Quantcast
Channel: ZanziNews
Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Dhana 10 potofu kuhusu muungano wa Tanganyika na Zanzibar

$
0
0
Na Mwandishi wetu
Kuna tishio kubwa dhidi ya Muungano wetu.  Tishio hilo liko zaidi kwenye dhana kuliko udhaifu wa dhamira ya Muungano wenyewe. Tishio hilo limedhihirika katika kipindi hiki cha Mchakato wa Kuandaa Katiba Mpya ya nchi yetu.
 Mjadala wa rasimu ya Katiba mpya umetawaliwa kwa kiasi kikubwa na agenda ya Muungano.  Yamejitokeza makundi yenye mitazamo tofauti juu ya Muungano. Wako wanaoutaka uendelee, wako wasioutaka, wako wanaotaka urekebishwe, ilihali kuna kugongana kwa fikra. Kinachowaunganisha wote ni muungano huohuo wanaoujadili.
 Mgongano wa maoni juu ya Muungano ni jambo jema na la kujivunia. Mgongano huu unadhihirisha jinsi ambavyo Muungano uko hai maana Muungano usiokuwa hai haujadiliwi. Mgongano huu wa fikra umetufunulia kile ambacho hatukuwa tukikijua au tukikipuuza. Mara zote tumekuwa tukiamini kuwa ni Wazanzibari pekee wenye ulalamishi juu ya Muungano, lakini mjadala unavyokwenda tumeona pia kwamba hata wabara nao wana malalamiko yao. Hivyo, ni sahihi kusema kuwa mjadala wa Muungano na mgongano wa fikra juu ya Muungano wenyewe vinatupa fursa ya kuuboresha Muungano kuliko kuuvunja.

 Sio sahihi kuogopa watu kuujadili Muungano wao, wala hatuwezi kuujenga Muungano wenyewe kwa kuukinga dhidi ya mjadala. Ikiwa sababu na dhamira ya kuungana ni njema, busara ile ile iliyopelekea kuungana itaendelea kutawala na hatimaye kushinda jaribio lolote la kuuvunja. Muungano wa hila ndio Muungano pekee ambao unapaswa kukingwa dhidi ya mjadala na kuhojiwa. Muungano wetu sio Muungano wa hila, hivyo unapaswa kujadiliwa na kuhojiwa. Wananchi wanayo haki ya kuutathmini ikiwa umetimiza malengo na matarajio yao, maana tatizo laweza kuwa ni kubadilika kwa matarajio ya wananchi kuliko kufeli kwa Muungano wenyewe.
 Tatizo tulilo nalo ni kuwa wenye dhamana ya kurithisha Muungano huu kwa vizazi vilivyofuatia wanagwaya kufanya hivyo. Kugwaya kwao, kwa maoni yangu hakutokani na Muungano wenyewe kuwa wa hila, bali udhaifu wa viongozi hao katika kuuelezea na kujenga hoja. Kuusimamia ukweli daima huhitaji ujasiri, wakati mwingine, ujasiri pekee hautoshi, ujasiri huo hutakiwa kuambatana na uadilifu. Maadam baadhi ya viongozi wetu wamekengeuka kimaadili, wanakosa ujasiri wa kusema na kuusimamia ukweli wanaouamini. Huusema ukweli huu pembeni tu lakini sio mbele ya jamii. Upungufu huu hufanya kusiwepo na watetezi wa Muungano mbele ya jamii.
 Silaumu hata kidogo wale wanaohoji Muungano wetu haswa Muundo na umuhimu wake leo. Ukiwasikiliza wanazo hoja, tena hoja nzuri na za kimantiki. Hili linadhihirisha kuwa hawana tatizo la uelewa, na wakipatiwa hoja mbadala wanaweza kuelewa. Wengi wa hawa hawana taarifa za kutosha juu ya Muungano wenyewe, hivyo wanauhoji kwa taarifa chache za kuokoteza. Hata mimi nimewahi kuwa mhanga wa hilo hadi nilipofanikiwa kudadisi na kupata taarifa zaidi kwa njia ya mapokeo, kwa kuwa nyingi ya taarifa hizi hazijahifadhiwa kwenye maandiko. Haiyumkini, hali hii inatokana na utamaduni wetu wa kutokuandika historia na matukio.
 Kutokana na pengo la taarifa juu ya Muungano, kumepelekea kuibuka kwa dhana mbalimbali nyingi zikiwa potofu. Uwepo wa dhana potofu ni kielelezo cha ombwe, na kawaida, ombwe huvutia ghasia na mwangwi. Katika mwangwi huo, dhana potofu hupata uhalali na huweza kuzaa nadharia. Katika mjadala unaoendelea kuhusu Muungano hivi sasa, zipo walau dhana kumi potofu ambazo zimetamalaki maoni ya wengi kuhusu Muungano. Dhana hizi potofu zinaainishwa na kuchambuliwa katika aya zinazofutia.
1)        Tatizo ni Muundo na Suluhisho ni Serikali Tatu
 Imejengeka dhana kwa muda mrefu kwamba tatizo la Muungano wetu ni Muundo wake wa Serikali mbili. Dhana hii inatuaminisha kuwa mwarobaini wa tatizo hilo ni Serikali moja au tatu. Ajabu zaidi, Serikali moja haipigiwi sana upatu kama serikali tatu.
 Hapa tatizo linasemekana ni Tanzania Bara kukosa Serikali yake. Wengine huenda mbele na kusema kwamba, kitendo cha Serikali ya Muungano kuwa ni hiyo hiyo inayoshughulikia masuala ya Tanganyika, kunaifanya Tanganyika kutumia rasilimali za Muungano kujinufaisha. Aidha, upande mwingine unasema, Serikali ya Muungano kuwa ndio hiyo hiyo ya Tanganyika kunainufaisha Zanzibar kwa kunufaika na mapato yatokanayo na uzalishaji ndani ya Tanganyika. Hivyo, Serikali tatu zitasaidia kutenganisha shughuli za Muungano na shughuli za Tanganyika na Zanzibar, hivyo, kuepusha kupunjana. Ni wazi, kila upande una mashaka juu ya upande mwingine. Hivyo, msingi wa kutaka Serikali tatu unatokana na kutokuaminiana tu. Kutokuaminiana huku hakutatuliwi kwa kuongeza idadi ya Serikali. 
 Hoja ya Serikali tatu sio mpya, ilikuwapo mezani wakati waasisi wa Muungano walipokubaliana kuwa na Serikali mbili badala ya tatu au moja. Busara ya waasisi ilitawala katika kutafuta msawazo kati ya gharama za uendeshaji wa Serikali ya Muungano na utaifa wa Mzanzibari. Muundo wa Serikali tatu ulionekana ungekuwa wa gharama kubwa haswa kwa Serikali ya Tanganyika ambayo ndio ingelazimika kubeba gharama kubwa. Hali kadhalika, Serikali moja ilihofiwa ingeufuta utaifa wa mzanzibari kwa kuzingatia udogo wa kisiwa chenyewe ikilinganishwa na Tanganyika na idadi ndogo ya watu ambayo wakati huo ilikuwa inakadiriwa kuwa laki tatu. Utaifa wa mtanganyika na utamaduni wake usingeweza kutishiwa kumezwa na Uzanzibari.
 Maumbile ya Tanganyika na Zanzibar hayajabadilika kwa miaka 49 kiasi cha kuifanya hoja ya Serikali tatu kuwa na mashiko sasa. Tanganyika ina kilometa za mraba 942,553 na Zanzibar ina kilometa za mraba 2650 (Eneo la Zanzibar linaingia mara 355 katika eneo la Tanganyika). Tangayika na Zanzibar kwa pamoja zina jumla ya kilometa za mraba 945,203.  Tanganyika ina idadi ya watu milioni 43,625,354 na Zanzibar ina watu 1,303,569 kwa mujibu wa Sensa ya Taifa ya 2012. Tanganyika ina kaya milioni 9,109,150 na Zanzibar 253,608. Ujazo wa idadi ya watu Zanzibar ni watu 530 kwa kilometa moja ya mraba wakati Tanganyika ni watu 49 kwa kilometa ya mraba. Takwimu hizi zingali zinahalalisha hoja ya Serikali mbili ya Waasisi wa Muungano.
 Tukienda na maelezo aliyotoa Mheshimiwa Jaji Warioba kuwa gharama za kuendesha mambo saba ya muungano yanayopendekezwa katika mfumo wa Serikali ya tatu ni Trilioni tatu, hoja ya serikali mbili inaimarika. Tukiwa na Serikali tatu, mantiki itataka nchi washirika wa Muungano waongeze michango ya gharama za uendeshaji wa Serikali hiyo ya tatu. Aidha, kutokana na ukweli kuwa Serikali ya Tatu inazaliwa katika mazingira ya kutoaminiana, hisia mbaya na dhamira ovu, utayari wa kila upande kuchangia gharama utabeba hulka hizo hizo. Bajeti ya Tanzania kwa mwaka wa fedha 2013/2014 ni shilingi Trilioni 18.2 na bajeti ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa 2013/2014 ni shilingi bilioni 658.5. Ikiwa tutaondoa masuala ya Muungano, bajeti ya Tanganyika itakuwa ni Trilioni 15.2.
 Ndani ya mfumo wa Serikali mbili, kuna unafuu mkubwa wa gharama kwa kuwa gharama za kiuendeshaji zinapungua kwa sababu Serikali ya Muungano kwa kutumia nguvu kazi na vitendea kazi hivyo hivyo inatekeleza pia shughuli za Tanganyika. Katika mfumo wa Serikali tatu, nachelea kuwa gharama zitakuwa zaidi ya trilioni tatu zinazosemwa na Jaji Warioba kwa kuwa hatutaweza kukwepa gharama mpya za kiuendeshaji za Serikali ya muungano inayojitegemea kama vile majengo, watumishi vitendea kazi nk. Ongezeko hilo maana yake ni kodi zaidi na michango zaidi kutoka nchi washirika. Serikali tatu ni neema kwa wanasiasa maana itapanua vyeo lakini msiba kwa wananchi maana watalazimika kuigharania kwa kodi zaidi.
 Takwimu hapo juu zinashindwa kunishawishi kuwa mantiki ya Serikali mbili kama ilivyokubaliwa na waasisi wetu imepitwa na wakati. Sioni ni kwa vipi, Muundo wa Serikali tatu leo hii utalinda utaifa wa Zanzibar dhidi ya hofu ya kumezwa huku ikipunguza gharama za uendeshaji wa Muungano wenyewe. Utaifa wa Tanganyika haujatoweka kutokana na ukubwa wake na tishio la Uzanzibar kutoweka bado lipo ikiwa tutakuwa na Serikali moja kama takwimu za idadi ya watu zinavyoonyesha.
 Ikiwa kweli tunayo dhamira ya kuendelea na Muungano, basi njia yenye uhalisia ni Serikali mbili sio tatu wala moja. Mazingira yaliyopelekea Serikali mbili yangali hayajabadilika hata sasa. Ni kweli Muundo wa Serikali mbili una changamoto zake, lakini changamoto hizo zinatokana na mfumo zaidi kuliko Muundo, na kuwa tunaweza kurekebisha mfumo ndani ya Muundo uliopo. Changamoto za Muundo wa Serikali mbili zinahimilika kuliko changamoto za Serikali tatu au moja zitakazoleta changamoto za gharama na utaifa wa Uzanzibari. Hivyo, nachelea kusema kuwa dhana kuwa tatizo ni muundo wa Serikali mbili na kwamba Serikali tatu ni suluhisho ni dhana potofu.
2)        Zanzibar inanyonywa, Tanganyika inafaidi kuliko Zanzibar (na kinyume chake)
 
