Na Mwashamba Juma
UMOJA wa Afrika (AU), umeitaka Tanzania kushajiisha masuala ya jinsia katika uchaguzi ujao ili kutoa ushiriki mzuri kwa wanawake na makundi maalum wakiwemo watu wenye ulemavu.
Msaidizi Mkuu, kitengo cha demokrasia na uchaguzi wa AU, Shumbana Karume, aliyasema hayo kwa niaba ya Kamishna wa masuala ya siasa wa umoja huo, Dk. Aisha Abdullai akizungumza hoteli ya Serena wakati akifungua mafunzo ya wiki moja yaliyohusu jinsia na uchaguzi.
Alisema katika kufanikisha uchaguzi huru na wa haki pamoja na ushiriki wa kila mlengwa, AU imeona haja ya kuchagua kipengele cha jinsia kwenye uchaguzi ili kuyafanya masuala ya jinsia kuwa ya kwaida katika harakati za uchaguzi ujao sambamba na kutoa fursa ya ushiki wa kila mmoja hasa wanawake na wenye ulemavu.
Alisema masuala ya jinsia kwa nchi wanachama wa AU ni mambo yanayopewa kipaumbele na kusisitizwa zaidi na Mwenyekiti wa AU, Dk. Dlamini Zuma, katika karakati za maendeleo hususan kwa wanawake na wenye ulemavu.
Alisema lengo la mafunzo hayo ni kuujengea uwezo uongozi wa Bodi za uchaguzi Tanzania (EMBs) ili kutekeleza kivitendo uchaguzi ulio huru na wa haki katika kuifikia demokrasia ya kweli.
Aliongeza AU itatoa wataalamu watakaofanya kazi na bodi hizo katika hatua za matayarisho katika kukabiliana na uchaguzi mkuu wa 2015.
Aidha aliuagiza uongozi huo kutoa taafa kwa AU ikiwa watahitaji msaada wa teknolojia na kwamba umoja huo uko tayati kuisaidia Tanzania katika kufanikisha chaguzi zake.
Alisema Kamisheni ya Umoja wa Afrika kupitia kitengo cha demokrasia na uchaguzi iko tayari kuisaidia Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) kufanikisha uchaguzi mkuu ujao na kuongeza kuwa mafunzao hayo yatafuatiwa na mengine kwa Tume ya Uchaguzi ya Taifa (NEC) ambapo Tanzania itakuwa nchi ya tatu kunufaika na misaada ya AU kwa mwaka ikitanguliwa na Bukina Faso na Madagascar.
Aidha mataifa kama Guinea, Cameroon, Ivory Coast, Jamuhuri ya Afrika ya Kati na visiwa vya Comoro pia zinatarajiwa kupokea misaada ya kiufundi kutoka AU katika chaguzi zao.
Aliwataka washiriki wa mafunzo hayo kujikubalisha kushiriki kikamilifu ili kufanikisha mafunzo hayo ambayo ni mtiririko wa makubadiliano baina ya Tanzania na AU katika kuunga mkono juhudi za maandalizi ya uchaguzi ujao.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mwenyekiti Tume ya Uchaguzi Zanzibar, Jesha Salum Jecha, alisema uchaguzi ujao 2015 unatarajiwa kutoa ushiriki zaidi kwa watu wenye ulemavu na wanawake ambao kwa kawaida hupata nafasi ndogo na kosesha haki zao za msingi.
Nae mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo, Mwanajuma Zahor Abeid ambae pia ni Katibu Mkuu Jumuiya ya Watu Wenye Ulemavu Zanzibar (UWZ), alisema anatarajia mafunzo hayo yatawajengea uwezo hasa kwa viongozi wa jumuiya yake na kwamba taaluma hiyo itawafikia walengwa kwa wakati ili kuwapa uwezo wa kupiga kura zaidi.
Kwa upande wake Naibu katibu Mkuu wa chama cha ADC, Juma Said Sanani, alisema anatarajia vyama vya siasa vitabadilika baada ya mafunzo hayo.
Mapema Mkurugenzi Tume ya Uchaguzi Zanzibar, Salum Kassim Ali, alisema mafunzo yatawasaidia wadau wengi kwenye uchaguzi ujao na kutoa uelewa wa uhuru na haki kwa mpiga kura.