Na Himid Choko, BLW
Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar Ndugu Ibrahim Mzee Ibrahim amesema ni kosa la jinai kwa Afisa yeyote wa Umma kutoa majibu ya uongo kwa kamati za Baraza la Wawakilishi.
Amesema Kifungu cha 22 cha sheria ya Baraza la wawakilishi Nambari 4 ya mwaka 2007 inayohusu Kinga, uwezo na Fursa kinakataza mtu kuidanganya kamati ya Baraza la Wawakilishi na atakaethibitika kwa makusudi kutenda kosa hilo ataadhibiwa kwa mujibu wa sheria ya Makosa ya Jinai.
Ndugu Ibrahim amesema hayo leo wakati akitoa mada inayohusu Wajibu na utekelezaji wa Kazi za makatibu Kamati huko hoteli ya Coconut Tree Village, Marumbi Mkoa wa Kusini Unguja.
Amesema Kamati za Baraza la Wawakilishi zinauhalali wa Kikatiba na sheria hivyo si vyema kwa maafisa wa umma kutoa majibu au ushahidi wa uwongo kwa kamati hizo.
“ Ni haki ya Wajumbe wa kamati kupata taarifa wazitakazo kutoka kwa maaafisa wa umma (kifungu cha 9 Cha Sheria ) . Maafisa wa Umma hawatakiwi kukataa kutoa ushahidi , hawatakiwi kukataa kuwasilisha nyaraka kwenye kamati , hawatakiwi kukataa kuwasilisha taarifa kwenye Sekretarieti ya Baraza isipokuwa kama Rais ataelekeza vinginevyo kwa maslahi ya Umma”. Alifafanua Mkurugenzi huyo wa Mashtaka.
Mkurugenzi huyo wa Mashtaka pia ametanabahishwa kwamba ni kosa la jinai kumtisha, na kumuadhibu mtu aliyetoa ushahidi kwenye kamati .
Amesema, pia ni kosa kuidharau kamati kwa kukataa wito wa kutoa ushahidi au kutokuwa na nidhamu na kuzuwia shughuli za kamati hizo.
Amesema Kamati za Baraza la wawakilishi zinauwezo wa kumuita mtu yeyote kuhudhuria kwenye kamati na kutoa ushahidi ama nyaraka aliyonayo ikihitajika katika kazi zake na kwamba mtu huyo atakuwa na fursa na kinga kama zile anazokuwanazo shahidi anapotoa ushahidi mahakamani.
Hata hivyo amesema mtu anaweza kukataa kujibu maswali anayoulizwa au kuwasilisha nyaraka zinazohusu mambo binafsi ya mtu huyo ambayo hayataathiri uchunguzi unaofanywa na Kamati.
Wakati huo huo Mkurugenzi huyo wa mashtaka amesema ni kosa kwa mjumbe au Afisa wa Baraza kutoa au kupokea rushwa au kufanya vitendi visivyofaa kulingana na hadhi na itifaki zao.
Wakitoa uzowefu wao katika kazi za kamati za baraza , Wenyeviti wa kamati za Baraza la Wawakilishi wamesema hadhi ya Baraza inashuka kutokana na tatizo kubwa la utoro na Ucherewaji pamoja na kukosa uwajibikaji mzuri kwa baadhi ya wajumbe suala ambalo mara nyengine huathiri akidi katika vikao vya Baraza na kamati zake.
Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha , Biashara na Kilimo Mheshimiwa Salmin Awadh Salmin na Mwenyekiti wa Kamati ya Kusimamamia Ofisi za Viongozi Wakuu wa Kitaifa Mheshimiwa Hamza Hassan Juma wameuomba uongozi wa Ofisi ya Baraza la Wawakilishi kufikiria utaratibu wa malipo ya Wajumbe ili kudhibiti mahudhurio na utoro katika vikao vya Baraza na kamati zake.
Mapema akifungua mafunzo hayo Spika wa Baraza la Wawakilishi Mheshimiwa Pandu Kificho amewataka Makatibu wa Kamati kutoa huduma kwa usawa na kuwa wastahamilivu wakielewa kwamba wanawahudumia wajumbe wenye uzowefu, elimu na misimamo tofauti .
Amewataka Makatibu hao kuweka kumbu kumbu za Mikutano yao vizuri na kuwashauri vyema wenyeviti wao ili kuhakikisha kwamba kanuni za baraza la wawakilishi zinafuatwa ili shughuli za kamati hizo kufanyika kama zilivyokusudiwa.
Kamati za kudumu za Baraza la wawakilishi hivi sasa zinaendelea na kazi zake za kawaida tokea tarehe 10/07/2014 hadi tarehe 23/07/ 2014 hapa Unguja na Mkutano ujao wa Baraza unategemewa kufanyika Oktoba 22 mwaka huu.