Ipo dhana nyingine kuwa Zanzibar inanyonywa ndani ya Muungano na Tanganyika inafaidi ndani ya Muungano. Kinachostaajabisha, pia wapo wanaosema Tanganyika inanyonywa na Zanzibar inafaidi. Zote hizi ni hoja ambazo msingi wake ni husuda, na husuda haiondolewi na idadi ya Serikali. Watu wenye husuda wataendelea kuwa na husuda hiyo ndani ya Serikali moja au tatu.
 Wenye kuunga mkono dhana ya Zanzibar kunufaika kushinda Tanganyika wanatumia mifano ya haki ya kumiliki ardhi, makazi na mgawanyo wa madaraka wanaoupata wananchi wa Zanzibar. Ni kweli kuwa wazanzibari wengi (inasadikiwa si chini ya laki nne) wanaishi bara na wanamiliki ardhi na nyumba. Aidha, wazanzibari wanashikilia nyadhifa kwenye Wizara na Sekta zisizo za Muungano kama afya na mawasiliano. Ni kweli pia watanganyika nao wanashikilia nyadhifa nyingi kwenye Wizara na Sekta za Muungano, na watanganyika wanashikilia ajira nyingi kwenye sekta ya utalii Zanzibar.  Isitoshe, wafanyabiashara wa Tanganyika wanauza bidhaa nyingi Zanzibar.
 Kilicho dhahiri ni kuwa hakuna upande wa Muungano ambao haufaidiki kabisa kutokana na uwepo wa Muungano. Sina mashaka, manufaa hayo yaweza kupishana kutokana na maumbile yenyewe ya nchi hizi mbili. Mathalani, watanganyika hawana tatizo kubwa la ardhi kiasi cha kuathirika kwa kukosa ardhi Zanzibar. Kupata ardhi ya makazi Zanzibar yaweza kuwa tabu kwa mtanganyika lakini sio ardhi ya uwekezaji, maana hata wawekezaji kutoka nje hupata ardhi Zanzibar. Tukirejea kwenye takwimu za ujazo wa watu Zanzibar kwa kilometa ya mraba, ni dhahiri kuwa tayari Zanzibar kuna tatizo la ardhi, sio tu kwa mbara, hata kwa mzanzibari mwenyewe. Hivyo, dhana ya kuwa upande mmoja unanufaika na mwingine haunufaiki ni dhana potofu. Pande zote zinanufaika, pengine, upo uwezekano wa kunufaika zaidi Ikiwa tutarekebisha mifumo ndani ya muundo wa Serikali mbili zilizopo.

