STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 15 Julai, 2014
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein leo amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi mpya wa Tanzania nchini Urusi Mheshimiwa Luteni Generali Wynjones Mathew Kisamba.
Balozi Kisamba alifika Ikulu kujitambulisha na kumuaga Mheshimiwa Rais tayari kutumikia wadhifa wake huo mpya kuchukua nafasi ya aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini humo Balozi Jaka Mwambi ambaye amestaafu.
Katika mazungumzo hayo Dk. Shein alimueleza Balozi Kisamba kuwa uhusiano wa Tanzania na Urusi ni wa miaka mingi na umekuwa wa kirafiki kwa hivyo azma ya Serikali wakati wote ni kuona uhusiano huo unaimarika kwa kupanua maeneo ya ushirikiano hususan biashara, uwekezaji na utalii.
Alimpongeza Balozi Kisamba kwa kuteuliwa katika wadhifa huo na kumshukuru kwa kukubali uteuzi wa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kubainisha kuwa hiyo ni heshma kubwa kwake kuitumikia nchi yake nje ya nchi.
Kwa hiyo alimkumbusha kuitekeleza vyema Sera ya Tanzania ya diplomasia ya uchumi wakati wote akiwa nchini humo na kueleza kuwa hiyo ni nafasi pekee kwa Tanzania kutangaza fursa za kiuchumi kuvutia biashara na uwekezaji.
Dk. Shein alifafanua kuwa hivi sasa Urusi ni moja kati ya mataifa yanayotoa watalii wengi duniani lakini watalii wa nchi hiyo si wengi wanaotembelea Tanzania hivyo ubalozi wa Tanzania nchini humo hauna budi kufanya jitihada kuonesha kuwa Tanzania ni nchi yenye vivutio na kuwafanya raia wa Urus i kuja Tanzania.
Kwa upande wa uwekezaji, alieleza kuwa Urusi hivi sasa inafanya vizuri hasa katika ya nishati ikiwemo gesi na mafuta hivyo ipo haja Ubalozi huo kuwahamasisha wawekezaji wa nchi hiyo kuja Tanzania.
Katika mazungumza hayo Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi alimueleza Balozi Kisamba haja ya kuendeleza jitihada za kupata fursa zaidi za masomo nchini humo kwa vijana wa Tanzania hasa ukizingatia kuwa gharama za masomo bado ni ndogo ikilinganishwa na nchi nyingine barani ulaya.
Pamoja na kufanya hivyo alisisitiza haja ya Ubalozi wa Tanzania nchini Urusi ya kuwapatia ushauri wa mara kwa mara wanafunzi wa Tanzania wanaosoma nchini humo na nchi inazoziwakilisha, kuishi vizuri na kwa ushirikiano ili waweze kuhitimu masomo yao vyema.
Alimueleza Balozi huyo kuwa ni muhimu wanafunzi hao wakaelimishwa juu ya umuhimu wa kurejea nyumbani mara wamalizapo masomo yao na kuelewa wajibu walionao kushiriki katika ujenzi wa taifa.
Kuhusu ushirikiano katika sekta ya afya, Dk. Shein alimtaka Balozi kufanya jitihada za kuangalia namna ya kufufua tena ushirikiano wa karibu katika sekta hiyo ikiwemo nafasi za mafunzo kwa watumishi wa afya nchini.
Alibainisha kuwa Taasisi za elimu ya afya za nchi hiyo zina uwezo mkubwa hivyo ni muhimu kwa Tanzania kuwa na ushirikiano wa karibu na nchi hiyo katika sekta hiyo kwa manufaa ya nchi.
Kwa upande wake Balozi Kisamba alimueleza Mhehimiwa Rais kuwa ni kweli kwamba wako watanzania wengi wanaosoma nchini Urusi katika vyuo mbalimbali na matarajio ni kuwa wanafunzi wengi zaidi wataendelea kwenda nchini humo kwa masomo.
Kwa hivyo alisema ipo haja ya kuimarisha uratibu wa wanafunzi wanaokwenda nchini humo kwa kuwa si wote wanaopitia serikalini bali wengine wanakwenda kupitia mawakala.
Alimshukuru Mheshimiwa Rais kwa kumpatia fursa ya kukutana naye na aliahidi kuyafanyia kazi maelekezo yake.
Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822