenzi wa barabara za Wete- Gando hadi Ukunjwi na Wete-Konde ambazo ujenzi wake ulisimama kutokana na changamoto mbalimbali unatarajiwa kumalizika mwezi Disemba mwaka huu.
 
Barabara hizo ambazo awali zilitarajiwa kumalizika mwaka 2012 zinajengwa kwa fedha kutoka BADEA, SAUDI FUND na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Hadi sasa alieleza kuwa utekelezaji umefikia asilimia 75.
 
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi yuko kisiwani Pemba kwa ziara ya siku tatu ambapo kesho anatarajiwa kuzindua ununuzi wa zao la karafuu,kutembelea mashamba ya karafuu pamoja na miradi ya ufugaji wa samaki.
 
Wakati huo huo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameuhimiza uongozi wa Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) kusogeza huduma za umeme katika vijiji vya Mlima Sudi, Buyuni na Mkote katika shehia ya Ukunjwi, wilayaya Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba.
 
Dk. Shein ametoa agizo hilo wakati akijibu ombi la wananchi wa vijiji vya jirani ya kijiji cha Raha wakati alipokuwa akikagua barabara za Wete-Gando na Gando-Ukunjwi.
 
Alieleza ni muhimu kuwapelekea huduma hiyo ambayo tayari inapatikana katika kijiji cha Raha ambapo ni karibbu na vijiji hivyo ambapo kwa kufanya hivyo kutalipatia shirika mapato zaidi na kujijengea uwezo.
 

Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822 

Viewing all articles
Browse latest Browse all 35036

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>