3)        Nje ya Muungano Zanzibar itanufaika zaidi na Tanganyika itatua mzigo
 
Ipo dhana kuwa nje ya Muungano, Zanzibar itanufaika zaidi na Tanganyika itatua mzigo. Wenye kujenga dhana hii, hujenga hoja kuwa Zanzibar itaweza kujenga mashirikiano yake yenyewe na dunia na nchi za kiarabu na kiislamu zenye uchumi imara. Wengine huzungumzia Zanzibar kuja kuwa bandari huru kama ilivyo Singapore. Tanganyika au Muungano huonekana kuwa ni kikwazo kwa Zanzibar kujiunga na Jumuiya ya Nchi za Kiislamu (OIC). Tunazidi kuaminishwa kuwa kwa kujiunga OIC, Zanzibar itajikwamua na umasikini.
Waumini wa Tanganyika wanatuaminisha kwamba nje ya Muungano, Tanganyika itakuwa imetua mzigo. Hawa wanataka tuamini kuwa Zanzibar inaielemea Tanganyika na kwamba gharama za kuendesha muungano zingeliweza kutumika kwenye miradi ya maendeleo. Wanatuaminisha kuwa Tanganyika imekuwa ikibeba gharama hizi peke yake na kwamba Tanganyika itaendelea kwa kasi sana baada ya kuachana na Zanzibar.
Dhana hii kuwa Zanzibar itanufaika nje ya Muungano ni dhana muflisi na potofu. Hoja ya kuwa kwa kujiunga na OIC Zanzibar itaneemeka ni ya kusadikika. Visiwa vya Comoro vina ukubwa wa kilometa za mraba 2170, vina idadi ya watu wapatao 984,500 na ni mwanachama wa OIC na Jumuiya ya Kiarabu (Arab League).  Visiwa vya Comoro vingali masikini kuliko Zanzibar na ukuaji wake wa uchumi kwa mwaka 2012 ulikuwa ni asilimia 2.7. Tunachokipata hapa ni kuwa sio OIC wala Arab League yenyewe inayoweza kubadili uchumi na maisha ya mzanzibari.
Uchumi wa Zanzibar kama ilivyo Comoro kwa muda mrefu umefifishwa na migogoro ya kisiasa. Zanzibar ina tabaka kubwa la wanasiasa na utawala kuliko uwezo wa uchumi kuhimili, hivyo migogoro ya kisiasa haiepukiki. Nje ya Muungano, wanasiasa wengi wa Zanzibar watakosa ajira, hawa watajiunga na siasa za ndani za Zanzibar, hapatatosha. Migogoro ya kisiasa baina ya visiwa huko Comoro ina athari kubwa kiuchumi kuliko migogoro ya kisiasa baina ya Unguja na Pemba kutokana na siasa hizo kumezwa na siasa za Muungano.
Isitoshe, nje ya Muungano, Tanganyika na Zanzibar zote kwa pamoja zitalazimika kubeba mzigo wa kugharamia ulinzi na usalama pamoja na uendeshaji wa Ofisi za Balozi nje ya nchi. Gharama hizi zikigawanywa kwa kila nchi kuendesha mambo haya yenyewe ni kubwa kwa kila nchi. Pengine tunapofushwa na gharama za kifedha pekee na kuacha kuangalia gharama za kiusalama. Usalama wa Zanzibar na Tanganyika unategemeana sana na Muungano ni chombo muhimu cha kuhakikisha usalama wa pande zote mbili. Tanganyika itagharimika sana kiusalama nje ya Muungano kuliko tunavyofikiria, hususan katika kipindi ambacho Tanganyika inatarajia kuvuna gesi katika pwani ya bahari ya Hindi. Mahasimu wa Tanganyika watakuwa wamepata upenyo mzuri wa kutimiza azma yao ya kuidhuru Tanganyika, au mahasimu wa Zanzibar kuidhuru Zanzibar. Hivyo, ustawi wa Zanzibar na Tanganyika unategemeana, wala sio kweli kuwa yuko mmoja anayembeba mwenzake au atakayekuwa salama zaidi nje ya Muungano.
 
4)        Wananchi wengi wa Zanzibar hawataki Muungano na Wananchi wengi wa Tanganyika hawataki Muungano
Wanasiasa wetu wa pande mbili wasioupenda Muungano kwa sababu wanazozijua wao, wanatuaminisha kwamba Muungano umechokwa na Watanzania wa pande zote mbili.  Wanasiasa hawa hawa walifanikiwa kutushawishi kuwa Watanzania wengi wanataka Katiba mpya. Takwimu ya waliojitokeza mbele ya Tume kutoa maoni juu ya Katiba mpya ni za kushtua. Katika nchi ya wapiga kura wanaokadiriwa kufikia milioni 20 kwa mujibu wa Tume ya Uchaguzi, waliojitokeza kutoa maoni yao hawakufika laki tano. Aidha, mwamko mdogo ulioonyeshwa katika ushiriki wa mabaraza ya Katiba unaacha maswali mengi.
Wanasiasa na wanaharakati hutumia shinikizo kama mojawapo ya nyenzo kufikia malengo yao. Mojawapo ya nyenzo wanayoipenda sana ni kutumia umma kuhalalisha matakwa yao. Kwa sababu hiyo haishangazi kwa wanasiasa kupenda kutumia njia ya maandamano na lugha ya ‘wingi’ katika kujenga hoja zao. Kwa mbinu hii, lugha ya ‘wingi’ imetumika kutuaminisha kwamba wazanzibari wengi hawautaki muungano, hali kadhalika, watanganyika wengi hawautaki muungano.
Lugha ya jumla imetumika pia kujenga dhana kuwa wanachama wa CUF wote hawaupendi muungano, wapemba wote ni CUF na waunguja wote ni CCM na wanaupenda Muungano tena wa Serikali mbili. Hali kadhalika, tunaaminishwa kuwa wanachama wa CHADEMA wote wanapenda Serikali tatu na wana CCM wanapenda Serikali mbili. Katika kunogesha dhana yenyewe, inajengwa hoja kwamba, iwapo kura ya maoni ya kutaka au kutotaka muungano itapigwa, basi haitapatikana theluthi mbili Zanzibar, kwa kuwa katika matokeo ya uchaguzi uliopita, hakuna chama kilichopata theluthi mbili ya kura.
Wanaoshabikia dhana hii wanawachukulia wananchi kama misukule. Wanaamini wananchi watapiga kura kwa mlinganyo ule ule hata kama jambo ambalo wanalolipigia kura limebadilika. Kwa kutumia dhana hii, tunakatishwa tamaa ya kuutafuta ukweli kwa kuwapa fursa wananchi ya kuchagua iwapo wanautaka muungano au hawautaki, wanataka Serikali mbili au tatu. Hata Tume ya Katiba imetuingiza katika mkenge huu kwa kutuambia kuwa ‘wengi’ waliohojiwa wametaka Serikali tatu. Hatujaambiwa waliotaka serikali mbili wangapi na waliotaka moja wangapi. Tunatakiwa tukubaliane tu kuwa wengi hawautaki muungano pande zote mbili.
Dhana hii haiakisi hali halisi. Wazanzibari na Watanganyika wameoleana, kuzaliana na wengine wanaendesha biashara kwa ubia. Ukisikiliza Sauti ya Radio Zanzibar katika taarifa za vifo utastaajabu kuwa karibu kila msiba una ndugu na jamaa bara tena sio Dar es Salaam pekee. Ukikaa katika bandari ya Dar es Salaam au Zanzibar utashangazwa na idadi ya wasafiri kutoka pande zote mbili za mbili za Muungano. Wananchi wa kawaida wa pande zote mbili hawana tatizo na muungano maana hauathiri maisha yao ya kila siku zaidi ya kuyarahisisha. Hawa, haswa wafanyabiashara, wanazo kero zinazohusiana na mifumo ya kodi zaidi kuliko muundo wa muungano, au muungano wenyewe. Hapana shaka, watakapoulizwa juu ya uwepo au kutokuwepo kwa muungano, maamuzi yao yatakuwa tofauti, kwa kuwa hatma ya muungano ina athari kubwa sana kwao. Ni vyema tukaruhusu kura ya maoni juu ya uwepo au kutokuwepo kwa muungano. Kura hii ya maoni, itatukwamua kutoka kwenye tope la wanasiasa, ambao ndio kero kuu ya muungano.
5)        Muungano umepitwa na wakati
Waswahili husema, ukitaka kumuua mbwa mpe jina baya. Ukimuita Mbwa Koko au Kichaa unapata uhalali wa kumuua. Ukimpa jina zuri unamuhamishia sebuleni. Katika kutimiza azma yao, wale wasioupenda Muungano hutoa dhana ya Muungano kupitwa na wakati. Kwao suala la Muungano huchukuliwa kama tukio la kupita na sio suala la kudumu. Hivyo, tunatakiwa tuamini kuwa muungano wetu umepitwa na wakati, na ulikuwa na mantiki tu wakati ule wa vita baridi na umajumui wa Afrika (Pan-Africanism). Zama hizo zimepita na hivyo Muungano nao umepitwa na wakati.
Hoja hii nayo inajibika. Muungano wowote unaingiwa kwa lengo la kuwa Muungano wa kudumu. Chini ya Sheria za Kimataifa, uko msingi kuwa nchi huingia Mkataba kwa dhamira njema ya kuutekeleza.  Hivyo, Muungano wetu kama ilivyo miungano mingine ikiwemo ule wa Marekani na Ujerumani, inadhamiriwa kuwa ya kudumu.
Tukirudi kwenye hoja yenyewe, Muungano wetu haujapitwa na wakati, labda baadhi ya viongozi wetu wamepitwa na wakati. Taifa letu linapita katika dunia ya utandawazi. Katika dunia ya utandawazi, nchi zinachukuliwa kuwa ni masoko. Muelekeo wa dunia ni kuunganisha nchi kuelekea kwenye utaifa mkubwa zaidi na na sio kinyuke chake. Nchi ndogo zina nafasi finyu katika dunia ya utandawazi hususan pale nchi zenyewe ndogo zinapokuwa masikini. Nchi za Ulaya zinafanyia kazi wazo la kuungana kuwa nchi moja chini ya Umoja wa Ulaya. Nchi ya Ubeligiji yenye pato kubwa la uchumi kuliko jumla ya nchi zote kusini mwa jangwa la Sahara inajiunga na nchi nyingine za Ulaya kujenga utaifa mkubwa kukabiliana na utandawazi. Aidha, tunaona jinsi ambavyo nchi zenye watu wengi kama India, China na Brazil zinavyotikisa katika utandawazi kutokana na kuwa na idadi kubwa ya watu. Ni kichekesho kuwa sisi nchi masikini tunafanya kinyume chake. Tunadanganyana kuwa tunayo fursa ya kuneemeka zaidi katika utandawazi tunapokuwa nje ya Muungano. Ukweli ni kuwa hatujiimarishi kwa kuwa nje ya Muungano bali tunajidhoofisha. Muungano unahitajika zaidi katika dunia ya utandawazi kuliko tunavyojifariji.
6)        “Sisi” ni Muhimu Kuliko “Wao”
Tunalo tatizo la kimtazamo miongoni mwa watanganyika na wazanzibari ambalo kwa maoni yangu msingi wake ni ubaguzi. Iko dhana ya ‘sisi’ na ‘wao’. Wananchi wa kila upande wamepandikizwa mitazamo dhidi ya wenzao wa upande mwingine. Baadhi ya Wabara huwaona wazanzibari kama watu goigoi na huwaita ‘yakhe’ au ‘mdebwedo’. Hali kadhalika baadhi ya wazanzibari huwaona wabara kama watu wa shamba na wasio staarabika, huwaita ‘machogo’. Mitazamo hii imeathiri kwa kiasi kikubwa mahusiano baina ya wananchi wetu, lakini baya zaidi, imetulewesha kwa kutupa majivuno kuwa ‘sisi’ ni bora kuliko ‘wao’.
Athari kubwa itokanayo ni mitazamo hiyo ni kujenga kutokuaminiana. Wabara wanadhani wazanzibari wote ni wazembe, hawana uwezo wa kiakili. Wazanzibari hali kadhalika wanawaona wabara kama watu wasiostaarabika, wenye majivuno na kupenda kuburuza. Matokeo yake, mitazamo hii huambukiza vizazi na vizazi.
Wananchi wa Zanzibari na Tanganyika waliopata bahati ya ama kuishi au kusoma na wenzao wa upande wa pili, watakubaliana nami kuwa mitazamo hii ni potofu. Binafsi, nimesoma na wazanzibari na kufanya kazi na wazanzibari wenye uwezo mkubwa sana kushinda wabara. Kama ilivyo kwa wabara, tunao wazanzibari wengi nje ya nchi kwenye mashirika ya kimataifa wanaotujengea heshima kubwa.
Changamoto ya kimfumo iliyopo ni kwamba, kutokana na wingi wa wabara, wengi wao hujikuta hawajawahi kufika wala kuishi Zanzibar, Isitoshe, hawajawahi kusoma ama kuishi na wazanzibari. Hivyo, wanasiasa hutumia mwanya huo kupandikiza mitazamo ya ‘sisi’ na ‘wao’ katika kutafuta kujijenga kisiasa. Maoni yangu ni kuwa, ‘sisi’ sio bora kuliko ‘wao’, wala ‘wao’ sio bora kushinda ‘sisi’. Wazanzibari, kama walivyo watanganyika wamelifia taifa letu la Tanzania katika kulinda na kutetea heshima na uhuru wake. Watanganyika na Wazanzibar wamekufa katika vita vya Uganda wakipigania taifa letu. Majuzi, watanganyika na mzanzibari wamekufa huko Darfur wakiwa katika shughuli za kulinda amani. Maadui waliowaua wanajeshi wetu kule Darfur hawakutofautisha mzanzibari wala mbara, waliua wanajeshi wa Tanzania katika jeshi la kulinda amani la Umoja wa Mataifa. Haya yanayotuunganisha, ni muhimu zaidi, kuliko yale yanayotugawa.
 Mwalimu Nyerere katika hotuba yake ya ‘Nyufa’ aliyoitoa 1995 alionya juu ya dhana hii ya ‘sisi’ na ‘wao’. Katika hotuba ile, alikumbusha kuwa kinatochufanya tuwe ‘sisi’ ni kutokana na ‘wao’ kuwepo. Akaonya, Ikiwa ‘wao’ hawapo, basi hata ‘sisi’ hatupo. Sote kwa pamoja ni bora zaidi kuliko ‘sisi’ au ‘wao’.
 
7)        Kero za Muungano lazima Zipate Majawabu ya Kudumu na Ziondoke, Manung’uniko ni kufeli kwa Muungano
 
Muungano wetu wa miaka 49 unazo changamoto zake. Changamoto hizi zimebatizwa jina la ‘kero’. Sidhani kama ‘kero’ ni neno sahihi, na nachelea kama neno ‘kero’ lilizuka tu pasipo kuwa na lengo nyuma yake. Kwa vyovyote vile, aliyezibatiza changamoto za muungano jina la ‘kero’ amefanikiwa sana. Sisi wengine huamini ‘maneno huumba’. Jina hili limeshakubalika na sasa changamoto zinaitwa ‘kero’, yaani mambo yanayokera.
Dhana tunayoipata hapa ni kuwa utatuzi wa ‘kero’ ni tofauti na utatuzi wa changamoto. Tofauti yenyewe ni ya kimtazamo. Changamoto ni vikwazo vya kutatulika, wakati kero ni vikwazo vilivyoshindikana. Kero zinapaswa kuondoshwa zote, na kama haziondoshwi, basi huwa ni sugu, na dawa yake ni kuvunja muungano wenyewe. Tunaaminishwa kuwa sio sahihi kuishi na kero kama hazitatuliki, na kuwa, muungano uliojaa kero ni muungano mfu. Kero hizi hudaiwa kwamba zinatokana na muundo wa muungano wenyewe. Suluhisho linalotolewa ni aidha kuwa na serikali tatu ili ‘kuunusuru’ muungano, kinyume na hivyo, ni muungano kuvunjika.
Tunadanganywa kuwa tunachojaribu kunusuru ni 'muungano'. Tunachotakiwa kunusuru ni 'utaifa' sio 'muungano', muungano ndio wenye kunusuru utaifa wetu, sio kinyume chake. Muungano wetu ni muungano unaoishi. Muungano unaoishi hupita katika nyakati na mazingira tofauti ya kisiasa, kiuchumi na kijamii katika maisha yake. Watu hubadilika, matarajio hubadilika na hali kadhalika mitazamo hubadilika. Changamoto za muungano ni kielelezo cha uhai wa muungano wenyewe na sio vinginevyo. Wala hakuna muungano duniani usio kuwa na changamoto, wenye kufurahisha watu wote, wakati wote. Changamoto za muungano ni fursa ya kuuimarisha muungano na sio kuuvunja. Huko tuendako tutarajie kujitokeza kwa changamoto nyingine hata tutakapofanikiwa kuzikabili zilizopo leo. Hivyo, dhana ya kuona changamoto za muungano ni kero na maana yake ni kufeli kwa muungano ni dhana potofu.
 
Changamoto za muungano ni kipimo cha uongozi. Changamoto hujitokeza ili zitatuliwe. Zisipotatuliwa ni udhaifu wa kiuongozi. Sina budi hapa kuwapongeza viongozi waliotangulia kwa kukabiliana na Changamoto hizi kila zilipoibuka. Uhodari wao ndio unaoufanya muungano wetu leo utimize miaka 49 na kuwa muungano pekee ulioweza kudumu katika Afrika. Kwa uongozi wao tumevuka jaribio la kuvunja muungano mwaka 1984, ambapo Mhe. Seif Sharrif Hamad, wakati ule alionyesha uzalendo wa kutukuka kulinda muungano wetu wa Serikali mbili (leo kageuka). Aidha tumevuka jaribio la kuvunjika kwa Muungano mwaka 1992-93 kufuatia Zanzibar kujiunga na OIC na Wabunge 55 wa Tanzania (G55) kudai Serikali ya Tanganyika. Tukavuka pia majaribio kadhaa kama hayo ndani ya mfumo wa vyama vingi hadi sasa.

Katika kitabu cha Uongozi Wetu na Hatma ya Tanzania, Mwalimu Nyerere alisema, “Maadamu matatizo halisi ya muungano hayazungumzwi wala hayashughulikiwi, watu wenye nia mbaya, wa bara na visiwani, wanaopenda kutumia hali hiyo kuivunja nchi yetu wanaendelea kufanya hivyo. Na wale wa huku na huku, wanachocheana kama mifukuto ya shetani. Na hiyo inawafanya hata watu wasio na nia mbaya, ila kwa ujinga tu, waamini kuwa inafaa wote tushiriki na tujiandae kuivunja Tanzania tusije tukashtukia kuwa Tanzania imevunjika na tumeachwa kwenye mataa! Anayedhani viongozi wetu ni wajinga yafaa achunguze akili zake! Wanajua wafanyalo”
Changamoto nyingi za Muungano zinaweza kutatuliwa chini ya muundo wa Serikali mbili kama ambavyo tumefanikiwa siku zote. Pengine, kilichotakiwa ni ubunifu tu wa mfumo mpya ya kutatua kero hizo kutokana na mifumo ya zamani kupitwa na wakati. Katika hili, ninayo kila sababu ya kumpongeza Mheshimiwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete na Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Mohamed Ally Shein kwa ubunifu wao. Nahodha mzuri hupimwa kwa uwezo wake wa kuhihimili chombo wakati wa dhoruba sio kukiendesha chombo wakati wa utulivu wa bahari. Chini ya uongozi wao, umeanzishwa mfumo rasmi wa kukutanisha Serikali ya Muungano na Serikali ya Zanzibar chini ya uenyekiti wa Makamu wa Rais kushughulikia changamoto hizo. Tangu kuanza kwa mfumo huo, changamoto 13 zimeshajadiliwa, changamoto 6 zimeshapatiwa ufumbuzi, hoja tatu ziko katika hatua za mwisho za kutatuliwa na hoja nne zinaendeea kushughulikiwa. Tokea mwaka 2011 hadi Aprili 2013, vikao 9 baina ya Serikali mbili vimekaa katika ngazi ya makatibu wakuu na mawaziri.
Kilicho dhahiri ni kuwa, changamoto nyingi zilitokana na viongozi wa pande mbili kutokutana rasmi. Kutokana na kuzoeana, mambo mengi yalikuwa yakimalizwa kwa mazungumzo baina ya viongozi wa ngazi za juu. Tatizo la utaratibu huo wa kindugu, ni kushindwa kupima ufanisi na kukosekana kwa mrejesho katika ngazi za chini ukiacha viongozi. Aidha, wakati mwingine kwa sababu za kisiasa, viongozi walipenda kuhodhi mchakato huu na taarifa zake. Pamoja na kwamba mfumo huo umetuvusha huko nyuma, kilicho wazi ni kuwa sio mfumo endelevu. Yawezekana ulifanya kazi vizuri chini ya mfumo wa Chama kimoja, lakini mazingira ya vyama vingi yanahitaji kurasimisha mfumo huu ili kuwezesha wadau wote wa muungano ndani na nje ya Serikali kupata mrejesho, na ikiwezekana kushirikishwa. Kinachostaajabisha, hili halizungumzwi, kinachozungumzwa ni muundo tu. Baadhi ya wanasiasa wamechagua kutoyazungumzia haya hadharani kwa kuwa yanakinzana na lengo lao la kuvunja muungano. Busara na umakini unatutaka kusikiliza tu sio kile tunachoambiwa, bali pia na kile tusichoambiwa na huyo anayetuambia
8)        Muungano wetu ni Batili na hauna Uhalali, ni wa Ajabu
Wanasheria nao hawako nyuma katika mjadala wa muungano na hatma yake. Baadhi ya Wanasheria wamehoji juu ya uhalali wa muungano kisheria. Wamekwepa siku zote kujadili uhalali wa muungano kisiasa kwa kujificha katika kile kinachoitwa uweledi. Mtazamo wa baadhi ya wanasheria umejikita katika kuangalia mchakato uliozaa hati ya muungano na matokeo ya mkataba huo. Mtazamo huo unachagiza dhana kuwa muungano wetu ni batili. Ubatili huo unatokana na kukosekana unyoofu katika mtiririko wa matukio katika kuelekea kufikiwa kwa Mkataba wa Muungano. Aidha, muungano wetu kutokufanana na miungano iliyoko kwenye vitabu vya kisheria kunawakwaza wanasheria. Maana, miungano iliyoko vitabuni ni mfumo wa muungano wa Serikali moja  au mfumo wa majimbo wenye serikali kadhaa za majimbo na moja ya muungano.
 
Wanasheria wengi wana matatizo makubwa ya aina mbili; kwanza wanajiamini kuwa wanajua (wanajiita kimombo ‘learnerd’); pili, jamii nayo imetokea kuamini  kuwa wanasheria wanajua. Wanasheria hawa hupenda kuwa na kauli ya mwisho kwenye kila jambo, na hawapendi kukosolewa na mtu asiye mwanasheria. Kinyume na mtazamo huo wa wanasheria, Muungano ni suala la dhamira kwanza, sheria baadae. Muungano hauanzi na sheria bali huhitimishwa na sheria, wala sheria pekee haibatilishi dhamira ya watu kuungana. Sheria yaweza kufa dhamira ikabaki. Watu ama nchi haziungani kwa lengo la kutekeleza sheria, bali wanaungana kwa malengo ya  kupanua maslahi ya kiuchumi au ya kiusalama au ya ustawi. Sheria na Katiba zinatumika kulinda dhamira hiyo sio kuiumba. Hivyo, Hati ya Muungano sio lengo, Hati ya Muungano ni matokeo. Hivyo, muungano wetu, na muundo wake wa Serikali mbili haulazimiki kukidhi au kufanana na miungano mingine kwenye vitabu, maana kila muungano huibuka katika nyakati, mazingira na malengo tofuti.
Ufafanuzi mzuri juu ya dhana ya uhalali wa Muungano imezungumziwa na Mwalimu Nyerere katika kitabu chake cha Uongozi wetu na Hatma ya Tanzania. Bahati, mbaya Hayati Abeid Karume, hakuishi muda mrefu kuweza kuacha maandiko, hivyo rejea kuhusu chimbuko la muungano zimetawaliwa na kauli za Mwalimu Nyerere. Katika kitabu hicho, Mwalimu Nyerere alisema, “Tanzania ni lulu ya pekee kabisa katika historia ya Afrika huru. Nchi nyingine zote ni za kurithi kutoka kwa wakoloni. Wako watanzania wa ajabu kabisa wanaosema kuwa uamuzi huo, au vyombo vilivyotumiwa au njia iliyotumiwa, au vyote, havikuwa halali. Hao hawana shaka na uhalali wa Tanganyika, ambayo iliunganishwa na Wajerumani, na ikamegwa megwa na Waingereza na wenzao. Kwa hao, kama Rwanda na Burundi na Tanganyika zisingetengwa na mabeberu, tukazirithi kama zilivyokuwa chini ya Wajerumani, wasingeushuku uhalali wa nchi moja hiyo. Lakini kama baada ya uhuru, Rwanda na Burundi na Tanganyika zingeamua kuungana ziwe nchi moja, kwa utaratibu wowote ambao zingekubaliana, ‘wazalendo’ hawa wangesema muungano huo sio halali.”
Katika aya inayofuatia, Mwalimu Nyerere akaendelea kujenga hoja juu ya mtiririko wa matukio uliopelekea kufikiwa kwa makubaliano ya nchi zetu kuungana. Alisema, “Hatukutafuta maoni ya watu kwa njia ya demokrasia wanayoijua wao. Wajerumani na Waingereza walitafuta maoni ya wazee wetu kwa mtutu wa bunduki! Hiyo ilikuwa halali. Nchi walizounda kwa njia hizo zilikuwa halali. Tunatakiwa tujivunie utanganyika na uzanzibari uliopatikana kwa njia hizo, lakini tuuonee haya Utanzania, tunda la uhuru wetu wenyewe. Sikuamini kama wakoloni walifaulu kiasi hiki katika kuzinywesha kasumba na kuzitawala akili za baadhi yetu!”
 
9)        Muungano na haswa Muundo wa Serikali Mbili ni Sera ya CCM
Suala la Muundo wa Serikali mbili limekuwa likihusishwa na CCM. Bahati mbaya, wana CCM nao wametokea kuamini kuwa suala hili ni Sera yao. Kuunasibisha muundo wa Serikali mbili na CCM kunafanya wale wengine wasiokubaliana na CCM kutokukubaliana pia kwenye suala la muundo wa Serikali mbili. Matokeo yake, suala la muundo wa Serikali mbili linapoteza sura ya utaifa, hivyo wanaopinga mfumo huo, wanaukataa wakati mwingine bila hata ya kuuelewa na kuuchambua. Ukiondoa CCM hakuna Chama chochote kingine cha siasa Tanzania kinachosimamia muundo wa Serikali mbili.
 
Muundo wa Serikali mbili kama zitakavyokuwa Serikali tatu au moja sio mwarobaini wa Muungano. Muundo wa Serikali mbili ulichaguliwa baada ya waasisi kujiridhisha kuwa katika mazingira ya tofauti za kimaumbile za Tanganyika na Zanzibar, ni muundo wa Serikali mbili tu ndio ungeweza kukidhi hitaji la unafuu wa gharama za uendeshaji na kinga dhidi ya hatari ya utaifa wa mzanzibari kutoweka. Si muundo wa Serikali mbili wala tatu ambao ulionyesha kuleta msawazo katika mahitaji hayo mawili wakati huo na hata sasa. Hoja ya kuwa muundo huu ni wa CCM kwa kuwa ulifikiwa chini ya vyama vya TANU na ASP ambavyo viliungana na kuzaa CCM ni hoja muflisi. TANU na ASP ndio vyama vilivyokuwa madarakani wakati huo, na mrithi wao CCM kiko madarakani hadi sasa. Ukweli huu haufanyi muundo huu kuwa wa CCM. Suala la Muundo lafaa kuwa suala la Kikatiba ili vyama vyote viuheshimu.
 
Muundo wa Serikali mbili unalo chimbuko lake. Haukutokana na nasibu bali tathmini na maamuzi yenye upeo wa hali ya juu. Mfumo wa Serikali mbili waweza usiwe mfumo bora kushinda mingine duniani, lakini ni bora kushinda mfumo wa Serikali tatu na moja katika mazingira ya Tanzania. Hili pia limezungumziwa na Mwalimu Nyerere kwenye kitabu chake cha Uongozi wetu na Hatma ya Tanganyika, alisema:
 
Tanganyika na Zanzibar zilipoamua kuungana na kuwa nchi moja, tungeweza kufuata mojawapo ya mifumo ya kawaida. Lakini tulishindwa kufanya hivyo kwa sababu ya udogo wa Zanzibar na ukubwa wa Tanganyika. Zanzibar ilikuwa na watu laki tatu (300,000) na Tanganyika watu milioni kumi na mbili (12,000,000). Muungano wa Serikali moja ungefanya ionekane kama Tanganyika imeimeza Zanzibar. Tulikuwa tunapigania uhuru na Umoja wa Afrika, hatukutaka tudhaniwe hata kwa makosa kwamba tunaanzisha ubeberu. Kwa hiyo mimi nilipinga mfumo wa Serikali moja. Shirikisho la Serikali Tatu lingekuwa ni gharama kubwa mno kwa Tanganyika. Zanzibar ingeendesha Serikali yake na kuchangia gharama za kuendesha Serikali ya Shirikisho; na Tanganyika ingefanya hivyo hivyo. Lakini ni dhahiri kwamba mchango wa Tanganyika ndio hasa ungeendesha Serikali ya shirikisho. Kwa hiyo, Tanganyika ingeendesha Serikali ya watu milioni 12 na pia ingetoa sehemu kubwa ya kuendesha Serikali ya Shirikisho la watu milioni 12,300,000. Ni watu wanaofikiri kwa ndimi zao wanaodhani kuwa gharama ya Serikali yoyote kati ya hizi ingekuwa ndogo. Gharama ya Serikali ya Tanganyika isingekuwa ndogo, hata bila ya gharama za mambo yasiyo ya Shirikisho. Na gharama zote hizo kwa kweli zingebebwa na Tanganyika. Kwa hiyo ilitupasa tujiulize kwa nini tunataka kuibebesha Tanganyika gharama zote hizo; na hasa kwa nini tunataka Serikali ya Tanganyika? Hivi tuna hofu ya kwamba Tanganyika, bila kuwa na Serikali yake, itaonekana imemezwa na Zanzibar? Hofu yetu ni kwamba tukiwa na Serikali moja Tanganyika itaonekana kuwa imeimeza Zanzibar. Basi na tutafute mfumo ambao utaiondolea Zanzibar hofu hii ya kumezwa bila kuibebesha Tanganyika mzigowa kuendesha Serikali mbili zenye uzito unaolingana. Hivyo ndivyo tulivyofanya, na hiyo ndio asili ya muundo wa Muungano wa serikali mbili. Badala ya kutungua mfumo uliopo kama wapumbavu, tulitazamia hali halisi yetu ilivyokuwa, na tukabuni mfumo uliotufaa zaidi".
 
Tukienda na maelezo hapo juu, lililo dhahiri ni kuwa, zipo sababu kwa nini muundo wa Serikali mbili ulibuniwa. Aidha, katika maelezo hayo, kilicho wazi ni kuwa sababu zilizozaa Serikali mbili hazikuwa sababu za kichama bali kitaifa. Hivyo, dhana kuwa muundo wa Serikali mbili ni suala la CCM ni dhana potofu. Hali kadhalika, muundo huu sio msahafu na unaweza kubadilika. Wala hakuna sababu ya kuendekeza muundo ambao hautakiwi. Muhimu ni kujadili kwa uwazi iwapo mazingira yaliyozaa Serikali mbili yamebadilika, na kama kwa kubadilika huko, sasa mbadala wake ni Serikali moja, tatu au kuvunja muungano.
 
 
10)    Kuvunja Muungano ni sawa na kuvua koti
 
Baadhi ya wanasiasa wanazungumzia suala la kuvunja muungano kwa wepesi sana. Suala la kuvunja muungano linachukuliwa kama jambo la usiku mmoja. Dhana hii inajengwa kwa makusudi ya kuwatoa hofu wananchi kwamba hakutakuwa na athari ikiwa tutafanya hivyo. Wanapozungumzia suala la kuvunjika kwa muungano, hutanguliza picha ya ‘pepo nzuri’ itakayokuja punde baada ya kuuvunja. Katika kurahisisha hoja yenyewe, inasemwa kuwa ‘muungano ni kama koti, ukilichoka unalivua’.
 
Funzo tunalolipata katika maisha ya kawaida na uzoefu kutoka nchi zilizopita njia tunayoshawishiana kupita, zinatufunza vinginevyo. Kuvunjika kwa ndoa tu huambatana na changamoto nyingi na wakati mwingine kusambaratika kwa familia na mali. Uzoefu wa kusambaratika kwa dola ya kisovieti ya Urusi na dola ya Yugoslavia kuliambatana na machafuko. Aidha, kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki mwaka 1977, pamoja na kuwa ulikuwa ni ushirikiano wa kikanda tu, uliambatana na ukakasi mkubwa. Hivyo, hatuna sababu yoyote ya kuamini kuwa kuvunjika kwa muungano wa Tanganyika na Zanzibar uliodumu kwa miaka 49 litakuwa ni jambo jepesi na rahisi.
 
Msingi wa kuvunja muungano ni dhamira zinazosukumwa na kutoaminiana na chuki miongoni mwa wanasiasa na baadhi ya wananchi. Hatuwezi kutarajia matokeo ya kuvunjika kwa muungano huo yazae upendo na mashirikiano. Upo uwezekano mkubwa wa wazanzibari walioko Tanganyika na watanganyika walioko Zanzibar kupita katika msukosuko mkubwa. Msukosuko huu waweza kuhatarisha usalama wa maisha na mali zao. Tayari vipo viashiria vya biashara za wabara kuchomwa moto na watu wasiojulikana Zanzibar. Njia hii, haitaweza kuzaa mazingira ya mashirikiano nje ya muungano. Hili likitokea, ustawi wa nchi mbili hizi utakuwa mashakani ikizingatiwa kuwa usalama wa nchi hizi mbili unategemeana.
 
Jambo la kuhofia zaidi iwapo muungano utavunjika ni kuendelea kuwepo kwa Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Zanzibar. Sina mashaka kuwa, hoja zilezile zilizofanikisha kuvunja muungano ndizo zitakazovunja jamhuri hizi mbili. Ni vigumu kuweka ukomo wa kutumika kwa hoja za mgawanyiko, ilihali watu watakuwa wamedhihirisha kuwa zinafanya kazi vizuri. Sioni ni kwa sababu gani maeneo mengine yasitake kujitenga kwa kujificha katika Sera ya Majimbo hususan kule zinakotoka rasilimali kama Mtwara, kanda ya Ziwa na Kanda ya Kaskazini. Nao watahoji uhalali wa Tanganyika na watasema ‘utaifa ni kama koti, likikubana unalivua’.
 
Ni hofu yangu kuwa Zanzibar nayo haitabaki moja. Mgawanyiko wa kisiasa kati ya kisiwa cha Unguja na Pemba, na waunguja na wapemba ni dhahiri. Chaguzi za Zanzibar kabla ya mapinduzi na baada ya mapinduzi zimeambatana na mgawanyiko mkubwa. Katika chaguzi mbili za mwaka 2000 na 2010, Chama cha Mapinduzi kinachoaminika kuungwa mkono na waunguja wengi hakikupata kiti hata kimoja cha Ubunge na Uwakilishi kisiwani Pemba. Ni vyema kukumbuka kuwa, uwepo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar hakujamaliza tofauti za wapemba na waunguja. Kikundi cha Wazee wa Pemba kilichoandika barua Umoja wa Mataifa kikitaka Pemba kujitenga hakijafa. Uamsho nao ni kikundi cha kukiangalia kwa makini sana. Mgawanyiko huu katika jamii ya wazanzibari ulijionyesha pia katika utoaji wa maoni ya Katiba mpya. 
 
Tukiangalia kijiografia na kiutawala, umbali kati ya Tanganyika na Unguja na Tanganyika na Pemba ni mdogo sana ukilinganisha na umbali kati ya Pemba na Unguja. Mazingira haya ya kijiografia, na fukuto la mgawanyiko ndani ya Zanzibar, yataipa changamoto kubwa sana Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kujitawala nje ya muungano. Mazingira haya yanatoa fursa nzuri sana kwa wasioitakia mema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kukamilisha azma yao ya kujitenga kwa Pemba. Gharama ya hili kwa wazanzibari na ustawi wao itakuwa kubwa sana. Mazingira haya, hayatavutia huo uwekezaji unaotumainiwa kutoka OIC wala uarabuni. Maana, ustawi hautokani na kuwa na rasilimali pekee, bali kuwepo kwa amani na utulivu. Hali kadhalika iwapo Zanzibar itaingia kwenye machafuko na kusambaratika, Tanganyika haitakuwa salama pia maana usalama wetu unategemeana.
 
 
Hitimisho
 
Hakuna siasa rahisi kama siasa ya kugawa watu na siasa ya kubomoa. Kuutetea muungano na haswa muundo wa Serikali mbili kunahitaji ujasiri na uongozi. Ujasiri na uongozi hukaa vifuani mwa viongozi makini. Wanasiasa makini huunganisha watu na ni jukumu gumu. Ndio maana haishangazi kuwa tuna wanasiasa wengi wanaohubiri mgawanyiko kuliko wanaohubiri umoja.
 
Ukweli unabaki, kutokuendelea kwa Tanganyika au Zanzibar hakutokani na Muungano bali Muungano ni 'bangusilo' tu. Zanzibar imerudishwa nyuma na matatizo yanayotokana na historia yake kabla na baada ya mapinduzi. Vivyo hivyo Tanganyika imerudishwa nyuma na matatizo ya kiutawala ikiwemo ubadhirifu na ufisadi. Matatizo ya Tanzania bara na Zanzibar hayatokani  na muungano wala muundo wa Serikali mbili. Kinyume chake Muungano umeijengea Tanganyika na Zanzibar umoja na utaifa, umoja uliotuwezesha kukabili misukosuko ikiwemo vita dhidi ya Uganda. Tusijifiche nyuma ya Muungano, tutafute suluhu ya matatizo yetu ya ndani ya pande zote.
 
Suala la muungano na muundo wake lafaa kufafanuliwa na kujadiliwa kwa kina na uwazi. Ikiwa tutajiridhisha kuwa mazingira yetu yamebadilika kiasi cha kuhitaji muundo mwingine si vibaya tukaubadili. Ni vizuri tu kuwaeleza wananchi kinagaubaga kuwa, kama ambavyo muundo wa serikali mbili unawagharimu, mabadiliko kwenda katika mfumo wowote tutakaokubaliana yatakuwa na gharama zake pia, tena zaweza kuwa kubwa kuliko zilizopo. Ni vyema wananchi wakafahamishwa gharama hizo ili wawe tayari kufanya maamuzi sahihi na kuzibeba.
 
Swali tunalopaswa kujiuliza kwa dhati mioyoni mwetu ni kama tunataka muungano uendelee au la. Ikiwa tunautaka, Napata shida kuamini kuwa tunaweza kuuendeleza nje ya muundo wa Serikali mbili. Maoni yangu, upo uwezekano mkubwa kuwa nje ya muundo wa Serikali mbili, na ikiwa muungano utaendelea kuwepo hatutakuwa na serikali mbili, bali muundo wa serikali nne ambazo ni serikali za Tanganyika, Pemba, Unguja na Shirikisho. Maana ni vigumu kupangua mbili ukasimamia kwenye tatu. Kupangua ni rahisi kuliko kupanga, kubomoa ni rahisi kuliko kujenga.
 
Hatimaye, ustawi na hatma ya nchi yetu, muungano wetu na vyote vile tunavyovithamini viko mikononi mwetu. Wakati umefika, wanaoamini katika utaifa wa Tanzania wasimame na waseme  sasa au wanyamaze na kuishi na majuto milele! Mimi nimechagua kusema!

 

 

 

Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>